Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Wadau wa habari wamesema, baada ya Bunge kupitisha marekebisho ya sheria ya habari, kinachofuata sasa ni kuomba fursa ya kukutana na serikali ili kupendekeza mambo gani yaingie kwenye kanuni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 17, 2023 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema kuwa wadau wa habari wangependa ukamilifu wa uundwaji wa kanuni za habari usivuke Oktoba mwaka huu.

Amesema kuwa miongoni mwa mambo ambayo wadau wa habari wangependa kuona yanaingia kwenye kanuni mpya na kuanza kutumika ni pamoja na suala la leseni ya magazeti kuwa zaidi ya miaka mitano tofauti na ilivyo sasa.

“Tunapenda ukamilifu wa uundwaji wa kanuni za habari usivuke Oktoba mwaka huu, pia tutashauri Serikali kanuni zielekeza kuwa kanuni mpya na kuanza kutumika ni pamoja na suala la leseni ya magazeti kuwa zaidi ya miaka mitano tofauti na ilivyo sasa na kitambulisho cha mwanahabari (press card), zidumu kwa zaidi ya miaka mitano,” amesema.

Ameongeza kuwa makosa ya kitaalumu yanapaswa kubaki kwa wanataaluma wenyewe, hili litasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.

Kwenye mkutano wake na wanahabari Balile amesema, eneo lingine wanalotarajia liingie kwenye kanuni, ni umiliki wa hisa katika vyombo vya habari kutowekewa mipaka.

Amesema, sio jambo rahisi kwa mwekezaji kutoka nje awekeze kwenye vyombo vya habari halafu asiwe na sauti, huku akitoa mfano wa uwekezaji wa bila kiwango cha asilimia katika maeneo mengine ikiwemo mitandao ya simu.

“Sheria inataka mwekezaji kutoka nje ya nchi amiliki hisa isiyozidi asilimia 49, jambo hili linapunguza uwekezaji kwenye vyombo vya habari.

“Tutamshauri Waziri wa Habari Nape Nnauye, kwamba, mwekezaji kwenye vyombo vya habari asiwe na ukomo kama ilivyo kwenye mitandao ya simu na maeneo mengine,” amesema Nape.

Pia amesema, miongoni mwa sehemu ya sheria ya sasa inaruhusu mwandishi wa habari kumshitaki mtoa taarifa endapo atakataa kutoa taarifa inayotakiwa na mwanahabari.

“Hili lieleweke vizuri, kuna maofisa wa serikali ambao wakitakiwa kutoa taarifa kwa wanahabari, wanagoma kufanya hivyo. Kwa sheria ya sasa, mwanahabari anaweza kumburuza mahakamani ofisa ambaye hatotoa taarifa inayotakiwa,” amesema Balile.

Balile amemshukuru Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Greyson Msigwa kwa kuingilia kati katika maeneo ambayo maofisa wa serikali walipotaka kunyanyasa wanahabari.

“Kuna maofisa wa serikali walitaka kuendeleza utamaduni wa kunyanyasa wanahabari. Jambo hili limekuwa likiwatesa wengi, lakini nimshukuru Msigwa maana amekuwa makini katika hili,” amesema.

“Ni kutokana na utaratibu wake wa kushirikisha wadau ndio maana anafanya hivyo, wala safari hii suala la kanuni za habari halipelekwi bungeni, linaishia kwa kwake Waziri Nape,” amesema.

Amesema, mwenye jukumu la kusimamia na kukamilika kwa kanuni ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.