TRA Chunya yajivunia sekta ya madini kwa ukusanyaji wa kodi

Na Richard Mrusha,JamhuriMedia

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imesema kuwa asilimia kubwa ya mapato katika Wilaya hiyo yanatokana na Madini ambapo wachimbaji wadogo wamekuwa na uelewa mpana juu ya kifaa kinachotumika katika kurahisisha ukusanyaji wa taarifa za raslimali hizo.

Kaimu Meneja wa TRA Wilayani Chunya Osmund Mbilinyi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na maonesho ya kwanza ya teknolojia ya madini wilayani humo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka hiyo Osmund Mbilinyi wakati akizungumza kwenye maonesho ya kwanza ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea kwenye viwanja vya Sinjiriri katika Mkoa wa Kimadini Chunya.

Amesema kuwa lengo kubwa la kuwapo kwenye eneo la maonesho ni kuhakikisha kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji pamoja na wateja wake wengine jambo ambalo hatua hiyo itakuwa imerahisisha kusambaa haraka zaidi kwa elimu hiyo juu yam lipa kodi.

“Wachimbaji wadogo ni wadau wetu muhimu pamoja na wanunuzi wa madini hayo na kwamba sekta hiyo ndiyo inayotuingizia pato kubwa serikalini pamoja na mambo mengine hasa hasa tunajikita kutoa elimu ya huduma za mlipa kodi kiganjani na watakuwa wanatumia huduma hiyo wao wenyewe pasipo kufuatwa na maafisa wa TRA,”amesema Mbilinyi.

Mbilinyi pia amesema kuwa TRA wapo katika kuboresha mfumo mpya wa mlipa kodi kiganjani ambao ataufanya mteja atafanya mwenyewe kila kitu, TRA itapitia kile alichokifanya mteja mwenyewe na kuongeza kuwa mbali na maonesho hayo pia TRA inao utaratibu wa kutoa elimu kila baada ya miezi mitatu kwa kuwafuata wafanyabiashara wa madini pamoja na wachimbaji wenyewe kwenye maeneo yao ya kazi.

Amesema kuwa Mkoa wa Kimadini Chunya una masoko ya Dhahabu zaidi 20 ya ununuzi wa Madini hayo na kwamba TRA inahakikisha inafikisha huduma karibu na wateja wake na kufafanua kuwa elimu inayotolewa ni kuanzia ukadiliaji, usajili,ujazaji wa litany pamoja na shughuli zote ambazo zinaihusu TRA kwa wateja wake hasa wa madini ambao ni muhimu sana.