Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

MAMLAKA ya mapato Tanzania Mkoa wa Dodoma(TRA) kupitia kampeni yake ya Tuwajibike imewashauri wafanyabiasha kuwa na mwamko na utamaduni wa kutoa risiti pindi wanapofanya mauzo ili kusaidia kuongeza mapato ya Serikali.

Hayo yameelezwa leo September 15,2023 Jijini hapa na Meneja wa TRA mkoa wa Dodoma Castro John wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa awamu ya pili wa kampeni ya Tuwajibike wenye lengo la kuwakumbusha wafanyabiasha kuwajibika katika kutoa risiti halali za EFD kila wanapofanya mauzo ya bidhaa au huduma.

Amesema Serikali inategemea mapato ya Kodi katika kujiendesha na kuboresha huduma za jamii hivyo ni muhimu kwa wanunuzi pia kudai risiti hizo na kuzikagua ili kujiridhisha uhalali wake ikiwemo kukidhi vigezo vyote muhimu kama tarehe na muda wa mauzo,jina la mnunuzi na gharama halisi hali itakayoepusha udanganyifu.

“Wafanyabiasha wanapaswa kuwajibika kutoa risiti halali bila kusubiri kushurutishwa ,tukifanya hivyo tunaisaidia Serikali kutumiza malengo ya kuwaletea Wananchi maendeleo na kukuza uchumi,nawasisitiza pia wafanyabiasha kufika kwenye Ofisi zetu kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yetu,”amesema

Akieleza kuhusu kampeni ya Tuwajibike amesema njia watakazotumia kufanikisha kutoa elimu kwa wauzaji na wanunuzi kwa mitaa yote ya Dodoma na Wilaya ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa utoaji risiti halali za EFD na kuwachukulia hatua wauzaji wasio fuata sheria.

“Kwa wasiotoa au kudai risiti watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwa kutozwa faini ambayo itakuwa kubwa kati ya shilingi milioni 1.5
au asilimia 20 ya thamani ya bidhaa iliyouzwa, kwa mnunuzi àsiyedai risiti atatozwa faini ambayo itakuwa kubwa kati ya shilingi 30,000 au asilimia 20 ya Kodi aliyokwepa,”amesema

Meneja huyo ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga maeneo yote ya biashara ambapo mkazo zaidi utawekwa Katika maeneo korofi ambayo ni usafirishaji wa vifurushi au vipeto vinavyikwenda mikoani Kwa kutumia usafiri wa mabasi na maroli na eneo la pili ni maeneo ya wauzaji wa jumla na maduka makubwa.

By Jamhuri