Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023 /24 imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shillingi Trilioni 6.63 sawa na ufanisi wa asilimia 95.17 ya lengo la kukusanya shillingi trilioni 6.97.

Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 11.68 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi trilioni 5.94 ya kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2022/23.

Akitoa taarifa ya hiyo Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, amesema kuwa katika mwezi machi 2024, TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi trilioni 2.49 sawa na ufanisi wa asilimia 97.05 katika lengo la kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 2.56.

Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 6.91 ukilinganisha na kiasi cha trilioni 2.32 kilichokusanywa mwezi kama huu katika mwaka wa fedha 2022/23.

Amefafanua kuwa mafanikio yaliofikiwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa  fedha 2023/24 yamechangiwa na kuongezeka kwa uhiari wa ulipaji kodi kufuatia maboresho yanayoendelea kufanywa ikiwemo kusogeza huduma jirani na walipa kodi kwa kuanza Divisheni za walipakodi wadogo na walipakodi wa kati pamoja na kuendelea kusuluhisha pigamizi za kodi nje ya mahakama.

Pia kuwa na mutikio mzuri wa walipakodi kuwasilisha kwa wakati ritani za kodi kwa mwaka 2024 kupitia mifumo ya Tehama ya Uwasilishaji wa Ritani.

Kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji na ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini zinazochangia mapato ikiwemo sekta za madini, taasisi za fedha ikiwemo mabenki, sekta ya utalii.

Kuongezeka kwa ufanisi kwenye huduma za forodha hususani katika kusimamia kodi zinazohusiana na uingizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi.

Amesema kuwa kuhakikisha lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2023/24 linafanikiwa TRA wananchi wanapaswa kuendelea kutoa taarifa juu ya vitendo vinayoashiria ukwepaji wa kodi nchini ikiwemo biashara za magendo na uuzwaji wa bidhaa ambazo hazijabandikwa stempu za kielektroniki (ETS).

“Ikumbukwe kukithiri kwa vitendo vya magendo haviathiri makusanyo ya Mapato ya Serikali pekee, bali vinahatarisha afya na usalama wa wananchi kwa bidhaa ya kuuzwa sokoni wakati wa hazina viwango vya ubora kwa matumizi ya binadamu” amesema Bw.Kidata.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kutoa risiti za kielektroniki (EFD) zenye viwango sahihi kila wanapouza bidhaa au kutoa huduma.

Amewashukuru walipakodi na watanzania kwa kuendelea kutoa ushirikiano wa kulipa kodi na kuthamini juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suruhu Hassani kuiletea nchi maendeleo.