Na Esther Mbussi, JamhuriMedia, Mbeya

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona, amesema moja ya malengo ya bodi hiyo kwa mwaka huu ni kuzalisha tani 60,000 kutoka tani 48,000 mwaka jana.

Kambona amesema hayo jijini Mbeya katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk.Moses Kusikula (kushoto), akipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona (kulia) katika banda la bodi hiyo wakati wa Maonesho Nanenane jijini Mbeya alipotembelea banda hilo. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvui, Profesa Riziki Shemdoe.

Amesema mwaka 2020 wakati TSB inapewa jukumu na serikali la kuhakikisha uzalishaji unapanda hadi kufikia tani 120,000 mwaka 2025, ilikuwa inazalisha tani 36,000 kwa mwaka na sasa hivi wamefunga mwaka jana kwa kuzalisha tani 48,000.

“Lengo letu ni kufikisha tani 60,000 na tayari hadi kufikia Juni, mwaka huu tulikuwa tumeshazalisha tani 34,000. Kwa hiyo tunajiona kabisa tutamaliza mwaka huu kwa kuzalisha tani 60,000 bila wasiwasi.

“Jitihada zimeshafanyika na serikali imeongeza bajeti ya maendeleo ya Bodi ya Mkonge kwa kuiwezesha kupata vyombo vya usafiri kwa ajili ya kushughulikia upatikanaji wa takwimu uliokuwa changamoto ndiyo maana utaona sasa hivi takwimu zimepanda sio kwamba mkonge haukuwapo lakini takwimu zilikuwa hazikusanywi ipasavyo, kimsingi mabadiliko ni makubwa,” amesema.

Akizungumzia takwimu za mapato amesema tangu serikali imechukua juhudi za kufufua mkonge mwaka 2019 na kutambulishwa kuwa zao la kimkakati mapato ya mauzo yake ya nje yameongezeka na yamefikia Dola milioni 56 za Marekani kutoka Dola milioni 42 kwa kipindi cha miaka miwili.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Gwakisa (kushoto), akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona katika banda la bodi hiyo kwenye Maonensho ya Nanenane jijini Mbeya alipotembelea banda hilo.

“Lakini mauzo ya ndani pia yaliongezeka kutoka Sh bilioni 41 hadi sasa Sh bilioni 43 kwa soko la ndani. Kwa hiyo soko la nje limefanya vizuri zaidi yaani mkonge mwingi umeuzwa zaidi nje kuliko ndani lakini takwimu zimepanda,” amesema.

Pia amesema wastani wa mauzo ya singa za mkonge (fiber) tani moja ni takribani Sh 3,500,000 kwa madaraja ya juu.

By Jamhuri