Nianze mada hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye sina wa kumfananisha naye kwa kutujalia zawadi ya uhai na kwa mema mengi anayotujalia kila siku. Kipekee namshukuru Mungu kwa kuwezesha Kikao cha Kawaida cha 39 kwa nchi wanachama 16 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufanyika hapa Tanzania.

Ni heshima kwa nchi yetu kuona Rais John Magufuli akikabidhiwa madaraka ya kuiongoza SADC.

Mkutano ulifanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam: kwanza wataalamu wakakutana, kisha wakafuatiwa na Kikao cha Baraza la Mawaziri na hatimaye Kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali kilichofanyika Agosti 17-18, 2019. Ulikuwa mkutano wa kihistoria kwa taifa letu hasa kutokana na rais wetu kuwa Mwenyekiti wa SADC baada ya Rais Hage Geinhob wa Namibia kumaliza muda wake.

Mkutano ulimalizika kwa mafanikio makubwa, hivyo naamini wakuu wa nchi na serikali na walioambatana nao waliondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri kuhusu taifa letu na hasa vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Watanzania tuangalie tukio hilo kama mwanzo wa fursa za kufanya vizuri zaidi hasa kuhusu kujiendeleza kiuchumi kupitia Sera ya Uchumi wa Viwanda na kufikia kipato cha kati mwaka 2025.

Iwapo wakuu wa nchi na serikali wamedhamiria kwa dhati kuwa nchi wanachama wa SADC ziwe kinara katika kujiletea maendeleo endelevu; ni dhahiri kuwa tunahitaji kujizatiti vya kutosha ili kukidhi nia hiyo njema kupitia fursa za elimu, afya, madini, kilimo, viwanda, ufugaji, maliasili na utalii.

Rais Magufuli alipokabidhiwa Uenyekiti wa SADC; alisema kuwa nchi zinazounda umoja huu ikiwemo Tanzania ni tajiri mno. Akapinga dhana ya siku zote ya kwamba nchi hizo ni maskini.

Kwa mtazamo huo hajafurahishwa na hali halisi ndani ya SADC kutokana na rasilimali tulizonazo kutotumika kuinua uchumi wa nchi husika na kuboresha maisha ya watu wake.

Nchi za SADC ziliweka lengo la asilimia saba kama matarajio ya kupanda kwa pato la eneo la SADC kila mwaka. Hali halisi inaonyesha kuwa pato limekuwa likipanda kwa wastani wa asilimia 3 tu kwa mwaka.

Inawezekana kumekuwapo changamoto kama madhara ya mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame wa muda mrefu au mafuriko ya mara kwa mara; wakulima kutowezeshwa vya kutosha na kuwa na ukosefu wa mbegu bora au miundombinu ya umwagiliaji; masoko na kadhalika. Hatuna budi kuchangamka na kuhakikisha changamoto za aina hizo zinatafutiwa ufumbuzi.

Mwenyekiti Rais Magufuli alisisitiza kuwa SADC inazo rasilimali za kutosha ikiwemo ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 9,882,959 na rasilimali watu milioni 327 ambao ni nguzo kubwa ya kujiletea maendeleo.

Kwa mantiki hiyo, iwapo nchi wanachama wa SADC zitajipanga vizuri na kuweka mikakati ya pamoja juu ya namna bora ya kutumia rasilimali hizo kwa maendeleo yetu, pato litaongezeka. Aliyekuwa Rais wa Tanzania (1961-1985); Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne: “ArdhiWatuSiasa Safi na Uongozi Bora”. Nathubutu kusema kuwa mpaka leo nyenzo hizo bado ni muhimu kwa taifa kuweza kujiletea maendeleo endelevu.

Nchi 16 wanachama wa SADC zinamiliki ardhi ya kutosha, rasilimali hii ikiambatana na uongozi bora; siasa safi na wingi wa rasilimali watu na maliasili [misitu, wanyamapori, madini, maji, na uvuvi]: tukiunganisha nguvu ya pamoja hakuna sababu ya SADC kutosonga mbele kiuchumi ipasavyo kwa manufaa ya wote.

Naamini kwa kutumia vyombo kama Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) tutafanya kweli tukizingatia kuwa kwa miaka mingi changamoto za umaskini, maradhi na ujinga zimetusumbua sana. Sasa ni wakati wa kukabiliana na changamoto husika ipasavyo bila kutetereka.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa wakati mwingine ni rahisi kusema kuliko kutenda, lakini naamini kutokana na mshikamano ulioonyeshwa wakati wa Mkutano wa 39 wa SADC yawezekana tukafanikisha malengo kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na kujiwekea malengo ya kiuchumi, jumuiya hii inahitaji kuwapo hali ya kuridhisha kiusalama na amani kwa wote. Hili ni suala muhimu mno maana bila utulivu na usalama tutabaki kuwa katika hali ya kutoaminiana. Uchumi wa viwanda na kufikia kipato cha kati kwa nchi wanachama wa SADC vitawezekana iwapo kuna utulivu na amani mijini na vijijini. Mfano, wakulima, wafugaji, wafanyakazi na wafanyabiashara shughuli zao zitakwenda vizuri iwapo kutakuwapo miundombinu imara na masoko.

Kwa bahati nzuri soko kwenye eneo la SADC na Afrika Mashariki halina shaka. Kinachotakiwa ni kuzalisha bidhaa na huduma bora ili kukidhi mahitaji ya soko. Hayo yote yanawezekana ndani ya nchi iliyo tulivu na yenye amani ya kutosha.

Vivyo hivyo, mafanikio yatapatikana iwapo umoja ndani ya SADC utaimarika zaidi: kukawapo kusikilizana na sauti moja yenye lengo la kuinua mapato ya nchi wanachama, lakini pia kuboresha maisha ya wananchi ndani na nje ya nchi husika; mathalani kupitia biashara, kusimamia masuala ya forodha vizuri, ulinzi au usimamizi wa pamoja na kadhalika.

Penye mafanikio hapakosi kuwapo wasiopenda kuona nchi za SADC zinasonga mbele kiuchumi, hivyo tukae chonjo na kuchukua hatua kwa faida ya wote.

Kwa Tanzania, tunawashukuru wakuu wa nchi wanachama wa SADC kukubali Kiswahili kiwe lugha rasmi ya nne ya jumuiya hiyo. Lugha nyingine ni Kiingereza, Kifaransa na Kireno. Hili ni jambo jema kwetu Watanzania, maana kupitia uamuzi huo tutakuwa na fursa za kuendeleza Kiswahili Kusini mwa Afrika. Hii ni pamoja na fursa za ajira na kuandika vitabu kwa matumizi ya ndani na nje ya SADC.

Naomba Baraza la kuendeleza Kiswahili liwe mstari wa mbele kuhakikisha maneno ya Kiswahili ni sahihi katika kutamka na kuandika. Nimekuwa nikisikia maneno kama ‘lisaa limoja’; ‘masaa mawili’ na kadhalika mpaka najiuliza ‘hilo lisaa limoja likoje?’

Kwanini hatusemi ‘saa moja’ au ‘saa tano’ – ukiulizwa utatumia muda gani badala ya kusema ‘lisaa limoja’ au ‘masaa mawili’ ukasema nitatumia ‘saa moja’ au ‘saa mbili?’ Tumeegemea sana matumizi ya Kiswahili cha mitaani badala ya Kiswahili sanifu. Tutahitaji maboresho na kujifunza Kiswahili.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki SADC na Mungu Ibariki Tanzania.

160 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!