Tume ya haki za binadamu yakamilisha uchunguzi dhidi ya kifo cha mwanafunzi UDOM

Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Hatimaye Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)i mekamilisha uchunguzi wake huru kuhusu kifo cha Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Nusura Abdallah na kueleza kuwa hakihusiani na ajali iliyotokea usiku wa Mei 26 mwaka huu ilioyomuhusisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dk.Festo Dugange.

Aidha imesema vipimo vilivyofanywa na Madaktari wa Hospitali ya Faraja vimeonyesha kuwa kifo cha mwanafunzi huyo kilitokana na shambulio kali la kupanda kawa sukari na upungufu wa damu.

Akizungumza na wandishi wa habari leo Juni 2,2023 jijini hapa, Mwenyekiti wa THBUB Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema tume hiyo pia imebainisha kuwa gari aliyopata nayo ajali Dk.Dugange ilikuwa binafsi na alikuwa peke yake.

Kwa mujibu wa Jaji Mwaimu tume imefanya uchunguzi kuhusu kifo cha mwanafunzi UDOM Nusura ili kubaini ukweli baada ya kuwepo kwa mkanganyiko huku baadhi ya watu wakihusisha na ajali ya gari iliyomhusisha Naibu Waziri TAMISEMI Dk.Dugange.

Amefafanua kuwa katika uchunguzi huo tume ilitembelea eneo iliyotokea ajali ya gari iliyomhusisha Dk.Dugange,Nyumbani kwake,kituo cha polisi Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Benjamini Mkapa na UD0M.

Pia amesema tume ilitembelea Kijiji cha Mandewa, Kata ya Mandewa, Wilaya ya Singida Mjini wanakoishi wazazi wa marehemu Nusura, Kitongoji cha Mtakuja Kijiji cha Kikonge, Wilaya ya Iramba alikozikwa Nusura, Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine kwa madhumuni ya kupata maelezo.

Pamoja na hayo amesema baada ya kupata maelezo katika maeneo yote ilikofika, THBUB imebaini usiku wa Aprili, 25 mwaka huu ilitokea ajali ya gari maeneo ya Iyumbu, karibu na Njia Panda ya Shule ya Mfano, Jijini Dodoma ambapo gari iliacha njia, kugonga mti na kupinduka majira ya alfajiri Dk. Dugange alipata msaada wa boda boda iliyomfikisha Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Amefafanua kuwa Aprili,27 mwaka huu marehemu Nusura alisafiri kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro kwa basi la Manning Nice baada ya gari la Kapricon alilokuwa amepanga kusafiria kuchelewa alipokelewa na mchumba wake Juma Mohamed Kundya, Mjini Moshi ambapo walifika nyumbani kwake saa tano usiku.

“Marehemu Nusura alijisikia vibaya na kuanza kutapika hadi kuishiwa nguvu hali iliyosababisha kufikishwa Hospitali ya Faraja kwa matibabu pamoja na hatua mbalimbali za kitabibu zilizochukuliwa na Madaktari wa Hospitali hiyo, alifariki dunia majira ya saa 5:00 usiku ya Mei mosi mwaka huu .

Aliongeza kuwa :Vipimo vilivyofanywa na Hospitali hiyo vilionesha kuwa kifo cha Nusura Hassan Abdallah kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu

“Gari iliyopata ajali ilikuwa ni gari binafsi aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za Usajili T454 DWV, iliyokuwa ikiendeshwa na Dk. Dugange alikuwa peke yake katika gari hilo kkutokana na mazingira hayo, THBUB imebaini kuwa kifo cha Marehemu Nussura hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya iliyomhusisha Dk. Dugange