Tumekubali kusarenda kwa watia mimba

Kumekuwapo mjadala mpana unaohusu nafasi ya wanafunzi wajawazito kurejeshwa kwenye mfumo rasmi wa elimu.

Jambo hili limezungumzwa kwa miaka mingi bila suluhu. Si jambo jepesi katika mfumo wa maisha ya Kitanzania, hasa tukizingatia kuwa wapo wahafidhina wasiopendelea mageuzi kwenye mambo ya kimaadili.

Kitu kimoja tunaweza kukubaliana wengi, japo si wote – nacho ni haki ya mtoto wa kike kupata elimu sawa na anavyopata mtoto wa kiume. 

Kwenye hili tumeona mara nyingi adhabu ikimwangukia mtoto wa kike, lakini mtia mimba ameachwa aendelee na masomo na maisha kama kawaida.

Waziri wa Elimu ametoa msimamo wake huku wimbi la watoto wanaotiwa mimba likipamba moto. Njia rahisi ya kukabiliana na hali hii tumeona ni kuruhusu au kuhalalisha mimba. 

Kwa maneno mengine watia mimba wametushinda. Tumesarenda. Fikiria, vidume vitakavyokuwa vikifarijika kuona vilivyotibua maisha ya watoto wetu wadogo. Hatari sana. 

Miaka mitatu iliyopita nilifanya utafiti wa namna tatizo la mimba linavyowaathiri watoto wa kike wilayani Butiama. 

Taarifa ya utafiti inasikitisha, maana wapo hadi viongozi wa dola wanaotumia hali hiyo kama kitega uchumi kutoka kwa familia za wavulana au wanaume waliowatia mimba wanafunzi.

Tunalo tatizo kubwa katika nchi yetu, na hili kwa kweli tunapaswa kulisema ili ikiwezekana tupate tiba yake.

Suala la watoto wenye mimba kuendelea na masomo si jambo la kuamuliwa na Waziri wa Elimu au kwa ufupi ‘serikali’. 

Hili si suala la waziri kulala, kuamka na kutangaza kuwa kuanzia sasa watoto wajawazito wataendelea na mfumo rasmi wa elimu. 

Huu haupaswi kuwa uamuzi wa mtu mmoja au kikundi cha watunga sera/sheria wachache. Hili ni jambo linalohitaji mjadala mpana, kwa sababu linavuka mipaka ya elimu ya darasani na kwenda hadi kwenye masuala ya kiimani.

Mambo kama haya yanahitaji mjadala mahususi wa kitaifa ili watunga sera na sheria wasikie wenye nchi wanasemaje. 

Hali hiyo itaiweka serikali mahali pazuri endapo mbele ya safari kwenye utekelezaji wa uamuzi huo kutatokea changamoto hasi.

Nasema hivyo kwa kuwa tayari ni kama suala hili limeshapitishwa. Hakuna mahali tumeulizwa, “wananchi mna maoni gani”.

Hili ni suala linalohitaji mjadala wa wazi na baadaye wa kitaalamu kutoka kwa wabobezi ili hatimaye tuwe na kitu kilichoridhiwa na wengi.

Makosa haya haya tunayafanya kwenye elimu, tunayafanya kwenye uraia pacha, tunayafanya kwenye mikataba ya madini na kadhalika. 

Tumeyafanya hata kwenye kugawana nyumba za umma. Nyumba za umma wanajiamulia watu wachache kuzigawana kwa bei ya kutupa kana kwamba ni mali yao binafsi. Hili si jambo jema hata kidogo. Mambo ya nchi yaamuliwe ki-nchi.

Elimu yetu imekuwa kama panya wa maabara. Kila anayekalia kiti cha elimu anajiona ana haki ya kuwaza na kuamua kwa niaba ya Watanzania milioni 60! 

Huko nyuma kiti cha elimu kilikaliwa na bwana mmoja, naye akaamua kufutwa kwa michezo shuleni. Kana kwamba haikutosha, akaamuru kufutwa kwa masomo ya biashara na akaja na mfumo wa kuungaunga masomo kwa namna isiyoelezeka. Athari za uamuzi wake zimeendelea kuligharimu taifa hadi leo.

Katika hali ya kawaida haiwezekani waziri aamke tu na kutangaza kufuta michezo shuleni. Haiwezekani, hasa katika nchi ambayo ina watu wenye maoni na mawazo mbadala. 

Kuamua jambo kama hilo ndani ya ofisi moja si kuwatendea haki wananchi. Elimu si mali ya serikali, ni mali ya wananchi, kwa hiyo ni wananchi wenye haki na wajibu wa mfumo au aina ya elimu wanayostahili kuipata.

Tunapojadili kuruhusu wenye mimba kuendelea na masomo kuanzia chekechea, msingi na sekondari hatuna budi kujua misimamo ya wengine, wakiwamo wale wa madhehebu ya dini. Tuliambiwa na ndivyo ilivyo kwamba Tanzania haina dini, lakini watu wake wana dini.

Japo hatupendi masuala la dini yawe nyenzo katika masuala kama haya, bado ukweli unabaki palepale kwamba madhehebu mengi ni wadau wakuu wa elimu nchini mwetu. Sasa tujiulize, zile shule za Kikristo zitaruhusu watoto wanaotiwa mimba kuendelea na masomo? Zile shule za Kiislamu zitakuwa radhi kuwapokea wajawazito katika vyumba vya madarasa na viwanja vya shule zao? 

Je, ndugu zetu Wahindu na Mabohora watakuwa wanyenyekevu kwa amri na sheria za serikali hata wakawa tayari kukiuka misingi yao ya kiimani?

Kwanini ninauliza haya? Nauliza kwa sababu madhehebu yote yanaamini mimba nje ya ndoa ni uzinzi. 

Je, watakuwa tayari kuwa na wanafunzi wazinzi? Je, elimu ya malezi inayogusia, pamoja na masuala mengine watoto kutojihusisha na ngono wataitoa wakiwa katika hali gani? Madhehebu haya hayaamini katika matumizi ya mipira ya kiume, je, kwa sheria hiyo mpya viongozi wa dini watahimiza matumizi ya hivyo vifaa ili watoto wasipate mimba?

Ninarejea kusema kwamba lengo langu si kupinga hatua ya watoto wa kike kupata elimu, bali ninashauri mambo makubwa yanayohusu nchi yawe yanajadiliwa kwa upana na kuamuliwa na walio wengi.

Elimu ni roho ya nchi. Wengi walalalamika kuwa mfumo wa elimu tulionao haukidhi mahitaji ya karne ya 21. Tunasema elimu yetu haimwezeshi mhitimu kujiajiri. Ni aina ya elimu inayowajenga vijana kuwaza kuajiriwa.

Jawabu la malalamiko haya haliwezi kutolewa na vipande vipande na watunga sera wawili au watatu. Ni suala linalopaswa kuwa ajenda ya nchi yenye kushirikisha wadau wengi kadiri inavyowezekana kabla ya kuwa na jopo la kuandaa hitimisho. 

Hili la mimba za wanafunzi linapaswa kuwa kiji-sehemu tu katika mjadala mpana unaohusu elimu.

Mathalani, tunaamua lugha ya kufundishia iwe ipi kati ya Kiswahili na Kiingereza? Nini faida na hasara za kuchagua au kupinga matumizi ya lugha mojawapo?

Tuangalie masilahi ya walimu. Je, yawe sawa kwa walimu wa mijini na vijijini, au wa vijijini kwenye mazingira magumu wawe na vivutio vya ziada? 

Tuamue nani awe na sifa za kuwa mwalimu? Je, ni wale waliopata daraja la tatu na la nne au iwe ni wale waliopata madaraja ya kwanza na pili sekondari? 

Tuwe na mjadala wa kitaifa kama ni wakati sasa sifa ya kazi nyeti kama hii ya ualimu iwe ni kwa waliopata daraja la nne kama tulivyoona Polisi na Uhamiaji?

Tujadiliane tuone namna gani ya kuboresha shule za kata. Je, tuendelee kuona watoto wakitaabika kutembea kilometa hadi 20 kwa siku, au tuwe na sheria ya kuwa na mabweni hasa kwa wasichana?

Haya na mengine mengi yatakuwa na majibu endapo wanasiasa wenye dhamana watakiri kuwa hata wasio na madaraka wana akili na busara za kushauri mambo mazuri kwa manufaa ya nchi. Tuamue mambo makubwa kwa pamoja ili baadaye asiwepo wa kumlaumu mwenziwe.