Na Deodatus Balile, Nzega

Wiki iliyopita nilipata fursa ya kumsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan wakati anafunga kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda lililofanyika Dar es Salaam. 

Rais Samia ameeleza umuhimu wa serikali kufanya kazi na wafanyabiashara kwa kushirikiana. Rais Yoweri Kaguta Museni wa Uganda naye alikuwapo pia katika kongamano hilo.

Rais Samia ameeleza umuhimu wa kulegeza masharti ya kufanya biashara. Amekemea misuguano iliyotokea kati ya wafanyabiashara na serikali miaka ya nyuma. 

Amerejea yaliyokuwa yanatokea kati ya Tanzania na Kenya. Akasema Kenya walikuwa wakidhibiti biashara za Tanzania, mkuu wa mkoa jirani kutoka Tanzania naye anafunga mpaka, kwa mawazo ya dawa ya moto ni moto au jino kwa jino.

Akaeleza masikitiko yake kuwa uhusiano wa kibiashara ulifika hatua mbaya hadi Kenya na Tanzania zikafikia hatua ya kuchomeana vifaranga vya kuku. 

Hali hiyo ameisawazisha na sasa biashara zinakua kwa kasi kubwa kati ya nchi hizi mbili. Amemkemea waziri mmoja aliyesema Tanzania haitanunua sukari kutoka Uganda, akasema ni mpuuzi tu. 

Akasema Tanzania itanunua sukari Uganda. Akaongeza kuwa inahitajika mikutano ya mara kwa mara kati ya wafanyabiashara na serikali kurahisisha utendaji.

Sitanii, kubwa amesisitiza kuwa biashara zote zitakazofanyika, zifanyike kwa mujibu wa sheria na wafanyabiashara wawe tayari kulipa kodi halali. 

Kwa kweli ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru Rais Samia. Ninamshukuru si kwa jingine, bali kwa kutambua hili nililolenga kuliandika katika kipindi hiki cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, ambayo sasa inaitwa Tanzania Bara.

Wakati tunapata Uhuru, nchi yetu ilidhani wafanyabiashara ni kundi la wanyang’anyi. Kundi hili lilitengwa badala ya kukumbatiwa. 

Nchi zote zilizoendelea, rasilimali fedha zimeipata kutokana na wafanyabiashara. Ni serikali chache, kama zipo, ambazo zinavuka mipaka na kwenda kuwekeza katika nchi nyingine.

Wafanyabiashara wanapomiliki viwanda, biashara kubwa kubwa, wanawekeza katika nchi nyingine na kutengeneza faida. 

Wakitengeneza faida, wanalipa kodi kwa nchi zao. Sisi hapa kwetu tangu tumepata uhuru tulibaki na fikra kuwa Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi. 

Hatukukifanya kilimo kuwa cha kibiashara (kilimobiashara), kilibaki kuwa kilimo cha kujikimu, kumbe ni tanuri la kuzalisha umaskini.

Sitanii, enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakulima sehemu nyingi nchini walianzishiwa mazao ya chakula na ya biashara. 

Ni bahati mbaya mazao ya biashara hayakutiliwa mkazo uliostahili. Mazao kama pamba, kahawa, karanga, katani (mkonge), chai, karafuu na mengine yalibaki kuzalishwa kama hisani.

Zamani kulikuwapo na ma-Bwana na ma-Bibi Shamba. Hawa walikuwa wanapita vijijini kufundisha kilimo bora. Shule za msingi zilikuwa na walimu mahususi kwa ajili ya somo la kilimo. 

Mimi nikiwa shule ya msingi ndipo nilijifunza kulima nyanya, mchicha, kutengeneza wanga, kulima viazi mviringo, mahindi na mengine mengi.

Mwalimu wetu wa kilimo pale Shule ya Msingi Kyakailabwa, Jonathan Ifunya, alitufundisha hadi wimbo ambao sijausahau zaidi ya miaka 40 sasa. 

Wimbo huu uliimbwa: “Ninawatangazia ya kwamba kilimo ninakipenda, ninawatangazia ya kwamba kilimo ninakipenda, asiyependa kilimo kweli yeye ni maskini, asiyependa kilimo kweli yeye ni maskini, kweli…” Je, kuna shule ya msingi inafundisha wanafunzi kilimo kwa sasa? Mashamba ya shule bado yapo au yamevamiwa na kujengwa na walimu na ndugu zao?

Nakumbuka nyumbani kwetu tulikuwa tunauza kahawa kilo 2,200 kwenye Chama cha Msingi Nyakato, Bukoba. Mwaka huu nimemuuliza mama ameuza kahawa kilo ngapi, akaniambia wamepata kama kilo 40. Kilo 40! Kama mwaka 1980 tulikuwa tunauza kilo 2,200, leo mwaka 2021 nini kimetokea tukauza kilo 40? Ajabu, idadi ya wakaazi katika familia imeongezeka, ila uzalishaji umeshuka.

Sitanii, katika kuelekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika na siku chache baada ya Uhuru ninajipanga kuandika kuhusu tulipotokea kama taifa, tulipo na mwelekeo sahihi mbele ya safari. 

Nitaonyesha thamani ya mfanyabiashara, badala ya mwendelezo wa sasa ambapo Afisa Mtendaji wa Mtaa sheria inamthamini kuliko Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni kama Vodacom!

Nitaonyesha ukweli kuwa nchi haiwezi kuendelea bila watu wake kulipa kodi, na ninaposema watu wake kulipa kodi, simaanishi kodi ya kichwa kama ambavyo watu wenye mawazo finyu wanafikiri, bali kodi itokanayo na biashara. 

Tuwe na mfanyabiashara mmoja hadi 10 wanaolipa wastani wa kodi Sh trilioni 5 kila mmoja kwa mwaka. Tuwawezeshe wafungue biashara ndani na nje ya nchi. 

Ni neema kuwa na wafanyabiashara wenye uwezo kiuchumi na waadilifu. Tujenge maadili kwa sekta ya biashara, tuanze kuvuna neema ili tuishi kama malaika. Mungu ibariki Afrika. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri