Dar es Salaam

NA MWANDISHI WETU 

Kelvin John ajiandae kuubeba mzigo mzito wa kaka yake Mbwana Samatta katika soka la Tanzania. Ajiandae na maneno magumu ya Watanzania yatakapokuwa yanapenya kwenye ngoma za masikio yake. 

Ajiandae kuambiwa anacheza kwa kujisikia. Ajiandae kuambiwa hajitoi kikamilifu akiwa amevaa jezi ya Taifa Stars. Ajiandae kuambiwa si mzalendo. Ajiandae kukutana na vitu hivi. Hawa ndio Watanzania wa siku hizi. Wenyewe hata wala hawajali!

Samatta ana mengi ya kusema katika mpira wetu, lakini amechagua kukifunga kinywa chake. Haina maana kuwa hasikii  au haoni anachoambiwa siku Stars ikicheza na mambo yakienda kombo. Anasikia sana na anaona sana tu.

Rafiki yangu Kelvin anakaribia kumtua mzigo huu kaka yake Samatta na utakuwa mabegani mwake kwa miaka mingi ijayo.

Wiki iliyopita, Kelvin alitambulishwa rasmi kama mchezaji wa kikosi cha kwanza cha KRC Genk. Alisajiliwa Genk mwanzoni mwa msimu huu, lakini alikuwa akiitumikia timu yao ya vijana.

Kama Watanzania tumefurahi kuona Kelvin amepiga hatua moja mbele, lakini nyuma ya pazia huu ni mzigo mzito anaokaribia kuubeba. Ajiandae kwa kila kitu.

Watanzania watataka maajabu makubwa kutoka kwa Kelvin kila atakapokuwa akitua nchini kuitumikia Taifa Stars. Hawatataka kuona kitu tofauti. 

Watataka kila akiingia uwanjani, ama afunge bao au asababishe bao. Watataka acheze kama anavyocheza na Wazungu. Kila alichokipitia Samatta, ataanza kukipitia Kelvin.

Watataka vitu vyote vitokee kwa haraka bila kutazama nini kinachomfanya Kelvin afunge akiwa na Wazungu na nini kinachomsababisha asifunge akiwa na jezi ya Stars.

Unafuu atakaokutana nao Kelvin ni kuwa siku hizi kuna vijana wengi wa Kitanzania wanacheza nje. Samatta hakukutana na unafuu huu.

Uwepo wa vijana wengi wa Kitanzania katika soka la nje kwa kiasi fulani utamsaidia Kelvin, lakini hautaondoa lawama kwake. Yeye ndiye atakuwa ‘star’ wa timu.

Tunapofurahia maendeleo ya Kelvin nchini Ubelgiji, Morice Abraham pale Serbia, Novatus Dismas huko Israel, Yohana Mkomola akiwa Ukraine, tuendelee kuwasukuma na vijana wengine wa Kitanzania kwenda nje kwa wingi kadiri iwezekanavyo. 

Kelvin na hawa kina Morice walioko nje peke yao hawawezi kutuvusha kutufikisha nchi ya ahadi. Zaidi tutakuwa tunawakosoakosoa tu.

By Jamhuri