Tutapiga hatua muhimu kuandaa kanuni za mikutano ya hadhara

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Dk. Pindi Chana, kuandaa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Machi 12, mwaka huu na 

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Zuhura Yunus, Rais Samia ametoa agizo hilo baada ya kupokea maazimio ya awali kutoka kikosi kazi alichokiteua kufuatilia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa vyama vingi vya siasa uliofanyika Dodoma Desemba 15 hadi 17, mwaka jana.

Pia Rais Samia amemwagiza waziri huyo kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kutengeneza kanuni hizo.

Kikosi kazi hicho chenye wajumbe 24 kinachoongozwa na aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala na kinachowajibika moja kwa moja kwa Rais Samia, kiliwasilisha maazimio hayo Ikulu jijini Dodoma yakiwa yamegawanyika katika makundi matatu ya muda wa utekelezaji.

Huku azimio la muda mfupi likiwa ni uandaaji wa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Baadhi ya maazimio ya muda wa kati ni pamoja na rushwa na maadili katika uchaguzi, ruzuku, elimu ya uraia na masuala ya uchaguzi na Katiba mpya ni mpango wa muda mrefu.

Pamoja na mambo mengine, sisi Gazeti la JAMHURI tunaamini hatua ya kuandaa kanuni ya kuanza kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ni muhimu kwa sababu kimekuwa ni kilio cha muda mrefu, hasa kwa wanasiasa wa upinzani kulalamika kuzuiwa kuwahutubia wafuasi wao na kujenga uhai wa vyama vyao katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Licha ya jukumu hilo kupewa waziri huyo kwa kushirikiana na TLS na ZLS, lakini sisi JAMHURI tunaamini Jeshi la Polisi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia wataziheshimu kanuni hizo pindi zitakapoanza kutumika ili mikutano ya hadhara ifanyike bila kuvunja sheria za nchi.

Mbali na kanuni hizo kutaka kuundwa, lakini pia tunaomba mapendekezo 80 ya mkutano huo kama yalivyotajwa wakati huo na aliyekuwa Mwenyekiti wa mkutano huo, Profesa Mukandala, likiwamo la marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Polisi ili kuondoa vitendo vya uonevu kwa wanasiasa hapa nchini nayo yawekwe katika mpango wa muda wa kati.

Aidha, tunawaomba wadau wa siasa nao kufuata Katiba, sheria, kanuni na miongozo katika kutekeleza majukumu yao huku vyombo vya uamuzi navyo vinapaswa kutenda haki na kulinda amani.

Vilevile tunaomba pendekezo la muda wa kati lizingatie elimu ya uraia ili iwe endelevu na ianzie ngazi ya chekechea na isisubiri wakati wa uchaguzi huku serikali na vyombo vya dola navyo viepuke upendeleo vinapohudumia vyama vya siasa na wananchi nasi tuepuke siasa za chuki, bali tufanye siasa za kulinda masilahi ya nchi na kukuza maendeleo yetu.

MWISHO

By Jamhuri