Dar es Salaam

Na Andrew Peter

“Kocha mnabadili leo, baada ya miezi mitatu anakuja mwingine katikati ya msimu huo. Mnategemea mtafanikiwa vipi? Maana huyu timu bado hajaizoea, kaondoka, anakuja mwingine. Halafu mna mechi kubwa. Baadaye mkifungwa mnasema kumbe na huyu aliyekuja hana maana.”

Hiyo ilikuwa kauli ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, katika Mkutano Mkuu wa Yanga wa kupokea mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ya klabu hiyo.

Kauli ya Kikwete ndiyo imenisukuma kujiuliza ni kweli klabu zetu Yanga, Simba na Azam zinataka maendeleo ya soka la nchi hii au ndiyo uwekezaji unawekwa katika kamati za ufundi badala ya benchi la ufundi? 

Kama viongozi wa klabu hizo wangeweka misingi ya mafanikio ya timu kwa benchi la ufundi, leo tusingekuwa tunazungumza kuwa kati ya msimu wa 2015 hadi sasa, jumla ya makocha 30 wamefundisha soka ndani ya timu hizo.

Unaweza kujiuliza, kwa nini anauliza swali hili sasa wakati Yanga ipo chini ya Kocha Mohamed Nabi, Simba ikiwa kwa Mhispania Pablo Martin na Azam wapo kwa Mmarekani mwenye asili ya Somalia, Abdihamid Moallin.

Jambo la uhakika ni makocha hao kumaliza msimu huu wakiwa katika nafasi zao; hilo sina shaka nalo. Lakini baada ya hapo, lolote linaweza kutokea, wala usishangae! Ndiyo soka letu lilivyo.

Nabi anaweza kuiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa misimu minne, lakini mwishowe viongozi wakamtupia virago kwa kigezo cha kusaka kocha mwingine mwenye uwezo wa kuiongoza timu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pablo, pamoja na kufika Robo Fainali Kombe la Shirikisho Afrika, maisha yake ndani ya Simba yapo njia panda hata kama atafanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la ASFC kwa kigezo kile cha Simba kushindwa kucheza soka la kuvutia.

Mmarekani Moallin, pamoja na kusaini mkataba wa muda mrefu hivi karibuni na Azam, lakini maisha yake ndani ya klabu hiyo ni wazi hayana muda mrefu hasa kutokana na mwenendo mbovu wa timu katika ligi.

Azam kwao kuvunja mkataba na kocha si tatizo kabisa. Katika miaka hii saba, wamefundishwa na makocha 11, kaka zao Yanga makocha 10 na Simba makocha tisa.

Linapofika suala la kutimuliwa kocha ndani ya klabu hizi, usijidanganye kuwa ubingwa au soka la kuvutia ni vigezo vitakavyomfanya kocha abaki.

Tumeshuhudia makocha kadhaa wakitimuliwa muda mfupi tu baada ya kuziongoza timu hizi kutwaa ubingwa au kufanya vizuri kimataifa.

Hapo ndipo unajiuliza, je, ubingwa au mafanikio ya timu yametokana na juhudi za benchi la ufundi kweli au ndiyo mbinu binafsi za nje ya uwanja za viongozi?

Azam ilivunja mkataba na Joseph Omog akiwa kocha pekee aliyedumu kwa miaka mitatu; 2013 – 2015 akiiongoza Azam kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, tena kwa rekodi ya kutofungwa mechi yoyote.

Pia, mwaka 2015, Azam ilikuwa klabu ya kwanza Tanzania kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame bila kufungwa bao, lakini bado raia huyu wa Cameroon alitupiwa virago.

Mbali ya Azam, Simba waliwatimua Sven Vandenbroeck, Patrick Aussems, Pierre Lechantre na Joseph Omog pamoja na kuwaongoza kutwaa mataji ya Ligi Kuu na kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga walimtimua Hans Van Pluijm aliyeiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza. Pia George Lwandamina aliondoka pamoja na kuiongoza timu kutwaa mataji yote ya ndani.

Wakati Kocha Mwinyi Zahera pamoja na kujitoa kwake kutembeza bakuri Yanga ilipokuwa katika hali mbaya kifedha, haikumsaidia kubaki! Naye alitimuliwa baada ya GSM kuingia.

Wadau wengi wa soka wanalalamikia nchi na klabu zetu kukosa falsafa ya soka itakayokuwa msingi wa maendeleo wa mchezo huu unaopendwa.

Moja ya vikwazo vya kutimia ndoto hiyo nchini ni mwendo huu wa kutimua makocha kila mwaka. Unadumaza soka la Tanzania ingawa klabu hizi huleta makocha wenye viwango vya kimataifa.

Timuatimua hii inawafanya makocha washindwe kuwa na mipango ya muda mrefu kuendeleza klabu, badala yake wanatilia mkazo matokeo tu ya uwanjani.

Kuwaza ushindi zaidi kunawafanya makocha kuziingiza timu gharama ya kununua wachezaji wa nje na kushindwa kutengeneza mipango ya kukuza soka la vijana nchini.

Ni lazima klabu zetu zikubali kuwekeza kwa muda kwa makocha hawa pamoja na kutaka matokeo, tunahitaji kuona makocha wakikaa katika klabu hizi kwa muda ili kuingiza falsafa zao na kuleta mapinduzi ya kweli ya soka. 

Mafanikio yapo katika kuwekeza kwa makocha wazuri, wachezaji wazuri wanaopata malezi mazuri ya muda mrefu ikiwa timu moja.

0655 413 101

Makocha 30 waliopita Simba, Yanga, Azam

SIMBA

2021-2022: Pablo Franco Martin

2020-2021: Didier Gomez

2019-2020: Sven Vandenbroeck

2018-2019: Patrick Aussems

2018-2018: Pierre Lechantre

2016-2018: Joseph Omog

2016: Jackson Mayanja 

2015-2016: Dylan Kerr 

2015-2015: Goran Kopunovic

2014-2015: Patrick Phiri

YANGA

 2015-2016: Hans Van Pluijm (Uholanzi) 

 2016-2018: George Lwandamina (Zambia)

2018-2019: Mwinyi Zahera (DR Congo)

 2019:      Charles Boniface Mkwasa

 2019:     Luc Eymael (Ubelgiji)

2020:     Zlatico Krmpotick (Yugoslavia)

2020-21:    Cedric Kaze

2020-21:   Juma Mwambusi

2021-22:   Mohamed Nabi

AZAM

2013–2015: Joseph Omog 

2015: George ‘Best’ Nsimbe  

2015–2016: Stewart John Hall

2016: Zeben Hernandez

2017–2018: Aristica Cioaba

2018–2019: Hans van der Pluijm 

2019: Meja (mstaafu) Abdul Mingange

 2019: Etienne Ndayiragije

2019–2020: Aristica Cioaba

2020-2021: George Lwandamina

2021-2022: Abdihamid Moallin

By Jamhuri