a Mwanndishi Wetu, JamhuriMedia

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kufanya zoezi la uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Manispaa ya Tabora, mkoani Tabora na Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, mkoani Mara.

Akizungumza katika Mkutano wa Kitaifa wa Tume na Vyama vya Siasa kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo Novemba 16, 2023, jijini Dar es Saalm, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi , Jacob Mwambegele, amesema uboreshaji wa majaribio utafanyika kuanzia Novemba 24 hadi 30, 2023 na umepangwa kufanyika katika vituo 16 ambapo vituo 10 ni vya kata ya Ng’ambo na vituo sita (6) vipo kata ya Ikoma.

Amesema vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni

Amesema zoezi hilo linafanyika kwa lengo la kupima uwezo wa vifaa na mifumo ya uandikishaji itakayotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika nchi nzima kwa tarehe na ratiba itakayopangwa na Tume.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Ramadhan Kailima ameongeza kuwa uboreshaji wa majaribio utahusisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine, waliopoteza au kadi zilizoharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapiga lura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari.

Kailima amesema katika kufanikisha zoezi hilo, Tume itatumia vifaa mbalimbali vya uandikishaji yaani (BVR kits) ambazo zimeboreshwa na zina uwezo wa kuwasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura na ni tofauti na zile zilizotumika katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2015 na 2019.

Pia Mkurugenzi wa Uchaguzi amefafanua kuwa Tume imesanifu na kuboresha mfumo wa uandikishaji wa Wapiga Kura ili kukidhi muundo wa BVR Kits za sasa ambazo zinatumia programu ya android tofauti na BVR Kits za awali ambazo zilikuwa zinatumia programu ya Microsoft Windows.

“Mfumo wa uandikishaji ulioboreshwa utawawezesha wapiga kura ambao wameshaandikishwa na wapo kwenye daftari la wapiga kura kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zao ama kwa kubadilisha kituo cha kupigia kura iwapo amehama Mkoa au Wilaya nyingine au kurekebisha taarifa zao kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu zao za mkononi au kompyuta,” amesisitiza Bw.Kailima.

Ameongeza kuwa kuanzisha mchakato mtandaoni mpiga kura ataingia kwenye tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni www.nec.go.tz kwa kutumia kompyuta au simu janja kisha atabonyeza kiunganishi kilichoandikwa “Boresha Taarifa za Mpiga Kura” au atatumia anuani ya ovrs.nec.go.tz itakayompeleka moja kwa moja kuanzisha mchakato.

Bw.Kailima amesema vyama vya siasa vitashiriki kwa kuweka wakala mmoja kwa kila kituo cha kuandikisha wapiga kura ili waweze kushuhudia na kujiridhisha kuhusu taratibu zitakazotumika wakati wa uboreshaji wa majaribio wa Daftari.

Mkurugenzi wa Uchaguzi amesema kuwa utaratibu wa kuboresha taarifa kwa njia ya mtandao, hautawahusu wapiga kura wanaotaka kuandikishwa kwa mara ya kwanza na wapiga kura ambao kadi zao zimeharibika au kupotea.

“Hawa wanashauriwa wafike kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura na kufuata taratibu watakazoelekezwa na Maafisa wa Tume watakaokuwepo kwenye kituo,” amesisitiza Bw.Kailima na kuongeza:

“Tume inatoa wito kwa wananchi wenye sifa zilizotajwa wa kata ya Ng’ambo iliyopo katika halmashauri ya Manispaa ya Tabora na kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uboreshaji wa majaribio wa daftari.”