Ufisadi Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro unatisha

Pamoja na malengo mengine ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), lengo mojawapo ni kuboresha miundombinu ya utalii ili kuboresha huduma za kitalii (to provide high quality tourism services) kwa kutengeneza barabara kwenda kwenye vivutio kama Nasera Rock, Olkarian Gorge na aina mbalimbali za miundombinu ya utalii na si kufanya kazi za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Kwa kipindi cha miaka mitano ambacho Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro chini ya uongozi wa Mheshimiwa Pius Msekwa, Sh zaidi ya bilioni 15 (wastani wa asilimia 10 ya fedha zilizokusanywa kwa mwaka) zilitumika kwa ajili ya safari za kutangaza utalii zikilipwa kwa wakurugenzi.

 

Haya ni matumizi mabaya ya fedha kwani utangazaji wa aina hii hauna tija katika kukuza utalii kama ilivyooneshwa na mtaalamu wa utalii, Dk. Victor Runyoro.

 

Katika utafiti wake alisema hakuna uhusiano wa moja kwa moja wa watalii kuja nchi na safari zilizofanywa na Mamlaka (market strategies employed by TTB and other government institutions in Tanzania including NCAA, had shown no obvious impacts”). The question is why NCAA still use such amount of money notwithstanding the fact that no value for money).

 

Utalii hutengewa asilimia 14 wakati majukumu mengine yanatengewa ifuatavyo: Uhifadhi (asilimia 7) na maendeleo ya jamii (asilimia 10). Hivyo, huu ni ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali fedha kwa kutenga asilimia 10 kwa safari za nje pekee. Kuonesha kwamba fedha za kutangaza utalii na nyingine hazina usimamizi na hutumika kunufaisha watu binafsi, wakurugenzi na maofisa wanaohusika na mpango huo hujipatia wastani wa Sh 30,000,000 kwa mwaka.

 

Meneja anayehusika na Huduma za Utalii (mhariri anahifadhi jina) aliweza kujichotea zaidi ya bilioni moja kwenye Vote No.700905-100 katika kipindi cha miaka miwili tangu awe meneja, hivyo kumiliki magari na nyumba za mabilioni ya shilingi.

 

Hadi leo hii hakuna barabara za kwenda kwenye vivutio kama Ndutu, Orkeriani na Nasera Rock kwa sababu ya ukosefu wa fedha, lakini Bodi iliruhusu matumizi ya ziada (over expenditure) ya Sh 692,000,000 kwa ajili ya maonesho ya utalii mwaka 2011-2012 baada ya zaidi ya Sh bilioni 3 zilizopangwa kutumika kutotosheleza! Inashagaza kwani tangu Bodi hii ilipoingia hakuna gari la kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo lililonunuliwa.

 

Kuna uhaba wa vitendea kazi katika Idara ya Uhifadhi. Wajumbe wa Bodi wamekuwa wanaenda ziara za kimafunzo na safari za kutangaza utalii ambazo kimsingi walitakiwa watendaji ndiyo waende, hivyo pesa nyingi hutumika bila tija kwenye utendaji (operational expenditure).

 

Kwa mfano, Aprili 29, 2012 hadi Juni 4, 2012 ofisi za Ngorongoro zilikuwa wazi. Menejimenti ilikuwa safari nje ya ofisi na ziara mbalimbali zenye lengo la kujikusanyia fedha bila kujali shughuli nyingine za ofisi zitafanywa na nani. Mameneja huonekana ofisini ili kuchukua malipo mengine na kuondoka.

 

Hii ilisababisha matumizi mabaya ya fedha na magari. Wakuu wa idara ambao wanatumia fedha zilizotengwa kwenye bajeti za idara zao kama mali yao binafsi, wameweza kujinufaisha kadiri walivyotaka na washiriki wao. Hii ni kutokana na menejimenti kuamua ‘kujichukulia chao mapema’ kwa kuwa Bodi imekosa uwezo wa kudhibiti mapato na matumizi ya Mamlaka, kwani nao wanahusika kwenye ufisadi kupitia vikao vya dharura vya mara kwa mara, ziara za kamati za bodi za mara kwa mara pamoja na safari zisizokuwa na tija za kutangaza utalii nje ya nchi.

 

Mkurungenzi hupangiwa safari tatu na Mwenyekiti safari nne kwenda nchi atakayoichangua kwa kila mwaka wa fedha. Kila mkuu wa idara hutumia gari la shirika kama mali yake binafsi kwa shughuli zake binafsi bila kuingiliwa na mtu.

 

Kwa mfano, kila mwisho wa wiki wakuu wa idara huondoka Ngorongoro kwenda kuona familia zao zilizopo Arusha kwa kutumia magari ya umma, mafuta na kujilipa pamoja na dereva posho za kujikimu. Kwa wastani gari moja hutumia mafuta ya Sh 100,000 kila wiki; posho kwa wakuu wa idara ni wastani wa Sh 160,000 na madereva 105,000.

 

Hii ni kusema kwamba wakuu wa idara hutumia Sh milioni 500 kama malipo kwenda kuona familia zao na kutumia magari ya shirika ambayo hugharimu mafuta ya Sh zaidi ya milioni 400.   Hatimaye Pius Msekwa akiwa Mwenyekiti wa Bodi alikubali kwa shingo upande kustaafu kwa Bernard Murunya baada ya  kushirikiana naye kwa miaka zaidi ya minne, lakini cha ajabu ni kule kukaimisha ofisi ya Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro kwa Shaddy Kiambile, ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala ambaye akiwa Msimamizi Mkuu wa Mapato na Matumizi, alichukua mkopo kwa niaba Mamlaka kwenye Benki ya NBC na overdraft kwenye Benki ya Exim.

 

Mambo haya yalifanyika bila kujadiliwa na menejimenti, kibali cha Bodi wala wizara kama ilivyothibitishwa na taarifa za wakaguzi wa nje (external auditors) zilizoonesha ukweli. Msekwa alikuwa akiingilia shughuli za utendaji wa kila siku wa Mamlaka kiasi cha kuifanya menejimenti kukosa uamuzi.

 

Alijua Murunya hakuwa mweledi aliyebobea kwenye uhifadhi, lakini alikubali ashike nafasi aliyokuwa nayo. Hapo ndipo mambo kadhaa yakiwamo haya, yalifanyika:

  • Kugawa maeneo ya ujenzi wa hoteli
  • Upitishwaji wa zabuni kubwa kama za barabara, ununuzi wa magari na mitambo.
  • Mikataba ya hoteli na wadau wengine isiyo na maslahi mapana kwa Mamlaka.
  • Mchakato wa sheria mpya ya NCAA
  • Uhuishaji wa mpango mkakati (GMP) wa NCAA.
  • Murunya alipoachia madaraka, Msekwa alitumia madaraka na uzoefu wake wa kuwapo kwenye uongozi wa nchi, akafanya yafuatayo:
  • Kumuunga mkono Murunya kwenye ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki,
  • Kumkaimisha Shaddy Kiambile ambaye alikuwa mshirika mkubwa wa Murunya.

 

Kitendo cha kumwachia Shaddy kinashawishi mtu yeyote kuamini kwamba Mheshimiwa Msekwa na Bodi yake walikuwa na maslahi binafsi.

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, umekabidhiwa taarifa ya Tume ya Jaji mstaafu, Thomas Mihayo, aishughulikie ili kuinusuru NCAA iondokane na mtandao huu.

 

Kwa maoni yangu Mheshimiwa Msekwa atakumbukwa na Watanzania kama kiongozi hodari wa kuzima hoja zenye maslahi ya Taifa kwenye Bunge na nje ya Bunge akiwa Spika, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA ambako amefanya kazi kama Mwenyekiti Mtendaji na si wa vikao.

 

Naomba nimpongeze Mheshimiwa Saning’o ole Telele (Mbunge wa Ngorongoro) bila kuuma maneno wala kujali vitisho vya Msekwa. Alisimama na kueleza ufisadi unaoendelezwa na Mheshimiwa Msekwa katika kugawa maeneo ya NCAA kwa wawekezaji bila kujali ushauri wa kitaalamu na kuingilia utendaji wa kila siku wa Hifadhi kama ‘mwenyekiti mtendaji.’

 

NCAA kwa sababu ya ufisadi uliokomaa, matabaka matatu yamejengeka:

1. Tabaka la utawala likijumuisha Bodi na Menejimenti – hawa wanagawana fedha zinazopatikana kwani hakuna wa kuwazuia kufanya hivyo. Tabaka hili ndilo linaloneemeka na fedha za Mamlaka kwa kujilipa posho kwa wakurugenzi pamoja na mishahara minono.

2. Tabaka la wateule ambao ni wapambe wa watawala wanaopendelewa kwa sababu mbalimbali, zikiwamo za ukabila au urafiki (nepotism and favoritism).

3. Tabaka la wafanyakazi walalahoi ambao wamepoteza matumaini kwa kuishi kwenye umaskini ukizingatia changamoto za eneo lenyewe kutokuwa na fursa za kijamii na kiuchumi.

 

Matabaka ndiyo yanayoleta hali ya kutoridhika kwa wengine, hivyo kusababisha madhara kama yaliyotokea Serengeti National Park ambako maaskari ambao ndiyo wasimamizi wa rasilimali kama faru hulipwa posho ya Sh 10,000 kwa siku, wakati maofisa wengine wakisafiri kwenda kutangaza utalii hulipwa dola 400 hadi 600 kwa siku.

 

Hata walipolalamika hawakusikilizwa. Wakashushwa morali ya kufanya kazi. Kimsingi hili ndilo tatizo kubwa kunapokuwa na wachache wanaonufaika. Tunaomba Waziri mwenye dhamana achukue hatua madhubuti kulinusuru eneo hili la urithi wa dunia, kwani tayari amekabidhiwa taarifa ya Tume ya Jaji Mihayo iliyotumia Sh zaidi ya milioni 130.

 

Kwa mujibu wa Tume hiyo, tuhuma za matumizi ya madaraka na rasilimali ziko wazi. Ushauri kwa Mheshimiwa Rais azingatie ushauri wa wataalamu, asiteue watu wa aina ya Msekwa. Mungu ibariki Tanzania ipate viongozi waadilifu na wasio wanafiki na wabinafsi.

 

Maswali ya muhimu ya kujiuliza: Kwanini Bodi chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Msekwa ilazimishe mtu mmoja asimamie ukusanyaji wa mapato, aidhinishe matumizi na kuratibu masuala yote ya fedha yeye mweyewe?

 

Kwanini bodi iruhusu over expenditure ya Sh milioni 692 kwa ajili ya maonesho ya utalii mwaka 2011-2012? Waziri wa Maliasili na Utalii atachukua hatua stahiki?

 

Kwanini Ngorongoro iwe na over expenditure hadi kusababisha bank overdraft ya Sh bilioni 16.88 na mkopo wa Sh milioni 800 wakati makusanyo ya miaka mitatu kuanzia 2010 hadi 2012 ni Sh zaidi ya bilioni 120?

 

Bodi kutochukua hatua stahiki hata baada ya kujua kwamba Murunya na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala walikiuka taratibu za kukopa fedha, inamaanisha kwamba wana maslahi binafsi au la?

 

Je, misingi ya utawala bora na natural justice inaruhusu mtu mmoja kujisimamia, kujichunguza, kujihukumu na kujiidhinishia matumizi ya fedha za umma?

 

Kwanini NCAA inanunua vifaa mbalimbali kwa bei za juu sana na visivyo na ubora? Swali hili linatupeleka kuangalia ufisadi mkubwa unaoendelea kwenye ununuzi wa vifaa chini ya Kamati ya Ununuzi ya NCAA. Kumekuwa na tatizo la ununuzi wa vifaa vilivyotumika na vilivyo chini ya kiwango cha ubora, lakini kwa bei kubwa. Mfano, ni majenereta mawili yaliyonunuliwa kwa Sh 362,330,800. Hadi leo kuna utata kama ni mapya au la, na kama yanakidhi masharti ya mkataba.

 

Je, Mwenyekiti wa Bodi Msekwa ana kinga ya kutoshitakiwa kwa makosa ya jinai? Kampuni moja ilipewa mkataba wa Sh bilioni 6 kutengeneza barabara kutoka lango la Lodoare hadi golini kwa maelekezo ya Bodi. Mkataba huu ulipigiwa kelele na wadau kwamba ulikuwa na harufu ya ufisadi, lakini kampuni ililipwa pesa zote bila kujali ubora wa kazi.

 

Je, fedha za NCAA ni mali ya umma au za Bodi? Kama ni za umma, kwanini Serikali isiingilie kati kujua mapato na matumizi?

 

Nawasilisha.