Tanzania ni moja ya nchi zinazoendelea zilizoathiriwa kwa kiwango kikubwa na Magonjwa Yasiyoambukiza,kutokana na kuwaathiri watu wengi na kusababisha vifo.

Mwaka huu kitaifa maadhimisho ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanafanyika mkoani Mwanza yakiwa na kauli mbiu ya Badili Mtindo wa Maisha,Boresha afya.

Takwimu za karibuni za Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza yanatajwa kuathiri figo na kusababisha watu 4,533 kupoteza sawa na asilimia 1.03 ya vifo vyote ambapo kiwango cha magonjwa ya figo ni asilimia 14.

Taasisi ya Figo ya Taifa inaonyesha gharama za kusafisha figo kwa wiki ni zaidi ya sh. milioni 4.5 ambapo kubadilisha viungo hivyo nje ya nchi kunagharimu zaidi ya sh. milioni 50.

Idadi kubwa ya watanzania watu wazima na watoto wasio na hatia wameathiriwa na magonjwa ysiyombukiza na kuwapa mateso makubwa ya ugonjwa wa moyo,kisukari,shinikizo la juu la damu, mishipa ya damu,mifumo ya hewa na neva.

Licha ya Serikali kuhangaika na kuweka mipango na mikakati ya kupambana na kudhibiti magonjwa yasiyoyakuambukiza,bado Watanzania wengi wanaathirika na kupoteza maisha kutokana na magonjwa hayo yanayosababishwa na mtindo wa maisha na ulaji wa vyakula usiofaa.

Wananchi na wadau wa afya wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima (hayupo pichani) wakati kitoa taarifa kwa uma kuhusu maadhimisho ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, yanayofanyika mkoani humu kitaifa. 

Kisababishi kikuu cha vifo vya wagonjwa hao ni figo na mishipa ya moyo kushindwa kufanya kazi au madhara yanayotokana na matatizo ya magonjwa hayo yanayochangiwa na mtindo wa maisha na ulaji vyakula usiofaa.

Pia ujenzi wa mipango endelevu ya matibabu kwa wagonjwa wa figo,moyo,kisukari,mifumo ya neva na hewa ingali changamoto nchini,ushirikiano na jitihada za pamoja katika kudhibiti,kuzuia na kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza katika kiwango cha kimataifa zinahitajika kwa kutekeleza mambo yatakayosaidia kupunguza magonjwa hayo.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi, kula mlo kamili na kuepuka tabia hatarishi za unywaji pombe, dawa za kulevya na matumizi ya tumbaku.

Kuelekea maadhimisho ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia Novemba 5 hadi 12,2022 mwandishi wa makala hii alifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania(TDA), Profesa Andrew Swai kuhusu magonjwa hayo.

Profesa Swai ananza kwa kueleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza hayana vimelea vinavyoweza kusambazwa isipokuwa hutokea kutokana na uzembe wa mtu au kurithi.

Anasema magonjwa hayo ni saratani,magonjwa sugu ya njia ya hewa,figo, shinikizo la juu la damu,kisukari,magonjwa ya afya ya akili,ajali pamoja na selimundu.

“Magonjwa haya yameendelea kuongezeka kwa kasi,takwimu zinaeleza kuwa asilimia 71 ya vifo vyote duniani kwa mwaka 2016 vilitokana na magonjwa hayo pia magonjwa hayo huku asilimia 75 ya vifo vyote vya watu wenye umri wa miaka 30-70,” anasema Profesa Swai.

Anasema kuwa sababu za magonjwa hayo ni pamoja na ulaji usiofaa,matumizi ya vilevi,tumbaku,kutoshughulisha mwili,msongo wa mawazo na kutopata usingizi wa kutosha.

“Idadi ya Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha wa matatizo ya figo,uelewa huo mdogo kwa umma umesababisha wengi kushindwa kufahamu madhara makubwa katika mifumo ya mwili kama ubongo, moyo,figo, macho,mishipa ya damu na fahamu,”anasema.