Na Mwamvua Mwinyi, JAMHURI MEDIA, Kisarawe

Ofisa Uhamiaji Wilayani Kisarawe, Mkoani Pwani ,Mrakibu Mwandamizi Rose Mkandala amekemea tabia ya usafirishaji haramu wa watoto wadogo chini ya miaka 18 ,kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Kigoma ,na kuwafanyisha biashara ndogo ndogo ya karanga na mahindi .

Amesikitika kwamba , kwasasa Kisarawe inataka kugeuka kama sehemu ya biashara haramu ya usafirishaji watoto wadogo .

Akijibu swali la mzee Zelubabeli Michael Mahigima, alilotoa katika mkutano wa hadhara katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wilayani Kisarawe ,Rose amedai kuwa inashangaza mzee huyo kuuliza swali wakati ni mmoja wapo wa watu wanaofanya biashara hiyo kujinufaisha kupitia watoto hao.

Vilevile Rose ameeleza, zoezi hilo ni gumu ,linawapa usumbufu ,kwani wamekuwa wakibaini watoto ambao sio raia na kugharamika kuwarudisha walipotoka suala ambalo ni mzigo kwa Serikali .

Amesema, watoto hao ni wadogo na wamekuwa hawaendelei na masomo ,wanapangiwa chumba kimoja wanakaa wakifanyishwa kazi.

“Watoto hawa sio siri wanadaiwa kutoka Kigoma ,wanaacha shule hawasomi ,wanachukuliww huko kwa madai ni ndugu zake kwa wazazi wake wakati tukichunguza tunabaini sio kweli”

Rose amefafanua kuwa, wanaendelea na uchunguzi japo ni zoezi linalosumbua kwani wengine hawana uraia na vitambulisho vyao vya NIDA hawajafuata utaratibu.

Amesema, wanaojiridhisha na maelezo ,wanawarudisha kwao suala ambalo linaipa Serikali gharama kubwa .

Rose amesema kuwa, wale vijana ambao bado hawajajirishisha na taarifa za uraia wao wamewahifadhi.

Amewataka wananchi wilaya ya Kisarawe kama yupo anaetaka kuthibitisha uraia wa watoto wao ni mzazi mmoja,pasipo shaka wanawapigia simu mikoa walipotoka ama kuzaliwa.

Awali akiuliza swali mzee Zelubabeli aliinyooshea kidole Idara ya Uhamiaji Kisarawe kuwa haina ushirikiano ,wakienda kufuatilia uraia wa watoto wanaoishi nao wanaambiwa ni wakimbizi na kupewa masharti .

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, alieleza suala la kutumikisha watoto wadogo ni kinyume cha sheria,wanaobainika wachukuliwe hatua na sheria isipindishwe.

Kunenge alisema ,asionewe mtu ,Ila mtu akifanya makosa anapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

By Jamhuri