Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Ramadhani Kailima, amesema Tume hiyo inaendesha majaribio ya uboreshaji wa dafftari la kudumu la wapiga kura katika vituo 16 vya kuandikishia katika Mikoa ya Tabora na Mara kuanzia Novemba 24 hadi 30 mwaka huu.

Kailima amabainisha hayo leo November 10,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa majaribio wa daftari hilo na kueleza kuwa lengo la kuendesha zoezi hilo ni kupima uwezo wa vifaa na mifumo itakayotumika wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura utakaofanyika nchi nzima baada ya ratiba kutangazwa.

“Zoezi hili litafanyika katika kata ya Ng’ambo iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Tabora (Tabora) na Kata ya Ikoma iliyopo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rolya (Mara)katika vituo 16 vya kuandikisha wapiga kura kati ya hivyo 10 ni vya kata ya Ng’ambo na sita vipo kata ya Ikoma,Vituo vya kuandikishia vitafunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa 12 jioni,”amesema

Mbali na hayo ameeleza kuwa zoezi hilo litakaohusisha raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea na atakayetimiza umri huo kabla au ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Amesema zoezi hilo litahusisha vifaa na mifumo mbalimbali inayowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura na kwamba katika uboreshaji huo vyama vya siasa vitashiriki kwa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikishia lengo ni kushuhudia na kujiridhisha kuhusu taratibu zinazotumika wakati wa zoezi hilo.

“Mfumo wa uandikishaji ulioboreshwa utawawezesha wapiga kura ambao wameandikishwa na wapo katika daftari kuanza mchakato wa kuboresha taarifa zao kwa kubadili kituo cha kupiga kura iwapo amehama Mkoa au Wilaya kwa kutumia simu zao za mkononi, ” amesema na kuongeza,

Baada ya kukamilisha taratibu zote za kuwasilisha taarifa katika mfumo,mpiga kura atapokea ujumbe mfupi wenye kumbukumbu namba kupitia simu yake namba hiyo ataenda nayo kwenye kituo cha kuandikishia kwa ajili ya kumalizia hatua zilizobakia na kupatiwa kadi, “amefafanua Mkurugenzi huyo wa NEC.