Tamasha la wakati Mungu Season 2 kufanyika Desemba 15, 2023 Mlimani City

SIMPLY Special decor kwa kushirikiana na Halisi Ministry wameandaa tamasha kubwa la Wakati wa Mungu Season 2 litakalofanyika Desemba 15, 2023 katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam.

Katika tamasha hilo waimbaji maarufu wa muziki wa Injili kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajia kutumbuiza katika tamasha hilo huku waandaaji wa Tamasha la Wakati wa Mungu wakielezea maandalizi yanayoendelea kufanyika kuelekea siku hiyo itakayokutanisha watu wa kada mbalimbali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza tarehe ya kufanyika kwa tamasha hilo Mkurugenzi wa Simply Special decor Lilian Mkumbo amesema matarajio yao kwa mwaka huu Tamasha la Wakati wa Mungu Season 2 litakuwa zaidi ya lile la mwaka jana.

Amefafanua katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye tamasha la Wakati wa Mungu Season 2 wataendelea kutoa orodha ya watumishi wa Mungu watakaopanda jukwaani kuimba nyimbo za Injili huku akifafanua katika tamasha hilo Desemba 15

Amesema kuwa watanzania watarajie kuwa kadri siku zinavyozidi kusogea wataiona orodha ya waimbaji watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo linakusudia kukusanya watu ambao ratiba zao ni ngumu kutokana na majukumu yao au nyadhifa zao, taaluma zao na mambo mengi yanayosababisha wakose muda.

Ameongeza tamasha la Wakati wa Mungu hufanyika kwa mwaka mara moja kwa lengo la kukusanya watu hao ambao wanakosa muda, hivyo wameona ni vema wakaandaa tamasha ambalo litawafanya wahudhurie kwa ajili ya kumtukuza na kumuabudu Mungu sambamba na kuliombea Taifa kwa kuliweka katika mikono ya Mungu.

Wakati huo huo Mtumishi wa Mungu Rehema Simfukwe kutoka Halisi Ministry amesema ameshirikiana na Lilian Mkumbo kuandaa tamasha hilo kubwa lenye lengo la kuwaleta watu pamoja na kupata fursa ya kumtukuza Mungu.

“Tunawakaribisha sana watanzania wote pale Mliman City Desemba 15, 2023 , tamasha la Wakati wa Mungu Season 2 litakuwa la aina yake , hakika tunaomba waje na sisi watumishi wa Mungu tumejipanga na tuko tayari.”

Akizungumzia tamasha hilo Mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili Joel Lwaga amesema amejiandaa vya kutosha kwa ajili ya Wakati wa Mungu Season 2 huku akieleza amejiandaa vizuri.

Baadhi ya waimbaji waliotambulishwa kwamba watakuwepo katika Wakati wa Mungu Season 2 ni Lilian Mkumbo, Rehema Simfukwe, Christina Shusho, Joel Lwaga, Bena Kombo, Gwamwaka Mwakalinga pamoja na Patrick huku ikielezwa wataendelea kutoa orodha ya waimbaji watakaoshiriki siku hiyo.

Hata hivyo baadhi ya wageni waalikwa wakiwemo watumishi wa Mungu pamoja na Wachungaji wamewapongeza waandaaji wa tamasha la Wakati wa Mungu huku wakiwaomba kuendelea na tamasha hilo kwani limekuwa likiwakutanisha watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi,wafanyabiashara, watu mashuhuri na maarufu.