Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Kisiju ,Kata ya Kisiju ,Mkuranga mkoani Pwani ,bado kaa la moto ,kizungumkuti kwani umechukua muda mrefu huku wananchi wakiwa katika sintofahamu.

Wajumbe wa Bodi ya Barabara ,Mkoani humo, wameonesha kutoridhishwa  na muenendo wa mradi wa ujenzi huo ambao unatekelezwa na mamlaka ya bandari  nchini TPA .

Hali hiyo imejidhirisha  kwenye  kikao cha bodi ya barabara  kilichofanyika kwenye ukumbi  wa jengo la Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Pwani .

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga  Khadija Nassir ,aliibua hoja kwa nini ujenzi wa bandari hiyo imekua ikisuasua huku  Kila mwaka TPA (Mamlaka ya Bandari nchini )ikitenga  fedha  kwa ajili ya mradi huo.

‘”Mradi huu unadaiwa kusuasua licha ya kutengewa fedha za ujenzi wake na Mamlaka ya Bandari nchini TPA kila mwaka.”

Alieleza, mwaka wa fedha ulioisha ilitengwa sh. Bilion. 1. 2 (Moja nukta mbili) na mwaka huu wa fedha zimetengwa sh. Milioni 500.  

Hoja hiyo ni moja ya hoja iliyohitaji pia kutaka kujua msimamo wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) .

Mwenyekiti  wa CCM ,Mkoa wa  Pwani  Mwishehe Mlao akitoa tamko la chama kwa changamoto hiyo alisema CCM haiungi mkono  wananchi kunyanyasika kwa kucheleweshewa  huduma za bandari ili hali shughuli za kiuchumi zinakwama na  kurudisha nyuma maendeleo ya watu. 

Mkuu wa Mkoa Pwani – Abubakari Kunenge aliitaka TPA kupanga siku ,mkuu wa Wilaya na Viongozi wengine wafike Kisiju na kuwaeleza  wananchi ukweli na sio kuahidiwa na TPA kila mara kuwa wanakamilisha  ujenzi ndani ya muda mfupi wakati uhalisia ukiionekana wazi ujenzi bado utachukua muda. 

Mkurugenzi wa  huduma  za uhandisi  kutoka mamlaka ya bandari nchini , Baraka Mdima ambaye pia alimwakilisha Mkurugenzi mkuu wa TPA  alisema mradi ulihamia eneo jingine la  Kwale kutokana na  eneo la awali la Kisiju kujaa mchanga .