KATIBU wa Kamati ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis amesema kuwa madai ya ACT-Wazalendo ya kujitoa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) yapuuzwe na hayana mashiko kwani Serikali hiyo imeundwa kwa nguvu ya kura ya maoni ya Wananchi wote  kupitia mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

Hayo ameyasema wakati akitoa ufafanuzi juu ya hoja mbalimbali kwa Waandishi wa Habari hapo Ofisi kwake Kisiwandui Zanzibar.

Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) haikuundwa kwa matakwa,hisani na ridhaa ya Chama kimoja cha ACT-Wazalendo bali ipo kwa matakwa ya Wananchi waliopiga kura ya maoni ya kukubali wote kupitia kura ya maoni na kwamba hata kujitoa katika Serikali hiyo unafuatwa mfumo ule ule wa kupiga kura ya maoni.

Kupitia Mkutano huo Mbeto,alifafanua kuwa  ACT-Wazalendo wana ajenda binafsi ya kuirejesha Zanzibar katika machafuko ya kisiasa ni kutokana na vitendo na kauli zao hizo za vitisho dhidi ya Serikali iliyopo madarani.

Mbeto,alisema kama dhamira ya kujitoa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa itatimia litakuwa sio jambo jipya kwani walishawahi kususia vikao vya Baraza la Wawakilishi na  Uchaguzi wa marudio mwaka 2016 na nchi ilipiga hatua kubwa za kimaendeleo bila uwepo wao.

“Kwanza nataka ACT-Wazalendo wajue kuwa CCM na Serikali zake hazitishwi na yeyote iwe mtu,Chama cha kisiasa,kundi,taasisi ya ndani na nje ya nchi tupo imara hivyo waweke maneno ya akiba wasije kujuta juu ya maamuzi yao ya kukurupuka na mihemko ya kisiasa.

Pia Wajitoe tu Vyama vipo vingi wengine watachukua nafasi yao wasijione  wao ndiyo wenye hati miliki ya Zanzibar na nchi itaendeleza kubaki salama na CCM kuendelea kuwa Chama Tawala.”,alisema Mbeto.

Alitoa ufafanuzi juu ya Rais  Dk.Mwinyi,kuwaita ACT-Wazalendo kuzungumza nao alisema hilo ni jambo la Kawaida Rais wa nchi kukutana na watu mbali mbali kusikiliza maoni yao kisha yeye ndo mwenye maamuzi ya kutekeleza kile anachoona kinafaa.

Alisema vikao vya Rais wa Zanzibar na ACT-Wazalendo vilikuwa vya maridhiano havina uhalali wa kisheria wa kumlazimisha Rais Dk.Mwinyi atekeleze matakwa yao na kwamba kama ipo nyaraka yoyote yenye saini za makubaliano ya pande zote mbili basi zitolewe hadharani kama wanavyotoa madai yao mengine.

Hata hivyo alieleza kuwa CCM ipo tayari kukaa mezani kusikiliza maoni,ushauri na hoja za Chama chochote cha kisiasa chenye ushauri mzuri wa kuimarisha masuala mbalimbali ya kijamii,kisiasa na kiuchumi.

Katika maelezo yake Mbeto,alisema Chama hicho cha upinzani kimefilisika kisiasa Viongozi wake hawana hoja zenye mashiko wanapodai kuwa Uchaguzi wa mwaka 2020 ulikuwa sio halali inamaana hata wao pia hawana uhalali wa kuwa katika Serikali ya SUK wanayoichafua.

Sambamba na hayo Mbeto alisema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuheshimu utawala wa Kisheria wenye kujali misingi ya haki za binadamu huku kikihubiri siasa za uwazi zenye maridhiano kwa ujenzi wa nchi.