Home Makala Ukikata Tamaa, Palilia Matumaini

Ukikata Tamaa, Palilia Matumaini

by Jamhuri

Usikate tamaa, jua linapozama, nyota na mwezi vinachomoza, kuwa na matumaini. Alexander the Great alipokuwa anafanya kampeni aligawa zawadi mbalimbali kwa rafiki zake. Katika ukarimu wake karibu alitoa kila kitu alichokuwa nacho. Rafiki yake alimwambia: “Bwana hutabaki na kitu chochote.”
Alexander the Great alijibu: “Nimebaki na kitu. Nimebaki na matumaini.” Ukibaki na matumaini umebaki na jambo kubwa. “Usimnyanganye mtu fulani matumaini; huenda ndicho kila kitu alichonacho,” alisema H. Jackson Brown Jr.
Kwanza, palilia matumaini kwa kuwa na mtazamo chanya. Maana ya matumaini imeelezwa kwa mtazamo chanya na Askofu Desmond Tutu wa Afrika ya Kusini: “Matumaini ni kuweza kuona kuwa kuna mwanga licha ya giza lote.” Kuwepo kwa vivuli kunatupa matumaini kuwa kuna mwanga mahali fulani.
Watu wanaposema kuna dhiki matumaini yanasema baada ya dhiki faraja. Watu wanaposema umeshindwa, Watu wanaposema kesho haitabiriki, matumaini yanasema kesho itapendeza.
Watu wanaposema matatizo hujipanga foleni, matumaini yanasema, yana mwisho. Watu wanaposema yakimwagika hayazoeleki, matumaini yanasema kwa nguvu ya Mungu yanazoeleka.
Watu wanaposema, la kuvunda halina ubani, matumaini yanasema, la kuvunda lina ubani kwa nguvu ya Mungu. Watu wanaposema tumeshindwa, matumaini yanasema, jaribu ushindwe usishindwe kujaribu.
Watu wanapokusingizia na kusema una shitaka la kujibu, matumini yanasema, palipo na mshitaki kuna mtetezi. Watu wanaposema maovu yamezidi, matumaini yanasema neema imezidishwa ni neema juu ya neema.
Watu wanapoweka kituo na kusema mambo kwisha, matumaini yanaweka alama ya mkato na kusema utukufu ni mbele kwa mbele.
Watu wanapokwambia acha, matumaini yanasema, jaribu tena. Watu wanapokwambia, haiwezekani, matumaini yanasema, inawezekana. Watu wanapopaza sauti na kusema, hapana haiwezakani, matumaini yanasema, labda inawezakana.
Usiku watu wanaposema, kuna giza, matumaini yanasema, kuna nyota. Watu wanaposema, ni mwisho wa matumaini, matumaini yanasema, ni matumaini yasiyo na mwisho. Kuwa na matumaini unapokabili matatizo.
Kuwa na matumaini unapokabili misukosuko. Kuwa na matumaini unapokabili shida. Kuwa na matumaini unapokabili magumu. Kuwa na matumaini unapokabili mateso.
Watu wanaposema hiki si kipaji chako, matumaini yanasema juhudu na imani “huumba” kipaji. Kuna mwandishi ambaye alitaka kujua kama uandishi ni kipaji chake. Ilimchukua miaka kumi na tano kujua uandishi kuwa si kipaji chake wakati huo alikwisha kuwa mwandishi maarufu. Juhudi, imani na maarifa “vinaumba” kipaji.
Nani anaweza kuishi bila matumaini? Mtumbwi kabla ya kufika bandarini mawimbi yanakuwa makubwa. Hapo unajua mnakaribia kutia nanga. Unachangamka, na kuinua kichwa kama ishara ya matumaini. Ndege inapoanza kutelemka inapitia kwenye dhoruba ya mawingu unajua mnakaribia kutua. Hapo unainua kichwa kama ishara ya matumaini. Unachangamka.
“Basi mambo hayo yaanzapo kutokea changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia” (Luka 21: 28). Ukombozi ni neno la faraja. Ukombozi ni kuinuliwa tena na kurudishwa.
“Matatizo ya dunia yanapozidi kuwa mengi, inua vichwa vyenu, mioyo yenu ifurahi… ukombozi unakuwa karibu mnaotafuta,” alisema Baba wa Kanisa Gregori.
Pili, palilia matumaini kwa kufikiria ahadi za Mungu. “Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu” (Zekaria 9:12).
Juu ya kifungu hiki cha maneno mchungaji Joel Osteen wa Marekani alikuwa na haya ya kusema: “Wewe ni mfungwa wa matumaini? Wafungwa wa matumaini ni watu ambao wana mtazamo wa imani na mategemeo hata kama mambo yanaenda ndivyo sivyo.
“Wanajua Mungu ana mpango wa kuwavusha kwenye matatizo, mpango wa kuwarudishia afya, fedha, ndoto na mahusiano. Leo inawezekana upo ambapo usingetaka kuwa. Kuwa na matumaini maana mambo yote yanatii kanuni ya mabadiliko.”
Mungu anaahidi kurudisha maradufu. Matumaini yanasimama katikati ya kukata tamaa na utopia. Matumaini yakizidi sana ni utopia. Utopia ni maji ya matumaini yanayozidi unga wa uhalisia. Tunasema maji yanazidi unga.

You may also like