Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Wizara yake imejipanga  kuanzisha programu ya BBT Mifugo katika Ranchi ya Mkata kwa lengo la kuwawezesha vijana na wafugaji wengine kufanya ufugaji wa kisasa na wenye tija kubwa zaidi kwao na kwa Taifa kwa ujumla.

Ulega ameyasema hayo wakati akiongea na Wafugaji wa Kijiji cha Parakuyo wakati alipofanya ziara katika Ranchi Mkata iliyopo Wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro Julai 4, 2023.

Wakati akiongea na Wafugaji hao alibainisha kuwa mpango wa Wizara ni kutumia maeneo ya Ranchi hiyo ambayo ni moja kati ya Ranchi za Taifa (NARCO) kupangisha vijana na wafugaji kwa muda maalum ambao utawawezesha wafugaji kutumia eneo kwa muda mfupi kufanya unenepeshaji wa mifugo na kisha kuiuza ndani na nje ya nchi.

Amesema utekelezaji wa programu hiyo ni maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuanzishwa kwa programu maalum ya vijana itakayo wawezesha vijana kujiajiri kupitia sekta ya mifugo.

“ Tumepanga kutengeneza vitalu  kwenye Ranchi hii kwa ajili ya Vijana waliomaliza mafunzo kwenye vituo atamizi na Wafugaji wa Mkoa wa Morogoro ambao wanahitaji maeneo ya malisho (Livestock Guest House) kwa ajili ya kufanya unenepeshaji wa mifugo”, alisema

Amefafanua kuwa katika maeneo hayo watakayoyatenga kwa ajili ya kupangisha wafugaji kwa muda mfupi wataiwekea  miundombinu kama vile majosho, mabwawa, mabilika, mazizi, ghala la majani na nyumba  maalum ya mifugo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema kuwa wao kama Mkoa wapo tayari kuunga mkono programu hiyo ili yale malengo ya Wizara ya kufanya mageuzi katika sekta ya mifugo mkoani humo yaweze kufanikiwa.

Ameongeza kuwa programu hiyo ikifanikiwa itakuwa chachu kwa wafugaji wa Mkoa huo kubadilika na kuachana na migogoro ya kila uchao.

By Jamhuri