Kundi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, linasonga mbele kwenye hujuma zake katika maeneo ya kimkakati, mashariki mwa nchi hiyo, baada ya kuiteka miji miwili muhimu.

Umoja wa Mataifa umetowa tahadhari hiyo jana Jumatano, ukionesha msisitizo wa kitisho cha uwezekano wa mgogoro huo kuwa wa kikanda.

Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja huo wa Mataifa katika eneo la maziwa makuu, Huang Xia, amesema ikiwa taarifa walizo nazo ni sahihi, basi inaonesha kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda linaendelea kusonga mbele kuelekea maeneo muhimu ya kimkakati katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini.

Wakati huo huo, mkuu wa ujumbe wa kulinda amani wa umoja huo nchini Kongo Bintou Keita, pia amezungumzia wasiwasi wake kuhusu kusonga mbele kwa M23 ambao hivi sasa wako katika eneo la makutano ya mipaka kati ya Kongo, Rwanda na Burundi.