Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Romania, Klaus Iohannis, atafanya Ziara ya Kitaifa nchini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Novemba 2023 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, lengo la ziara hiyo ni kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Romania. Sambamba na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta mbalimbali kama Uwekezaji, Elimu, Utalii, Afya na Utamaduni.
Uhusiano wa Kibiashara na Uwekezaji
kushirikiana katika sekta ya biashara na uwekezaji ambapo bidhaa kuu za Tanzania zinazouzwa Romania ni minofu ya samaki aina ya sangara, chai, tumbaku na parachichi. Pia, Tanzania inanunua kutoka Romania bidhaa za mashine za umeme, vifaa vya matrekta, magari na vifaa vya matibabu.
Kupitia ziara hii Tanzania na Romania zimedhamiria kuinua na kuimarisha kiwango cha biashara kati ya nchi hizi mbili ambacho licha ya Tanzania kuuza zaidi bidhaa zake nchini Romania, kiwango cha biashara kati ya mataifa haya mawili bado ni kidogo na kimeshuka katika miaka ya hivi karibuni ikilinganishwa na fursa za kibiashara zilizopo.
Mathalani mwaka 2021 Tanzania iliuza Romania bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 7.9 ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 4.06. Kadhalika,Romania ilinunua bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 11.6 ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo ilinunua bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 2.4. Kwa upande wa uwekezaji, Romania imewekeza nchini kwenye miradi ya usafirishaji, viwanda na utalii yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 6.04 na kuzalisha ajira 89. Romania pia imewekeza Zanzibar miradi mitatu yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 7.5 kwa mwaka 2023 na kuzalisha ajira 64.
Vilevile ziara hii ni fursa kwa Tanzania kuimarisha soko lake la utalii nchini Romania ambapo kwa sasa takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watalii kutoka nchini humo imeongezeka kutoka 6,418 mwaka 2018 na kufikia 12,148 mwaka 2022.
Uhusiano wa Kidiplomasia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Romania zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1964 ambao umejikita katika sekta za elimu na afya hususani ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Tanzania.
Katika kuimarisha uhusiano huo,mwaka 2018 Tanzania na Romania zilitia saini Hati ya Makubaliano kuhusu mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia. Mtiririko wa matukio ya ziara Rais Iohannis na ujumbe wake watawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba tarehe 16 Novemba 2023.
Rais Iohannis atapokelewa rasmi Ikulu Dar es Salaam tarehe 17 Novemba, 2023 na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Baada ya mapokezi hayo, viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha na baadaye watashiriki katika mazungumzo rasmi kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Romania. 11/16/23, 12:43 AM Rais Klaus Iohannis wa Romani
Aidha, viongozi hao watashuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano kati ya Tanzania na Romania katika sekta za kilimo, mifugo, misitu, chakula na masuala ya uokoaji wakati wa dharura na kuzungumza na Waandishi wa Habari kuelezea masuala muhimu yaliyojiri katika mazungumzo yao.
Akiwa nchini, Rais Iohannis na ujumbe wake watakwenda Zanzibar kuzungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi tarehe 18 Novemba, 2023 na baadaye kutembelea vivutio vya utalii ukiwemo Mji Mkongwe. Kufanyika kwa ziara hii ni kielelezo cha jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo.