Usiyapoteze machozi yako

Na Padri Dk. Faustin Kamugisha

Ukimpiga mbwa viboko vitano na binadamu viboko vitano, binadamu anaumia sana kuzidi mbwa kwa sababu binadamu analeta mateso aliyoyapata wakati huu, na aliyoyapata zamani na atakayoyapata; anaumia sana. Anatoa machozi. 

Msemo wa kuwa ‘wafalme hawalii’ si kweli. Kenneth Kaunda wa Zambia alitembea na leso ya kufuta machozi. Baraka Obama alidondosha machozi alipofiwa na nyanya (bibi) yake. Bill Clinton alitoa machozi mara nyingi. Jambo la msingi usiyapoteze machozi yako. 

Kuna aina mbalimbali za machozi. Kuna machozi ya kusingiziwa. Kuna machozi ya kurubuniwa. Kuna machozi ya kufiwa. Kuna machozi ya kufadhaika. Kuna machozi ya kuchanganyikiwa. 

Kuna machozi ya mpendwa kuwa mbali. Kuna machozi ya kukataliwa. Kuna machozi ya kutopata mchumba. Kuna machozi ya kutozaa. Kuna machozi ya kupoteza. Kuna machozi ya ahadi zilizovunjwa. Kuna machozi ya kusemwa. Kuna machozi ya kukata tamaa. Kuna machozi ya mateke ya shukrani ya punda. 

Kuna mama ambaye alimwambia mara nyingi mtoto wake abadilike. Mtoto hakumsikiliza mama yake. Alikuwa nchi za mbali. Mama alilia ameinama kwenye bakuli. Alichukua machozi hayo na kuyaweka kwenye chupa. Alimtumia mtoto chupa hiyo yenye maneno: “Machozi yangu ya kukulilia yafanyie kazi yasipotee, badilika.” 

Nyakati za zamani za Agano na Kale machozi yalitiwa katika chupa zilizoitwa chupa za machozi (lachrymatories). Zilitumika kukusanya machozi ya waombolezaji. Chupa hizi ziliwekwa juu ya kaburi la marehemu. 

Umepokea machozi yangu umeyakusanya katika chupa. Je, si yameandikwa katika kitabu chako.” (Zab 56:9). 

Ni kama kwamba Mungu ana chupa ya kukusanyia machozi. Hii ni lugha ya picha ya kusema kuwa Mungu anakumbuka magumu yote watu wake wanayopitia. 

Machozi ni sala ‘yanakwenda’ kwa Mungu pale ambapo hatuwezi kusema wala kuzungumza. Mungu anafuatilia machozi yako. 

Machozi ni tiba. Tunasoma hivi katika Biblia: “Macho yetu yachuruzike machozi.” (Yeremia 9:18). Huko Japan kuna tukio linaitwa ‘Ruikatsu Kansai’.

‘Rui’ maana yake machozi na ‘katsu’ maana yake shughuli. ‘Kansai’ ni eneo. Katika tukio la Ruikatsu huko Osaka, Japan watu hupangusa machozi kwa vitambaa. 

Watu kama 20 wanahudhuria wenye umri wa kuwa shule za msingi hadi watu wenye umri wa miaka 60. Wanatazama video zinazowafanya walie. Hii ni tiba ya kulia. Ili upate uponyaji wa vidonda vya moyo; “Macho yako yachuruzike machozi.” 

Kulia machozi ni ukamilifu wa ubinadamu. Binadamu ana hisia. Kulia machozi ni tiba ya kisaikolojia. Kibaiolojia kuna aina tatu za machozi; machozi ya kusafisha macho, machozi ya kitoto ambayo hutiririka pale jicho linapopigwa au kuingiwa na pilipili. Aina ya tatu ya machozi ni machozi ya hisia, ambapo mhusika anapata faraja au nafuu ya kisaikolojia. 

Aina hii ya tatu ndiyo inashughulisha akili zetu katika kitabu hiki.  

Muombolezaji kama amekuwa akitunzwa na marehemu na kupata matumizi ya kawaida humuita marehemu majina kama sukari yangu, chumvi yangu, taa yangu, usafiri wangu – kutaja machache. 

Kutoa machozi huku ni mtakaso wa hisia. Ni tiba kwa vile hisia zilizochemka zinapozwa. Katika kulia baadhi ya watu huongea na marehemu kana kwamba bado yuko hai. Katika kufanya hivyo hutua mzigo wa huzuni. 

Biblia ina mifano ya watu walioomboleza kifo cha jamaa yao na kutoa hisia zao kwa njia ya maneno. Mfalme Daudi alipotaarifiwa kuwa mtoto wake Absalom amekufa, alishikwa na huzuni na kuomboleza akisema: 

“Mwanangu Absalom, mwanangu Absalom! Laiti ningalikufa badala yako! Ole, Absalom mwanangu! Mwanangu!” (2 Samueli 18: 33). 

Machozi makali yatiririkayo juu ya makaburi ni ya maneno ambayo hayakusemwa na matendo ambayo hayakutendwa.” (Harriet Beecher Stowe).