*Anaendeleza ujenzi wa miradi mikubwa

*Anaimarisha diplomasia ya uchumi

*Anaboresha utawala bora, demokrasia

DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Rais Samia Suluhu Hassan ametimiza mwaka mmoja tangu aapishwe Machi 19, mwaka jana na kuanza kuongoza nchi baada ya kifo cha Rais Dk. John Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka jana wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena iliyopo Dar es Salaam.

Mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani umetimia wiki iliyopita huku nchi ikiwa inashuhudia mambo mengi mazuri ya uongozi wake, hasa serikali kuongoza kwa kufuata utawala wa sheria na kuanza kufunguliwa kimataifa.

Jumamosi ya wiki iliyopita kupitia akaunti yake rasmi ya Mtandao wa Twitter, Rais Samia, ameshukuru kwa kutimiza mwaka mmoja tangu aanze kuongoza nchi.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na kudra zake hadi hii leo ninapotimiza mwaka mmoja tangu nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawashukuru nyote kwa pongezi na salamu za kheri. Tuendelee kufanya kazi na kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, ndani ya mwaka mmoja Rais Samia amefanya mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali hapa nchini, ikiwamo kuboresha huduma za jamii, kuimarisha demokrasia, kuboresha mazingira mazuri ya biashara na idadi ya watalii imeongezeka hasa baada ya kufanya kipindi maalumu cha ‘Royal Tour’ akiwa kama mwongoza watalii.

Ujenzi wa miradi mikubwa ukiwamo wa reli ya kisasa (SGR) kutoka ‘lot’ ya tatu hadi ya tano, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) limefikia asimilia 60 sasa kutoka asilimia 46 alizozipokea kutoka kwa mtangulizi wake, barabara, madaraja na vivuko nao bado unaendelea, ukusanyaji mapato unaongezeka baada ya kuipiga marufuku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi kwa njia ya ubabe, uhuru wa vyombo vya habari umerejea na baadhi ya magazeti yaliyofungiwa yamefunguliwa kwa kukabidhiwa leseni za uendeshaji na nchi inazidi kufunguka kiuchumi kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji.

Pia tangu ameingia madarakani ametekeleza mambo mengi kwa vitendo, ikiwamo kupitia mienendo ya baadhi ya kesi nchini, hatua hiyo ikilenga kuimarishwa kwa utawala wa sheria.

Kupitia uamuzi huo, watu zaidi ya 400 waliokuwa mahabusu kwa kesi zisizo na ushahidi wameachiwa huru, wakiwamo viongozi wa Uamsho waliosota mahabusu kwa muda wa miaka minane kwa tuhuma za ugaidi, huku hatua hiyo ikienda sambamba na kuzipitia sheria zenye ukakasi na kuzifanyia marekebisho.

Katika kukuza demokrasia, Rais Samia ameruhusu utungwaji wa kanuni zitakazoruhusu vyama vya siasa nchini kurejea katika ulingo wa siasa za majukwaani, kwa kufanya mikutano ya hadhara na shughuli za kisiasa bila vikwazo.

Pia mageuzi makubwa ya uongozi wa Rais Samia yameshuhudiwa katika kushughulikia masuala ya diplomasia ya uchumi.

Katika eneo hilo, amefanikiwa kurejesha uhusiano wa  kimataifa baina ya Tanzania na mataifa mengine duniani ambayo awali ulitaka kuzorota.

Uhusiano huo umeleta matunda makubwa na hadi sasa mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwamo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yamezidi kuahidi kuikopesha Tanzania mikopo yenye riba nafuu.

Kuimarika kwa uhusiano huo na mashirika ya kimataifa tumeshuhudia matunda ya mkopo wa Sh trilioni 1.3 wa masharti nafuu uliotolewa na IMF kwa ajili ya mapambano dhidi ya Uviko-19 na fedha hizo zimetumika katika miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ununuzi wa vifaa tiba na miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na salama.

Kuimarishwa kwa mashirika ya umma

Rais Samia ameimarisha mashirika ya umma kwa kuteua viongozi wenye uwezo na ujuzi wa kuyaongoza kwa tija.

Baadhi ya mashirika hayo ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kumteua Masha Msomba kuwa Mkurugenzi Mkuu. Pia hivi karibuni amemteua Peter Ulanga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na amemrudisha Nehemia Mchechu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kisha akamteua Erick Hamis kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Elimu

Katika kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inakuwa na ubora, Rais Samia ameruhusu kufanyika kwa mchakato wa kuboreshwa kwa mtaala wa elimu.

Hatua hiyo inakwenda sambamba na kuboreshwa kwa elimu ya ufundi nchini na kuhakikisha hilo linafanyika, serikali imetenga Sh bilioni 30.84 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika wilaya 25.

Sekta ya Afya

Kwa kipindi cha mwaka mmoja, Wizara ya Afya imepokea Sh bilioni 891.5 kwa ajili ya kutekeleza huduma bora za afya ikiwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu yake katika hospitali mbalimbali zilizopo nchini.

Sekta ya Kilimo

Ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake, kilimo kimeongezewa bajeti na kuna maeneo matano ambayo bajeti hiyo imeelekezwa.

Eneo la utafiti limepangiwa Sh bilioni saba hadi bilioni 11; uzalishaji wa mbegu Sh bilioni 5.42 hadi bilioni 10.58; eneo la umwagiliaji Sh biloni 17.7 hadi bilioni 51.48 na maofisa ugani Sh milioni 603 hadi Sh bilioni 11.5.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akiwa Arusha ameuzungumzia mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia kuwa umechochea ukuaji wa uchumi na sasa unaimarika kwa asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.8 mwaka 2021.

Mwigulu amesema ukuaji wa uchumi ulishuka baada ya mlipuko wa ugonwa wa Uviko-19 kutoka ukuaji wa asilimia 7.0 hadi asilimia nne na baadaye asilimia 4.8 mwaka 2021.

Amesema kwa sasa ukuaji umepanda tena kutoka asilimia 4.8 hadi 4.9 huku Benki ya Dunia wakitabiri ukuaji huo kufikia asilimia tano hadi asilimia 5.5 kulingana na hali ya mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa sasa.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda, akizungumzia mafanikio ya uongozi wa Rais Samia amesema wilayani hapo wamefanikiwa kupata Sh bilioni nne kwa ajili ya mradi wa umeme.

Amesema kupitia fedha hizo, hadi sasa jumla ya kaya 656 zimeshaunganishiwa umeme huku hatua nyingine za kukamilisha uunganishwaji umeme kwa kaya zilizosalia ukiendelea.

Amesema matarajio ya serikali wilayani hapo ni kuhakikisha jumla ya kaya 1,500 zinaunganishiwa umeme kupitia fedha hizo.

Naye, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk. John Pima, amesema Rais Samia amedhamiria kuboresha mazingira ya elimu nchini huku akibainisha kuwa serikali imeipatia halmashauri hiyo Sh bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 105, kutengeneza madawati 5,250 na ujenzi wa matundu 44 ya vyoo.

Dk. Pima amesema ujenzi wa madarasa, madawati na vyoo ulikamilika tangu Desemba, mwaka jana na kukabidhiwa kwa wahusika.

Kwa upande mwingine amesema Januari, mwaka huu Arusha imepokea zaidi ya vitabu laki moja vya kiada na ziada kwa shule zote za serikali za msingi zenye mchepuo wa Kiingereza na Kiswahili kuanzia darasa la awali hadi la saba kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Baadhi ya walimu waliozungumza wakati wa upokeaji wa vitabu hivyo akiwamo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Themi, Zebedayo Mollel na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Daraja Mbili, Zukra Karunde, wamesema serikali itarajie mabadiliko makubwa kitaaluma.

Wamesema awali kitabu kimoja kilikuwa kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya watano lakini kwa idadi ya vitabu walivyopokea kitabu kimoja kitatumiwa na mwanafunzi mmoja au wawili tu.

By Jamhuri