Na Bituro Kazeri, JamhuriMedia, Mwanza
Hakuna tukio linaloibua maswali mengi kama kuukuta mtumbwi ufukweni ukiwa hauna wavuvi, huku samaki waliomo wakiwa wameoza.
Watu hujiuliza; wenye mtumbwi wamezama? Wameukimbia? Au kuna jambo kubwa lililotokea nyuma yake?
Ndivyo ilivyo kwa matukio ya Oktoba 29, 2025. Tukio hilo limeacha maswali mengi kuliko majibu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Tume ya Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, waliohusika walionekana kuwa na maandalizi ya kina, ikiwamo ramani za maeneo ya kupita, maeneo ya kushambulia na maeneo ya kuyaacha.
Wafanya vurugu kuwa na maji ya kujikinga dhidi ya mabomu ya machozi ni ishara kuwa kulikuwa na maandalizi maalumu. Kulikuwapo pia watu waliokuwa wakichukua picha na kurekodi ushahidi kwa matumizi ya baadaye dhidi ya serikali.
Maiti zilipigwa picha, majengo yaliyoteketezwa yakarekodiwa kwa picha mjongeo, ingawa usambazaji wa taarifa ulikwama baada ya kuzimwa kwa mitandao ya mawasiliano.
Kuzimwa kwa mitandao ndilo jambo ambalo wanaharakati wengi wameendelea kulilalamikia kwa madai kuwa liliwanyima uwezo wa kusambaza taarifa kwa wakati.
Dunia ina ushuhuda mwingi kuhusu nguvu ya uchochezi, uhisishaji na uaminishaji katika kuathiri uwezo wa watu kufikiri kwa utulivu. Mara nyingi mifano hiyo imeonekana zaidi kwa viongozi wa dini kuliko kwa wanasiasa au wanaharakati.
Tukio la Oktoba 29, 2025 linaonyesha kuwa hata wanasiasa wanaweza kutumia hisia na imani kali kuwafanya watu wasitumie tena mantiki katika kufanikisha malengo yao.
Walioshawishi matukio hayo hawana tofauti kubwa na Mchungaji Joseph Kibwetere wa Uganda aliyewaaminisha wafuasi wake mwaka 2000 kuwa mwisho wa dunia umefika, wakauza mali zao na kuingia kanisani walikoteketea kwa moto ulioua mamia ya watu.
Hali kama hiyo ilitokea Kenya pale Mchungaji Paul Mackenzie alipowahamasisha waumini wake kufunga hadi kufa kwa madai ya kwenda kukutana na Yesu.
Katika matukio yote hayo viongozi husika walikana kuhusika moja kwa moja, kama ambavyo baadhi ya wanaharakati wa Tanzania wanavyojitenga na yaliyotokea Oktoba 29, 2025 kana kwamba hawakuwepo kabla ya siku hiyo.
Mtu mwenye busara anakubali kuwajibika kwa jambo ambalo ana mchango nalo. Hekima inaonyesha kuwa tukio lolote kubwa hutokana na mchango wa pande mbili au zaidi. Haiwezekani lawama zote zibebwe na upande mmoja pekee.
Ukitaka kujua nani amechangia zaidi katika mgogoro, lazima ujiulize; nani mwenye dhamana ya mwisho? Nani anayenufaika kisiasa au kiuchumi kutokana na tukio hilo?
Kwa mujibu wa Katiba, sheria na mikataba ya haki za binadamu, jukumu la kulinda uhai, mali na usalama wa wananchi ni la serikali. Kauli ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), sasa Makamu wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa hakuna anayeharibiwa zaidi na matukio ya utekaji, mauaji na kupotea kwa watu kuliko CCM na Serikali yake, inaonyesha wazi kuwa matukio hayo hayawezi kuwa chaguo la kwanza kwa chama tawala.
Mantiki hiyo inaibua hoja kuwa huenda yapo makundi yenye masilahi ya kuona Serikali na CCM vinaingia kwenye lawama ili kuharibu taswira yake mbele ya wananchi na jumuiya ya kimataifa.
Katika miaka ya karibuni, baadhi ya nchi za Afrika zimeshuhudia vurugu za uchaguzi zikisababisha serikali za umoja wa kitaifa. Kenya mwaka 2008, Zimbabwe na Zanzibar mwaka 2015 ni mifano ya mazingira hayo. Inawezekana baadhi ya waliokuwa nyuma ya Oktoba 29, 2025 walikuwa wakiamini mazingira kama hayo yangeweza kujitokeza Tanzania.
Athari za tukio hilo zimeonekana pia katika uchumi na diplomasia. Tanzania sasa inaangaliwa kwa shaka katika masuala ya haki za binadamu, uhuru wa kisiasa na uhuru wa kujieleza; mambo ambayo mara nyingi huathiri misaada na mikopo ya maendeleo kutoka mataifa ya nje.

Makala hii inasimama juu ya dhana ya “The Thucydides Trap” iliyoasisiwa na mwanahistoria wa Kigiriki, Thucydides, aliyefuatilia vita kati ya Athens na Sparta. Dhana hiyo baadaye ilipanuliwa na mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Harvard, Graham Allison.
Kwa mujibu wa dhana hiyo, vita au migogoro mikubwa hutokea pale kundi lenye nguvu linapohofia kuondolewa kwenye nafasi yake na kundi jipya linalokua kwa kasi. Hali hiyo husababisha matumizi ya nguvu, tahadhari kali na wakati mwingine hatua zinazozalisha migogoro mikubwa zaidi.
Dhana hiyo inaweza kusaidia kuelewa mvutano uliopo kati ya CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kukua kwa CHADEMA kunazalisha hofu kwa CCM, huku hatua za tahadhari zinazochukuliwa na CCM zikiongeza hasira kwa upande wa upinzani. Tatizo kubwa ni kwamba kila upande unaona lawama ziko kwa mwenzake.
Katika kitabu chake cha Destined for War, Graham Allison anaonyesha kuwa katika matukio 16 ya kihistoria ndani ya miaka 500, migogoro 12 iliishia kwenye vita kwa sababu busara na hekima zilishindwa kutawala.
Matukio ya kabla na baada ya Oktoba 29, 2025 yanafanana kwa kiasi kikubwa na maelezo ya wanafalsafa hao. Leo tunasema walioingia barabarani walikuwa na hasira kutokana na madai ya kunyimwa Katiba mpya au kutoridhishwa na mfumo wa uchaguzi. Lakini kufanya uamuzi kwa hasira si hekima!
Hasira inapozidi, akili na uwezo wa kutafakari hupungua. Ikiwa hasira ndiyo iliyosukuma yaliyotokea Oktoba 29, 2025, basi jamii inapaswa kukubali kuwa wengi waliokuwa barabarani hawakuwa wakitumia utulivu wa kiakili kwa kiwango kinachostahili.
Hakuna anayekubali kuwajibika kwa yaliyotokea. Hivyo jamii inapaswa kukubaliana na matokeo yake, kujifunza na kusonga mbele.

Mwandishi wa makala hii ni mwanachama wa Tanzanian Association of Sociologist anayepatikana kwa simu namba: +255784659187, baruapepe: [email protected]
Ends
