Vita ya Ukraine ni neema kwa kampuni za mafuta

Na Nizar K Visram

Baada ya Urusi kuishambulia Ukraine, Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) wakatangaza vikwazo dhidi ya Urusi, lengo likiwa ni kuibana isiweze kuuza bidhaa zake kama mafuta na gesi katika soko la Ulaya na kwingineko. Urusi ni nchi ya pili duniani katika uzalishaji wa mafuta, ikitanguliwa na Saudi Arabia.

Takriban asilimia 40 ya bajeti yake inatokana na usafirishaji wa mafuta na gesi na soko lake kubwa ni nchi za Ulaya. Asilimia 70 ya gesi na mafuta yanayozalishwa na Urusi yananunuliwa na Ulaya. 

Ndiyo maana katika vikwazo vya Magharibi, bidhaa hizi za nishati ni za kwanza kuzuiwa. Lakini hii si rahisi kwa sababu Ulaya nayo inategemea nishati kutoka Urusi. 

Mkuu wa EU, Ursula Von Der Leyen, amesema vikwazo katika sekta ya nishati maana yake kampuni za EU zitakatazwa kuuza vifaa vya kiufundi kwa ajili ya viwanda vya mafuta na gesi nchini Urusi. 

Na Wizara ya Fedha nchini Marekani imesema itaibana kampuni ya gesi inayomilikiwa na serikali nchini Urusi (Gazprom) isiweze kukopa fedha katika soko la Marekani. Licha ya yote haya Urusi ingali inasafirisha mafuta na gesi.

Ni kwa sababu nchi za Ulaya zinategemea sana gesi kutoka Urusi. Kwa wastani asilimia 35 ya gesi inayotumika katika nchi za EU inatoka Urusi. Mwaka jana kutokana na janga la Uviko-19 uzalishaji wa nishati uliathirika, kwa hiyo bei yake ikaongezeka. 

Hali hii sasa imezidi kuharibika kutokana na vita na vikwazo. Vita ilipoanza tu bei ya gesi iliongezeka kwa asilimia 51.

Machi 2, mwaka huu, wakuu wa EU walisema kuna mkakati wa kupunguza kutegemea nishati kutoka Urusi kwa kuendeleza nishati mbadala, yaani nishati ya jua, bahari, upepo na kadhalika. Lengo ni kupunguza utumiaji wa mafuta na gesi kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2030. Mpaka wakati huo wataendelea kutegemea nishati kutoka Urusi.

Swali ni je, Ulaya itaweza kuacha kabisa kutegemea gesi kutoka Urusi? Hatua zimechukuliwa ili kuagiza gesi (LNG) kutoka Marekani na Qatar. Kwa vile kipupwe kimemalizika, mahitaji ya gesi yatapungua, hivyo haitakuwa shida kwa Ulaya kununua kutoka Marekani badala ya Urusi. 

Lakini tatizo la Ulaya ni kuwa nishati hiyo itakuwa na bei kubwa. Ulaya inaweza kuhimili bei kubwa kwa muda mfupi lakini hali itabadilika iwapo bei itaendelea kupanda hadi kipupwe kitakapoanza tena mwishoni mwa mwaka. 

Kwa sababu Ulaya imekuwa ikitegemea sana nishati hutoka Urusi, wamejenga bomba la masafa marefu (Nord Stream 1) na wamewekeza fedha nyingi. Bomba la pili liitwalo ‘Nord Stream 2’ kutoka Urusi hadi Ujerumani limemalizika kwa gharama ya dola bilioni 11. 

Lilitarajiwa kuongeza maradufu gesi ya Urusi kufikia Ujerumani. Sasa kutokana na vikwazo Ujerumani imeamua kutozindua mradi huo.

Baada ya Urusi kupoteza sehemu kubwa ya soko inasemekana itabidi watafute soko kwingineko duniani. Tatizo ni kuwa Marekani imeiwekea Urusi marufuku ya kutuma na kupokea fedha kupitia benki, kama ilivyofanya kwa Iran, Venezuela na Cuba. Huu ni mfumo wa kimataifa unaotawaliwa na Marekani. 

Kwa Urusi kutumia njia mbadala ni kuingia gharama, na hii maana yake ni kuongezeka kwa bei ya mafuta. Wachambuzi wanasema bei ya mafuta pipa moja huenda ikafika dola 130. Wengine wanatabiri dola 300.

Kutokana na vikwazo Ulaya sasa imeanza kupunguza ununuaji wa bidhaa za nishati kutoka Urusi na badala yake inanunua kutoka Marekani. Maana yake kampuni za mafuta kutoka Marekani zinafaidika kutokana na vikwazo. Vita ya Ukraine ni neema kwao.  

Hata hivyo, haitakuwa rahisi kwa kampuni za Marekani kuchukua nafasi ya Urusi. Bado Ulaya itategemea nishati kutoka Urusi kupitia bomba la ‘Nord Stream 1’ ambalo linaendelea kusafirisha gesi hadi Ulaya. 

Cheniere ni kampuni kubwa kushinda zote nchini Marekani inayoshughulika na kusafirisha LNG. Mara tu baada ya Urusi kuishambulia Ukraine, bei ya hisa ya kampuni hiyo ilipanda kwa asilimia nane. Mwaka jana kampuni hiyo ilichota dola bilioni 15.6. Iwapo vikwazo vitazidi kuibana Urusi ndipo na kampuni hiyo itaongeza faida yake.

Mkuu wa kampuni hiyo, Anatol Feygin, amesema meli za mafuta za Cheniere zimeongezwa tayari kwa kusafirisha mafuta na gesi hadi Ulaya.

Asasi ya mafuta nchini Marekani (American Petroleum Institute – API) inayowakilisha kampuni za mafuta imemuomba Rais Biden aongeze uchimbaji wa mafuta na gesi kwa kuondoa vikwazo vya kisheria nchini Marekani. 

Ikumbukwe kuwa sera ya Biden imekuwa kutopanua uzalishaji wa mafuta na gesi ili kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi. Alipingana na sera ya Trump. Ndiyo maana siku ya kwanza tu alipoingia Ikulu ya White House alipiga marufuku mradi wa bomba la Keystone. 

Hatua hiyo ilifungua mlango kwa Urusi kuiuzia Ulaya mafuta na gesi kwa wingi. Sasa itabidi Biden aachane na sera yake aliyokuwa ameahidi wakati wa uchaguzi.

Mtendaji Mkuu wa API, Mike Sommers, amesema kampuni za mafuta na gesi nchini Marekani; “ziko tayari kuwaunga mkono rafiki zetu wa Ulaya kwa kuwatumia mafuta na gesi.” 

Machi 1, aliandika barua kwa Rais Biden akihimiza uzalishaji wa mafuta na gesi kwa wingi nchini Marekani bila kujali masuala ya tabia nchi.

Wakati Biden akibadili sera yake na kuruhusu uchimbaji wa gesi na mafuta katika maeneo kama Ghuba ya Mexico, amemtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje, Antony Blinken, kwenda Ulaya ambako amewahimiza wakuu wa huko waachane na mafuta ya Urusi. Alifaulu kuishawishi Ujerumani isizindue bomba la ‘Nord Stream 2’ lililokamilika hivi karibuni.

Suala ni iwapo Marekani peke yake inaweza kukidhi mahitaji ya Ulaya na dunia. Ndipo tunaambiwa kuwa Rais Biden huenda akatembelea nchi za Kiarabu na kuzungumza na watawala wa huko ili nao waongeze uzalishaji wa mafuta kukidhi mahitaji na kudhibiti bei isipande sana.

Wakati wa uchaguzi, Biden alimlaumu Trump kwa kuwa na uhusiano wa karibu na mwana mfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman. Sasa Biden naye anatafuta ushirikiano na ‘muuaji’ huyo dhidi ya Urusi. Inasemekana Marekani huenda ikaondoa vikwazo vyake dhidi ya Iran na Venezuela ili wazalishe mafuta kwa wingi.

Hii si ajabu kwani Marekani wana msemo: “Sisi hatuna rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu, bali tuna masilahi ya kudumu.”

Marekani ingependa Ulaya iache kabisa kununua nishati kutoka Urusi, lakini hii haiwezekani. EU imekuwa ikipata asilimia 45 ya gesi, theluthi moja ya mafuta na nusu ya makaa ya mawe kutoka Urusi. Ni dhahiri kuwa EU imekuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara na Urusi. Ili kuvunja uhusiano huu inabidi kutafuta vyanzo mbadala vya nishati hizi. 

Ndipo tunaona Marekani ikijaribu kuchukua nafasi ya Urusi. Tatizo ni kuwa Ulaya haina bandari za kutosha za kupakua gesi na mafuta kutoka Marekani na Uarabuni. Itachukua muda mrefu kujenga bandari za kutosha huko Ulaya. Mpaka wakati huo Urusi itaendelea kusafirisha nishati hadi Ulaya.

Tatizo jingine ni kuwa kampuni kama ExxonMobil, BP, Shell na Total zimefungamana na Urusi. Wamekuwa wakinunua mafuta kutoka Urusi na kuyauza duniani. Wamediriki hata kununua hisa katika kampuni kubwa ya mafuta ya Rosneft inayomilikiwa na Serikali ya Urusi. 

Ili kuachana na Urusi, kampuni hizi itabidi wapandishe bei ya mafuta yao. Ili bei isipande sana wamezitaka serikali zao ziwape msamaha wa kodi. Kama watakubaliwa, basi hii pia itakuwa neema kwao na mzigo kwa walipa kodi. 

Kampuni za mafuta za kimataifa zimenufaika kutokana na vikwazo. Tayari bei ya mafuta imefikia kiwango cha dola 139 kwa pipa. Maana yake ni kuwa bei ya mafuta itaongezeka katika vituo vya petroli. Nchini Marekani tayari imefika dola zaidi ya nne kwa galoni.

[email protected]

0693 555373