Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Arusha

Wistone Massawe amefariki dunia jijini Arusha baada ya kuchomwa kwa kitu chenye ncha kali, ikidaiwa ni wakati alipotoka ndani ya ukumbi wa disko kwenda maliwatoni.

Kwa mujibu wa familia yake, mauti yalimkuta Wistone saa 10 alfajiri ya kuamkia Oktoba 9, 2022 pembezoni mwa Soko la Kilombero katika eneo la soko dogo linalomilikiwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT).

Familia yake pia inadai kuwa Wistone aliyekuwa na umri wa miaka 29, mkazi wa Boma, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro amefariki dunia baada ya kuvuja damu nyingi.

“Alichomwa na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa ni kisu na katika mkono wake wa kushoto lilikutwa jeraha kubwa lililosababisha kuvuja damu nyingi.

“Alikuwa ndani ya Club ya Bills River, maarufu kama Car Wash kuanzia saa tano usiku alipoingia kupata kinywaji hadi saa tisa alipomuaga kaka yake Victor kwamba anakwenda maliwatoni.

“Ndipo ikapita saa nzima bila kurejea na juhudi za kumtafuta zilipoanza bila mafanikio hadi Jumapili ya tarehe 10 tulipomtafuta katika vituo vyote vya polisi, kikiwamo cha Ngarenaro na Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha na kuambiwa twende Hospitali ya Mount Meru, tukaenda katika chumba cha watu majeruhi tukamkosa ila tukamkuta katika chumba cha kuhifadhia maiti,” amesema Glorious Massawe, ambaye ni dada yake Wistone alipozungumza Novemba 10, 2022 na Gazeti la JAMHURI.

Aidha, amesema kaka yake ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha United States International (USIU) cha Nairobi, Kenya hakuwa na ugomvi na mtu yeyote.
Amesema baadhi ya ndugu walionekana eneo ambako Wistone alikutwa na mauti pakiwa pametapakaa damu nyingi katika eneo la juu la kibanda kimojawapo cha biashara kabla ya kudondoka chini baada ya kuishiwa nguvu na kisha kupoteza maisha.

Amesema hadi sasa hawajajua sababu ya ndugu yao kuuawa kwa sababu kabla ya mauti kumkuta alipita kwao na kuwajulia hali huku lengo kuu la kwenda Arusha likiwa ni kuitikia wito kutoka kwa Victor.

Aidha, amesema walinzi wa eneo hilo walidaiwa kutoa taarifa za tukio hilo na polisi walifika saa 12 asubuhi wakati mauti yakiwa yameshamfika Wistone ndipo ikawalazimu kuuchukua mwili wake na kwenda kuuhifadhi.

Katika hatua nyingine, amesema kamera za CCTV zimemuonyesha Wistone alishika mawe mikono yote miwili kwa ajili ya kujihami na waliokuwa wanamshambulia.
Hata hivyo, amesema watu hao walimdhibiti asikimbilie maeneo ya karibu na Hospitali ya Kwa Faza Babu kwa sababu ni karibu na nyumbani kwao ndipo akajikuta anakimbia hadi eneo la Kilombero.

Soma zinazohusiana: Wawili washikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi Dodoma

“Tulifuatilia kamera na tulimuona Wistone akiwa amezungukwa na bodaboda na namba zao zilikuwa kama zimefunikwa hazikuweza kuonekana na alikuwa anapambana nao, pia walimfukuza kwa bodaboda.

“Baada ya kifo hicho Wistone alizikwa Oktoba 14, 2022 eneo la Lyamungo Kati, wilayani Hai na mazishi yake kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo marafiki zake aliosoma nao nchini Kenya,” amesema.

Vilevile amesema Polisi walifanikiwa kupata simu na pochi la Wistone huku kifo chake kimefunguliwa jalada namba AR/RB/12232/2022 na AR/IR/10319/2022 na uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.

Polisi wanena

Licha ya taarifa za awali kudai kwamba mtu aliyefanya mauaji ya Wistone anafahamika ila hajakamatwa, lakini hadi sasa walinzi wawili wa Soko la Kilombero waliodaiwa kutoa taarifa ya tukio hilo bado wanashikiliwa polisi kwa takriban wiki tatu sasa hawajapewa dhamana na hawajafikishwa mahakamani.

Novemba 10, 2022, JAMHURI lilizungumza na mpelelezi wa kesi hiyo katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Rajabu Zubery, lakini hakutaka kuzungumza kwa undani zaidi kwa kile alichodai kuwa suala hilo lipo katika ofisi ya mwanasheria wa serikali.

“Hii ni kesi, uchunguzi unaendelea na kwa sasa shauri lipo kwa mwanasheria wa seikali, ndiyo hicho tu na mengine naomba uwaulize viongozi wangu OC-CID kwa sababu mimi nafanya kazi chini yake hapa Central,” amesema.

Novemba 11, 2022, JAMHURI lilizungumza na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) ya Arusha, Gwakisa Minga, kwanza hakuwa analifahamu hilo tukio, kisha akasema apigiwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha (RPC), Justine Masejo.

“Taratibu zetu zinafahamika, mimi si msemaji wa jeshi, mimi mwenyewe sina cha kukwambia, wala Rajabu hana cha kukwambia, labda mpigie afande RPC ndiye msemaji, lakini kabla haujampigia hilo ni tukio gani? Labda nilifuatilie kwanza hili tukio,” amesema.

Kuanzia Novemba 10-13, 2022, JAMHURI lilimtafuta RPC Masejo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa tukio hilo lakini licha ya kupigiwa mara kadhaa kwa nyakati tofauti kupitia simu ya mkononi, hakupokea.