*Sasa imetimia siku 58 tangu watoweke

*Wazazi wakanusha watoto wao kuuza dawa za kulevya

*Polisi yasema inaendelea na uchunguzi

DAR ES SALAAM

Na Dennis Luambano

Tukio la vijana watano kutoweka na kutojulikana walipo hadi sasa unaweza kusema ni kama maigizo ya sinema za kule Hollywood nchini Marekani.

Kwa sababu mmoja wa shuhuda wa tukio hilo amedai kuwa vijana hao ambao ni Seif Swala, Rajabu Mdoe, Tawfiq Mohammed, Hemed Abbas na Edwin Kunambi walikamatwa na watu watatu wanaodaiwa kuvaa sare za polisi wakiwa wamepakizana katika bodaboda.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo aliyenukuliwa na gazeti moja linalochapishwa kila siku amedai kuwa watu hao walisimamisha gari dogo aina ya IST na baada ya majibizano ndipo risasi mbili zikapigwa hewani kisha mmoja wa watu hao akalipanda na kuliendesha huku kijana mmoja aliyekuwa dereva akaamriwa kushuka na kupanda katika bodaboda. 

Lakini ukweli ni kwamba tukio hilo si maigizo, bali limetokea kweli jioni ya Desemba 26, mwaka jana kama shuhuda huyo aliyekataa kutaja jina lake gazetini anavyodai na hadi leo zimetimia siku 58 tangu vijana hao wadaiwe kukamatwa katika maeneo ya Kamata – Kariakoo jijini Dar es Salaam wakidaiwa walikuwa njiani kuelekea ufukwe wa Kigamboni kusherehekea Sikukuu ya Krisimasi.

Hata hivyo, utata wa tukio hilo unaibua maswali mengi yasiyokuwa na majibu kwa sababu tangu vijana hao wapotee, wazazi wao wamekwenda kuwatafuta katika vituo vyote vya polisi vya Dar es Salaam, kikiwamo cha Oysterbay, Msimbazi, Chang’ombe, Chanika, Tazara, Maturabai, Kilwa Road, Central na katika hospitali zote lakini hawajafanikiwa kuwapata.

Marafiki zao wazungumza

Kutokana na utata huo ndipo Gazeti la JAMHURI nalo likafika Kariakoo katika maeneo ya Mtaa wa Aggrey ambako vijana hao walikuwa wanajishughulisha na biashara za kuuza simu za mkononi na kuzungumza na baadhi ya marafiki zao waliokataa majina yao kutajwa gazetini.

Mmoja wa marafiki wa vijana hao amesema aliwajua siku nyingi wakifanya kwa pamoja biashara ya kuuza simu za mkononi, wala hakuwahi kusikia labda kuna jambo lolote baya wamewahi kufanya.

Rafiki mwingine wa vijana hao amesema ni kweli kwamba tukio hilo limeibua maswali mengi, pia yanamvuruga kwa sababu kama kweli walikamatwa na askari labda walikuwa wanatuhumiwa kwa jambo fulani lakini mbona polisi wanasema hawana rekodi za uhalifu wao?

Mwingine naye anahoji kama katika mahabusu zote za polisi vijana hao hawapo je, wako wapi?

“Sisi tunavyojua kwamba mtu akipotea unaweza kwenda kuripoti polisi kisha ukampata ndugu yako au unaweza ukaenda hospitalini ukakuta labda alipata ajali ukamkuta,” amesema na kuongeza:

“Lakini tangu hao marafiki zetu wapotee kuna maneno mengi yanasemwa hapa Kariakoo kwamba wanatuhumiwa eti walikuwa ni wabeba dawa za kulevya na wamedhulumiana fedha na huyo jamaa waliyekuwa wanambebea ndiye amewateka. Anasema hadi apate fedha zake ndipo atawaachia. Hizo ni tuhuma tu hazijathibitishwa.

“Pengine inawezekana kama kweli kuna huyo anayedaiwa kuwateka kutokana na biashara hizo za dawa za kulevya, sasa hivi atakuwa anafurahia kuona tukio hili linavyoripotiwa, naye hatajwi kabisa, labda fununu kuhusu yeye zikianza kuibuka atajua amebainika na atawaachia rafiki zetu.”

Rafiki mwingine amesema japo taarifa za vijana hao kuhusishwa na ubebaji au uuzaji wa dawa za kulevya hazijathibitishwa na bado zimebaki kuwa ni tuhuma tu lakini si za kupuuzwa.

Rafiki huyo amesema kwa sababu katika maeneo ya Kariakoo katika miaka ya nyuma kumewahi kutokea matukio kadhaa ya vijana wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa hawajulikani walipo, nao wanapata wasiwasi.

“Ni kweli tangu tukio hili litokee kuna maneno mengi yanasemwa na hakuna uthibitisho wowote lakini hatupaswi kuzipuuza hata mara moja. Mfano kule Afrika Kusini kuna watu huwa wanatekwa wanafanywa bondi na fedha zikilipwa wanaachiwa,” amesema na kuongeza:

“Miaka ya nyuma kuna matukio kama haya yamewahi kutokea hapa Kariakoo na kuna vijana walipotea na haijulikani walipo hadi leo. Ni kweli hizo taarifa za wao kuhusishwa na dawa za kulevya zinasemwa hapa katika maeneo ya Kariakoo na Tabata, ingawa bado hazina uthibitisho wowote.

“Licha ya taarifa hizo kusemwa lakini huyo jamaa anayedaiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya kisha kuwateka hao vijana naye anasemwa yuko Kariakoo lakini hawamtaji jina na anadaiwa kuwa baada ya kufanya hivyo ndipo akatuma meseji kwamba hao vijana wamepelekwa Central Polisi.”  

Wazazi wakana watoto wao

kuuza dawa za kulevya

Wakizungumza na Gazeti la JAMHURI kwa njia ya simu wiki iliyopita, baadhi ya wazazi akiwamo Sylivia Quentin ambaye ni mzazi wa Tawfiq, amekanusha taarifa za mtoto wake kutuhumiwa kuuza ama kubeba dawa za kulevya kama baadhi ya watu wanavyodai.

Sylivia amesema hata yeye hizo taarifa za watoto wao kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya amezisoma katika ‘App ya Mange Kimambi.’ 

“Hata sisi wenyewe wazazi inazidi kutuchanganya, kwa mfano mimi inazidi kunichanganya kitu kimoja, mwanangu ninavyomjua hadi yupo katika biashara ya kuuza simu za mkononi mara nyingi alikuwa anakwama masuala ya fedha,” amesema na kuongeza:

“Huwa ananiambia mama leo mambo mabaya, nampa Sh elfu 20 au 30.  Kwa mfano, ilikuwa Novemba 24, mwaka jana nilikwenda pale kwake Mchikichini usiku saa moja nikamuuliza vipi? 

“Akaniambia yuko nyumbani amelala. Nikamwambia toka ndani, akatoka akaja kuniamkia niko katika Bajaj, akaniambia mama niko vibaya kweli. Nikamuuliza vipi, akaniambia sina kitu mfukoni na hata kesho Krismasi sijui itakuwaje na familia yangu itakula nini?

“Nikamwambia basi njoo nyumbani. Akaniambia mama unakuja hauna fedha tena nikupe mzigo wa kuchukua usafiri wa kurudi huku na familia kutoka Chamazi ninakoishi, acha tu hii kesho itapita. Ndipo nikachukua Sh elfu 20 katika pochi langu nikampa na akaniambia basi atakuja tu katika siku mbili hizo. Sasa mtu anayeuza dawa za kulevya anashindwa kupata hata fedha za kula na familia yake?”

Sylivia amesema hata wao wanaambiwa mambo mengi kwamba watoto wamepotea, pengine wananjihusisha na dawa za kulevya.

“Tena kuna kipindi yule mama yake (jina linahifadhiwa) kwa sababu simjui na yeye hanijui ila tulikuwa tunawasiliana kupitia simu lakini kuna siku moja ghafla alinipigia akaniambia mimi ndiye namtangazia mtoto wake kwamba anauza unga (dawa za kulevya),” amesema na kuongeza: “Nikamuuliza umechanganyikiwa wewe mama, nikamwambia mimi si mama wa katika magenge ya kwenye vijiwe na hao waliokwambia ni kina nani wakati mimi sina mazoea katika suala la mwanangu na watu wa mitaani?

“Nikamwambia nakuchukulia hatua ili uniambie ni nani aliyekwambia hilo suala la dawa za kulevya, kwa sababu pengine lipo katika watoto wetu watano au pengine mwanao linamhusu ndiyo maana unapapatika, akanikatia simu halafu baadaye nilivyopiga akawa hapatikani.

“Nikampigia simu mwanaye mwingine nikamwambia naenda kumfungulia mashitaka mama yako kwa sababu naona yeye kuna kitu anakielewa ila anakificha ficha kuhusu sababu ya watoto wetu kupotea. Yule kijana akaniomba msamaha nisifanye hivyo kwa sababu hilo jambo ni nyeti na zito na wamepotea vijana ni jambo kubwa halafu yeye mama analeta maneno kama hayo, yataleta mlolongo mwingine.”

Sylivia amesema pia kuna siku huyo mama ambaye ni mmoja wa mzazi wa vijana hao akamwambia wabadilishe namba za simu wakati wanapotaka kuzungumza masuala ya watoto wao waliopotea.

“Nikamwambia siwezi kubadilisha namba na kwanini nibadilishe, akanimbia ili tukiulizana masuala ya hawa watoto ni bora tutumie namba nyingine tu. Nikamwambia siwezi kusajili au kubadilisha namba mpya, hii ndiyo namba yangu na nitatumia hii kuongea,” amesema. 

“Watoto wote watano walikuwa marafiki na walikuwa wanauza simu pale Kariakoo. Seif Swala anaishi Manzese, Rajabu wazazi wake wanaishi Vingunguti na Sitaki Shari, wazazi wa Hemed wanaishi Tabata. Urafiki wao sikujua umeanza lini na nimekuja kuwajua hao vijana wengine na wazazi wao kupitia tukio hili,” amesema.

Kuhusu mwanaye kupotea, Sylivia, amesema Desemba 25, mwaka jana Tawfiq hakutoka na Desemba 26, mwaka jana pia hakutoka, alikuwa amelala nyumbani huku mkewe akiwa anajitayarisha kwenda kwao Mwanagati katika kikao, ndipo yeye akapigiwa simu waende baharini.

Sylivia amesema kwa mujibu wa mkwewe, Tawfiq akawaambia rafiki zake kwamba yeye hana fedha, ndipo wakamwambia achukue bodaboda awahi Kariakoo watamlipia.

“Baada ya mazungumzo hayo katika simu akamuaga mkewe akatoka na ndiyo imekuwa moja kwa moja hadi leo hajulikani alipo. Tawfiq hana ile kawaida ya kutoka tangu asubuhi asipige simu. Kwanza kwa upande wangu akiamka ananipigia simu kunisalimia na mchana anaweza kunipigia simu nimeshindaje kwa sababu nina matatizo ya moyo na presha,” amesema na kuongeza:

“Hata ile siku aliyoondoka bila kujulikana yuko wapi, mkewe aliposema amekwenda beach, sikuwa na wasiwasi kwa sababu yeye anapenda kuogelea na labda atakuwa amechelewa ndipo hadi Desemba 27, mwaka jana zilipokuja habari kwamba amekamatwa na Desemba 28, mwaka jana ndipo tukaanza kuwatafuta vituo vyote vya polisi na hospitali zote lakini hatujawaona hadi leo.”

Katika hatua nyingine, amesema kabla ya Tawfiq kuanza kuuza simu miaka mitatu iliyopita amefanya kazi katika Kampuni ya Alpha inayojihusisha na uvuvi wa samaki.

“Baada ya kuacha kazi akaanza kuuza simu. Kwa mfano akipata oda, alikuwa ananunua kwa bei za jumla katika maduka ya palepale Kariakoo yanayouza simu, kwa kumuuzia ‘pisi’ moja au mbili na kuna kipindi anachukua simu tano au sita anakuwa nazo kisha anaziuza kwa watu.”

Sylivia amesema mabosi wa kampuni hiyo iliyokuwa eneo la Kipawa, Uwanja wa Ndege bado wana maelewano mazuri na Tawfiq licha ya kwamba ameacha kazi miaka mitatu iliyopita.

“Kwa mfano, kuna kipindi nyumba yetu iliungua moto na yeye vitu vyake vyote viliungua, lakini wale mabosi wake wa zamani walimpa msaada wa fedha na magodoro na vitu vya ndani, ingawa ameacha kazi na wengine wanakuja kumtembelea, yaani ni watu ambao ni kama familia kwa sasa,” amesema na kuongeza: 

“Kwa kweli maelewano na mabosi wake wa zamani bado ni mazuri kama nilivyokwambia. Yaani wako pamoja naye, wanampigia simu na hata akiwa na shida zake ndogo ndogo anawapigia simu wanampa fedha. Saa nyingine Sh elfu 50 au Sh laki moja kama mtoto wake akiumwa.

“Amefanya kazi hapo Alpha na mabosi ni hao hao na wale wa Interchick. Pia wale wana kampuni ya ulinzi na yeye alikuwa sehemu tofauti tofauti, kuna wakati alikuwa Alpha kisha wakampeleka Mafia katika uvuvi na wakamweka Interchick na saa nyingine anawasimamia hao walinzi na wanampa gari anawapitia usiku.” 

Pia amesema bado wanaendelea kuwatafuta watoto wao katika maeneo mbalimbali pamoja na kuzungumza na baadhi ya marafiki zao maeneo ya Kariakoo na mitaani wanaodhani kwamba labda kina Tawfiq wamekamatwa kwa sababu ya kuuza simu zilizotumika katika matukio ya uhalifu.

Aidha, amesema baadhi ya marafiki zake wa mitaani wao wanashangaa Tawfiq kupotea kwa sababu si kawaida, wala hajawahi kuhusishwa katika matukio ya uhalifu au uvunjifu wa sheria.

Naye Longini Kunambi, ambaye ni baba yake Edwin, amesema hata yeye anasikia kwamba watoto wao wanauza dawa za kulevya lakini taarifa hizo hazina ukweli wowote.

“Unajua katika tukio kama hilo ndani yake lazima kila mtu anaongea jambo lake, lakini kwa mtoto wangu shughuli hizo hapana, kwa sababu kama ingekuwa kweli lakini hata kula yake inamshinda.

“Hata wakati mwingine anakuja nyumbani anakula ndiyo anaondoka. Sasa mtu kweli auze dawa za kulevya halafu akose hata fedha za kujikimu mwenyewe? Haiwezekani, na huyo ni kijana wangu katika uzao wa pili, baada ya kumaliza kidato cha nne nikampa msingi wa kununua simu kwa jumla kisha anaziuza rejareja kukidhi mahitaji yake.

“Hayo mambo yakishatokea ni kila mtu sasa anasema jambo lake. Hiyo yote ni maneno tu kwa sababu tabia ya mtu naijua tangu malezi yake, huyo hayuko hivyo, kwa sababy yeye akirudi nyumbani ni kucheza mpira na kukaa tu,” amesema.

Kuhusu mtoto wake kukamatwa, amesema taarifa hizo alizipata Januari 2, mwaka huu kwa sababu Edwin anajitegemea maisha yake peke yake alikopanga chumba eneo la Tabata Shule.

“Edwin alikuwa anaishi peke yake, hana mke na ana umri wa miaka 29, kwa mara ya mwisho Desemba 23, mwaka jana niliwasiliana naye na nikamwambia Krismasi inakuja aje nyumbani tule chakula pamoja, akaniambia hawezi kuja ila atakuja tarehe moja,” amesema na kuongeza:

“Sasa baada ya tarehe hiyo ya 25 hakuja, nikajua ahadi yake ni tarehe moja mwaka mpya. Nilivyoona tarehe moja kimya, kuna mtoto wangu mwingine aliyemfuata Edwin akaniambia baba nikimpigia simu kaka hapatikani. Nikamwambia kwa sababu anakaa peke yake, basi nenda kamuone. Nikampa nauli akaenda kule. Nikapata taarifa kutoka kwa mama mwenye nyumba kuwa tangu tarehe 26 hajarudi.

“Akajua yuko kwa wazazi anakula sikukuu. Nikamwambia hapana, ndiyo maana tunamtafuta hapatikani. Ikabidi sasa tuanze kumtafuta kwa marafiki zake wa karibu anaofanya nao shughuli pamoja za kuuza simu. Baadaye mwanangu akanipatia namba ya rafiki yake, tukampigia akasema alikuwa amesafiri, lakini nikapata taarifa hizo kwamba wamekamatwa vijana watano.

“Kisha nikaomba namba ya simu ya jamaa mwingine waliokuwa wote, huyo naye akasema hata yeye alipata taarifa kwa sababu anakaaa Mbagala-Mbande na siku hiyo alirudi mapema.”

Kunambi amesema Januari 3, mwaka huu akaanza kuwatafuta watoto wao kwa kuanzia Kituo cha Polisi Gongo la Mboto, Kituo cha Polisi cha Msimbazi kisha akaenda Tabata kwa mama mwenye nyumba anapoishi Edwin.

Vilevile amesema akaenda kwa mjumbe, Serikali ya Mtaa, kisha akatoa taarifa Kituo cha Polisi Tabata na wakampa maelekezo atembelee vituo vyote vya polisi vya hapa jijini Dar es Salaam na hospitalini, lakini hakupata mafanikio yoyote.

Amesema akarudi tena Kituo cha Polisi Tabata kuchukua ‘RB’ na kwa kushirikiana na wazazi wengine wa vijana hao wakaenda hadi Kamata – Kariakoo kulipotokea tukio hilo kuulizia kwa mashuhuda lakini hakuna jambo lolote walilolipata.

Polisi nao wafunguka

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI hivi karibuni kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema wao wanaendelea kufanya uchunguzi wa kawaida na ule wa kisayansi (cyber) katika tukio la vijana hao kupotea.

“Polisi tunafanya kila jitihada kufuatilia taarifa za kupotea vijana hao kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kujua vijana hao wako wapi au wamekwenda wapi? Tunafanya ule uchunguzi wa kawaida na cyber,” amesema Muliro na kuongeza:

“Kazi yetu ni kuchunguza, tumekutana na wazazi wa hao vijana na tumerekodi maelezo yao na huo ni mfumo wa kijeshi wa kawaida mtu akitoa taarifa yoyote inapokelewa, vituo vyote, kwa kawaida watu wakikamatwa wanapelekwa mahabusu kwa hiyo nilichokifanya ni kuuliza vituo vyote vya polisi kama kuna watu wamekamatwa.

“Watu wakikamatwa wanajulikana, tunawapeleka mahabusu, majina hayo hayapo katika vituo vyote vya polisi vilivyopo Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na wazazi wa hao vijana wakapita na wakajiridhisha kwamba hawapo katika vituo hivyo, kwa sababu mtu akipotea humtafuti polisi tu, maana kuna ajali lakini wakaniletea taarifa kwamba hata hospitalini nako wamekwenda wamewakosa.”

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amenukuliwa wiki iliyopita na gazeti moja linalochapishwa kila siku kwamba ameagiza kufunguliwa kwa jalada la uchunguzi kwa vijana hao wanaodaiwa kupotea.

“Tukio hilo nilielezwa lakini niliwaambia wafungue jalada la uchunguzi ili tufuatilie, kwa hiyo makao makuu wanafuatilia suala hilo ili tuweze kujua kuna nini,” amesema Sirro.

By Jamhuri