Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Katika kipindi cha miaka miwili mfululizo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS Tanzania imepata faida kutoka sh.bilioni 539 hadi sh.trilioni 1.5 sawa na asilimia 185.

Hayo yameelezwa Dar es Salaam leo Julai 31,2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala, wakati akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo ya habari nchini.

Migangala amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne mfululizo, Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS Tanzania imepata faida na mtaji unafikia sh.trilioni 1.5 kutoka sh.bilioni 2980 zilizopatikana mwaka 2014 hadi 2019.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa kiasi hicho cha faida ni kikubwa na hakijawahi kupatikana tangu kampuni hiyo ianzishwe ambapo lengo la awali la UTT AMIS ilikuwa ni kupata faida kutoka Sh.bilioni 290 hadi 485 kwa kipindi cha miaka mitano.

Mkurugenzi Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo mvalimbali vya habari leo Julai 31, jijini Dar es Salaam.

“Lakini mpaka sasa tuko kwenye mwaka wanne tumeshavuka lengo na kufikia shilingi trilioni 1.5 kutokana na mafanikio haya tumejiongezea lengo ifikapo mwakani tutakapokamilisha mwaka wa tano tuwe tumefikia shilingi trilioni 1.7,” ameeleza Migangala.

Amesema kuwa sababu nne za kupatikana kwa mafanikio hayo ya haraka kuwa ni kuboreshwa zaidi mifuko saba ya uwekezaji ya kampuni hiyo.

Amesema kuwa mojawapo ni uwekezaji kwenye teknolojia hali iliyosaidia huduma za kampuni hiyo kupatikana sasa hadi kwenye simu za kiganjani kupitia mitandao yote ambapo mtu anaweza kujisajili,kuwekeza na kufuatilia uwekezaji wake.

“Lakini pia tumeunganisha huduma zetu na benki ambapo mtu akienda kuwekeza kupitia benki moja kwa moja tunapata taarifa zake haina haja ya kusubiria risiti ya benki kama ilivyokuwa zamani,” alisema.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa awali uwekezaji katika mifuko hiyo ulikuwa na masharti magumu lakini sasa yamerahisishwa ili kuvutia zaidi wawekezaji.

Baadhi ya wahariri wakifuatilia mada mbalimbali katika kikao kazi na Kampuni ya Uwekezaji UTT AMIS jijini Dar es Salaam.

“Mwanzo kulikuwa na masharti magumu lakini pia kianzio cha uwekezaji kilikuwa ni shilingi milioni tano lakini sasa tumeshusha hadi kufikia 100,000. Pia nyongeza ya uwekezaji ilikuwa inaanzia shilingi milioni moja lakini sasa imeshushwa hadi 10,000 tu,” ameeleza.

Migangala ametaja eneo lingine la mafanikio kuwa ni kutoa faida kubwa kwa wawekezaji ambapo mwaka huu mfuko wa Umoja umetoa faida kwa mwekezaji ya asilimia 11, Wekeza Maisha asilimia 12.49, Mfuko wa Watoto asilimia 12.41, Mfuko wa Kujikimu asilimia 13.6, Ukwasi asilimia 12.49 na hatifungani asilimia 12.24.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS David Mbaga alichambua mifuko hiyo kuwa Mfuko wa Umoja kazi yake ni kuwekeza fedha za wawekezaji kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na ni kwa wale wanaowekeza kwa muda mrefu.

Amesema wakati mfuko huo unaanzishwa kipande kimoja cha Umoja kilikuwa sh 100 lakini leo thamani yake imepanda hadi kufikia Sh 932.

Kuhusu Mfuko wa Wekeza Maisha ni wa uwekezaji wa muda mrefu wa hadi kufikia miaka 10. Mfuko wa Watoto ni kwa ajili ya kuwajengea maisha bora watoto hususani katika eneo la elimu na afya.

Amesema Mfuko wa Jikimu ambao ndio maarufu hutoa mafao kila baada ya miezi mitatu, mfuko wa ukwasi ambao hauna hisa ambao unawekezaji baada ya muda unalipwa faida na hati fungani baada ya kuwekeza mwekezaji analipwa kila mwezi faida.

Aidha, alisema kwa sasa mfuko huo umekuwa kwa kasi ambapo hapo awali kulikuwa na akaunti za uwekezaji 500 kwa mwaka lakini mwaka huu zimefunguliwa akaunti 47,000 kutoka akaunti zilizofunguliwa mwaka jana 29,000. Pia una wawekezaji wanaofikia 300,000.

“Tumeanzisha progamu mbalimbali za elimu kuhamasisha Watanzania hususani vijana kuwekeza na UTT AMIS kwa faida yao ya baadaye. Na tuna mpango wa suala hili kufundishwa hadi shule za msingi na Sekondari,” amesema Mbaga.

By Jamhuri