Ving’ora na taa za vimulimuli marufuku kama huna kibali maalum – Polisi

Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani limewataka wale wote waliofunga ving’ora na taa za vimulimuli kwenye magari na pikipiki zao pasipo kuwa na kibali maalumu kutoa mara moja kabla ya ukaguzi haujaanza na atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake .

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani SACP Ramadhan Ng’anzi amesema kumeibuka wimbi la watu wanaitumia vyombo vya moto ikiwemo magari au pikipiki ambao hawana kibali chochote kununua ving’ora na taa za vimulimuli kufunga na kutembea navyo barabarani hivyo kuanzia sasa wameagizwa watoe mara moja kabla ya kuanza msako.

”Ving’ora na taa za vimulimuli hufungwa katika pikipiki iwapo imetengenezwa kwa matumizi maalumu kadri sheria ya usalama barabarani sura ya 168 kama ilivyopitishwa mwaka 2002 kufungua cha 54 (2)(5) king’ora kitafungwa kwenye gari au pikipiki za dharura (emergency motor vehicle) ambapo hutumika katika misafara ya viongozi Zima Moto na magari ya hospitali ” amesema Ng’anzi.

Sambamba na hayo amesema kuwa wapo baadhi ya watu ambao wamegeuza ving’ora na taa za vimulimuli kuwa fasheni katika magari na pikipiki zao hivyo kwa kuwa utaratibu maalumu umewekwa Jeshi la polisi litaanza kuwakamata watu binafsi, na makampuni au taasisi zinazofanya shughuli za kufunga vifaa na kuwapatia adhabu ikiwemo kulipa faini ya tozo.

Sambamba na hayo ameagiza baadhi ya watu wamejenga utamaduni ambao wamejihalalishia wenyewe kuweka namba za bandia katika magari yao hivyo nao wazitoe mara moja kwani operesheni kabambe itaendeshwa kwani watakaosalimika ni wale wenye magari akitokea Zanzibar lakini wakiwa na kibali maalumu .