Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini nchini wakiwemo wa Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqaama Tanzania waongeze juhudi katika kutoa mafunzo ya dini ili kupunguza au kuondoa kabisa mmomonyoko wa maadili unaoikabili jamii.

Waziri Mkuu amesema viongozi wa dini, viongozi wa umma wana wajibu mahsusi wa kuilea jamii kwa kutoa mafundisho sahihi na endelevu ya dini ili kuiwezesha kutambua na kufuata yote yaliyo mema kama ilivyo amrishwa na mwenyezi Mungu na kuacha kabisa yote mabaya yanayomchukiza.

Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally, baada ya Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Istiqama Tanzania, uliyofanyika katika Hoteli ya  Ledger Plaza Baharı Beach, jijini Dar es Salaam Novemba 5, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Jumuiya ya Istiqaama na Jumuiya nyingine mbalimbali za dini ambazo zimejikita katika kutoa mafunzo ya kiroho yanayoifanya jamii kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuwawezesha wananchi kuishi kwa amani.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 5, 2022) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya Istiqaama Tanzania uliofanyika ukumbi wa Mikutano wa Bahari Beach jijini Dar es Salaam. Amesema hivi karibuni jamii imeshuhudia vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili miongoni mwa Watanzania.

“Sote tumekuwa mashuhuda wa kuongezeka kwa baadhi ya vitendo viovu kama vile wazazi kuuawa na watoto wao, wanawake kuuawa na waume zao na vijana kutowaheshimu watu wazima, uvaaji wa mavazi yasiyo na stara hususan kwa wasichana na wavulana na matumizi ya dawa ya kulevya.”

“Katika suala hili la malezi, niendelee kuwasihi viongozi wa taasisi za dini kutumia vema huduma za kiroho na ibada kujenga jamii yenye tabia njema, utii pamoja na kuheshimu mamlaka zilizopo, Kwa kufanya hivyo, tutawasaidia vijana wetu kuwa raia wema, wazalendo na wenye manufaa kwa nchi yao.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Sad Al Shaidhany, baada ya Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Istiqama Tanzania, uliyofanyika katika Hoteli ya  Ledger Plaza Baharı Beach, jijini Dar es Salaam Novemba 5, 2022. Katikati ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Seif Ally Seif. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa taasisi za dini nchini, kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utoaji wa huduma za jamii hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali imewekeza katika miundombinu bora ya afya, elimu na maji pamoja na ongezeko la Watumishi katika maeneo ya kutolea huduma nchini.

Awali, akizungumza kwa niaba ya waumini wenzake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Istiqamaa, Sheikh Seif Ally Seif, aliishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwa taasisi za dini na alimpongeza Rais Mheshimiwa Samia kwa kusimamia haki upendo na kujenga umoja wa kitaifa, hivyo kuifanya nchi kuendelea kuwa katika uelekeo mzuri.

Mwenyekiti huyo alisema lengo la jumuiya ya Istiqaama ni kutoa mafundisho ya kidini na kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama elimu ambapo wana shule 14 Tanzania Bara na Zanzibar, pia wanatoa huduma za afya pamoja na uchimbaji wa visima vya maji.

By Jamhuri