Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Viongozi wa Chama na Serikali waliopata fursa ya kuzungumza wakati wa ibada ya mazishi ya aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi (mstaafu) wa Jeshi la polisi nchini na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha, Marehemu Zelothe Stephene Zelothe kuwa alikuwa ni kiongozi mwadilifu na mwenye nidhamu, aliyewapenda anaowaongoza na asiyependa makuu.
Viongozi hao licha ya kuhuzunishwa na kifo cha Zelothe lakini wamekiri kuendelea kuyaishi maisha ya yake, maisha ambayo wengi wametoa shuhuda za kuwa alikuwa mwenye nidhamu, muadilifu na mtiifu kwa watu wa kila rika.
Makamu Mwenyekitia wa CCM Taifa Tanzania Bara Abdulrahman Kinana, amesema kuwa, Zelothe alikuwa kiongozi mwenye uwezo wa kuongoza bila kujali mamlaka na vyeo alivyokuwa navyo kwa kuwa alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa wengine.
Ametoa mfano alioutoa Hayati baba wa Taifa Mwalimu JK Nyeree, kuwa uongozi ni tabia sio usomi wala elimu, kinachomtofautisha kiongozi na watu wengine ni tabia na sio wadhifa alionao, tabia ambazo amekiri alikuwa nazo Zelothe licha ya kuwa na nyadhifa kubwa serikalini na kwenye Chama alikuwa ni mnyenyekevu na mwadilifu mwenye kufanyakazi kwa kuweka mbele uzalendo.
“Wapo wasomi wameshindwa kuwa viongozi wazuri na wapo wasiosoma wamekuwa viongozi wazuri, Zelothe alishika uongozi kwa nyadhifa nyingi na za juu serikalini lakini hukuwahi kuwa na majivuno, aliendelea kuwa mnyenyekevu kwa watu anaowaongoza na watu wa kawaida, hii ni tabia ya kuigwa na viongozi wengine tuliobaki” amebainisha Kinana.
Akitoa salamu za serikali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene, licha ya kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa ajili ya maisha ya Mzee Zelothe, amesema kuwa, kupitia historia ya maisha ya Zelothe iliyoelezewa na watu wa makundi mbalimbali, inaonyesha wazi kuwa alikuwa ni mtu wa tofauti anayeweza kufananishwa na mtumishi wa Mungu na sio Polisi.
“Tumeshuhudia sura ya maisha ya Zelothe yaliyobeba dhamana nyingi ikiwemo baba, mlezi, mwalimu, kiongozi, Jemadari aliyewahudumia watu bila kujali hali za watu anaowahudumia, naweza kusema katika maisha yake ameandika hadithi nzuri, ambayo kila mmoja anaweza kuihadithia” amesema Simbachawene.
Naye Mwenyekiti wa Wabunge wa mkoa wa Arusha na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Steven Kiruswa ametoa pole kwa familia na kuelezea, msiba wa mzee Zelothe ni wa wana Arusha wote, Arusha imepoteza kiongozi hodari na makini, asiye na makundi mwenye kupenda kuunganisha watu bila kusita kusema ukweli pale inapostahili.
“Tumepoteza Mwenyekiti ambaye alitulea kwa upendo, alituunganisha wanachama, na mkoa ulitulia kisiasa, Zelothe ameondoka, tushirikiane na kuendela kumuomba Mungu atupe mtu sahihi kama Zelothe” amesema Kiruswa
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mongella amesema kuwa, mkoa wa Arusha umepata pigo, kwa kupoteza kiongozi makini ambaye alipenda uwazi na uwajibikaji unao shirikisha watu kama timu,kiongozi ambaye hakuogopa kusema ukweli.
“Mimi binafsi alikuwa ni rafiki yangu na rafikii asiyetaka kitu kutoka kwa mtu ,zaidi asiyogopa kukwambia ukweli, kimsingi nilijifunza mambo mengi kutoka kwakwe ikiwemo maadili ya uongozi, tunaahidi kuyaenzi yote yaliyo mema” amesema Mongella.