Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Serikali za nchi za Tanzania na Ujeruman zimesema zitafanya mazungumzo yatakayowezesha mabaki ya miili ya Watanzania walipoteza maisha wakati wa ukoloni yaliyopo nchini Ujerumani yanarejeshwa nchini.

Akizungumza leo Oktoba 31, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema katika mazungumzo yao wamezungumza masuala mbalimbali likiwemo kurejeshwa kwa mabaki hayo.

Kwa muda mrefu mabaki ya miili hiyo ya Watanzania imehifadhiwa katika makumbusho mbalimbali nchini Ujerumani na sasa uamuzi wa kuyarejesha umefikia hatua nzuri na hatimaye mabaki hayo yarejeshwe na kukabidhiwa kwa ndugu.

Ikumbukwe kwamba baadhi ya mabaki hayo ni ya miili ya machifu na viongozi waliokuwa vinara katika vita vya Tanganyika dhidi ya Ujerumani (Maji Maji).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Frank-Walter Steinmeier mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba, 2023.

“Nakushukuru Rais Frank – Walter Steinmeier kwa kukubali mualiko wangu wa kuja kufanya ziara nchini, huu ni uthibitisho wa uhusiano mzuri kwa miaka miaka 60 baina ya nchi hizi.

“Katika mazungumzo yetu tumejadili masuala mbalimbali lakini tumezungumzia kuhusu mabaki ya wapendwa wetu walioko Ujerumani , tunaendelea kuzungumza ili mabaki ya miili ya wapendwa wetu irejee nyumbani Tanzania,” amesema.

Wakati anazungumzia mabaki hayo , Rais Dk.Samia amesema anajua kuna familia ambazo zinasubiri mabaki ya miili ya ndugu zao ambayo yapo kwenye makumbusho za Ujerumani, lakini sasa wanakwenda kuyazungumza ili yaweze kurudishwa Tanzania.

Akielezea zaidi kuhusu mazungumzo kati yake na Rais Steinmeier, Rais Samia amesema wamezungumza kuhusu kuendelea kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili sambamba na kushirikiana katika nyanja mbalimbali kama elimu, afya, uhifadhi , kilimo, sekta ya ubunifu na maeneo mengine ambayo wamekuwa wakishirikiana.

Aidha Rais Samia ameishukuru nchi ya Ujeruman kwa misaada mbalimbali waliyoitoa na wanayoendelea kuitoa kwa ajili ya kusaidia maeneo mbalimbali akitolea mfano kuwa katika eneo la Bima ya Afya kwa Wote nchi hiyo iliahidi kusaidia lakini wanaendelea na ujenzi wa hospitali kubwa Dodoma.

“Ujeruman wamekuwa wakitusaidia katika maeneo mbalimbali, mbali ya ujenzi wa hospitali pale Dodoma lakini Ujeruman wametusaidia kujenga Hospitali Lugalo.Pia wamekuwa wakitusaidia katika uhifadhi katika hifadhi ya Serengeti na Selous.

Kwa upande wake Rais wa Ujeruman Steinmeier amemshukuru Rais Dk.Samia kwa kumualika kufanya ziara nchini huku akielezea namna ambavyo wamekuwa na mazungumzo mazuri yanayolenga kuimarisha uhusiano na kushirikiana katika sekta mbalimbali.

Kuhusu mabaki ya miili ya watanzania yaliyoko nchini Ujeruman amesema hilo ni jambo ambalo linazungumzika na watafikia pazuri huku katika hilo litaambatana na kupeleka Ujerumani taarifa za hali za wahanga wa vita vya majimaji ambao natarajia kukutana nao kesho.

” Nitakwenda kukutana na wahanga wa vita , nitawasikiliza na yale ambayo watanieleza nitakwenda nayo Ujeruman ili kufikisha ujumbe wao, “amesema huku akieleza ni vema pia nchi hizo kutosahau historia ya mambo yaliyopita na kubwa zaidi kudumisha uhusiano .

Pia amesema katika eneo la ubunifu, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwasaidia wabunifu wachanga ili kukuza bunifu zao lakini amesisitiza kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali.

Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Frank-Walter Steinmeier akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba, 2023. Pembeni yake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo Rasmi na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Frank-Walter Steinmeier, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Frank-Walter Steinmeier mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba, 2023.