Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashidi Shangazi, mkoani Tanga ameahidi kushirikiana na wadau wa habari kuhakikisha tasnia hiyo inakuwa na sheria bora.

Ameyasema hayo wakati alipokutana na timu ya Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma jana.

Shangazi ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, alieleza ukakasi uliopo kwa baadhi ya vipengele vya sheria vilivyomo kwenye muswada wa sheria uliwasilishwa bungeni Februari 10, 2023.

Akizungumzia hoja ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, kuhusu kuwekwa ukomo wa chini wa kiwango cha adhabu, Shangazi amesema jambo hilo hata mahakimu linawapa tabu.

“Tuliwahi kukutana na mahakama ambapo mahakimu tuliwaeleza watuambie baadhi ya changamoto wanazozipata katika utendaji kazi wao.

“Moja ya changamoto walilyoeleza ni sheria kuwawekea ukomo wa chini wa adhabu, jambo hilo wanasema linawapa tabu sana,” alisema.
Kauli hiyo ilitanguliwa na ya Balile aliposema, sio kila kisa la mwandishi linastahili kifungo kama ambavyo sheria inaelekeza.

Balile alisema, awali sheria ilikuwa inaelekeza kifungo kisichopungua miaka mitano na baada ya vikao na serikali, muswada uliowasilishwa bungeni umepunguza na kuweka miaka mitatu.

“Sio kila kosa kwa mwanahabari linahitaji kifungo, makosa yanatofautiana, wakati mwingine kosa linaweza kuhitaji mtu kupewa adhabu ya mwezi mmoja ama kifungo cha nje.

“Hii inategemea na uzito wa kosa, lakini sheria ilivyowekwa, inamlazimisha jaji kutoa kifungo kisichopungua miaka mitatu hata kama kosa ni dogo linalohitaji onyo,” alisema Balile.

Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TEF alimfafanulia Shangazi dhana ya sheria inayompa mamlaka Waziri mwenye dhamana kuzuia machapisho kutoka nje na athari yake.

“Kwanza katika ulimwengu wa sasa machapisho yapo kwenye mitandao, kuweka sheria kuzuia machapisho kunalenga dhana ya kuonesha kukabiliana na uhuru wa habari.

“Waziri anaweza kuamua kukataa kuingizwa labda gazeti lolote mfano la Kenya ama nchi nyingine kwa sababu tu, halitaki kutokana na mambo yake binafsi,” alisema Meena.

Hata hivyo, Shangazi alieleza kuwa, kwa wakati uliopo ni vigumu kuzuia machapisho hivyo sheria hiyo kuwa ngumu katika utekelezaji wake.

Saumu Mwalimu kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) alieleza kwamba, Mbunge Shangazi amewaeleza kwamba, mchakato wa sheria ya habari umekuja wakati mzuri kutokana na Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwa na utayari.

“Waziri Nape amefanya kazi sana mpaka kufikia hapo, naamini bado mnayo nafasi ya kukutana naye maana ni muelewa na ana utayari,” alisema.

Salome Makamba, amesema asilimia 35 ya mapendekezo ya wadau wa habari ni machache, walau yangevuka asilimia 50 ama 60.

Na kwamba, kuna kila sababu ya kuishauri kamati kujumuisha mapendekezo yaliyoachwa kadiri itavyowezekana ingawa sio rahisi kubeba yote.

“Nimejifunza zaidi kutoka kwenu lakini kuna jambo tunapaswa kufanya ili kuwa na sheria bora. Asilimia 35 ya mapendekezo iliyoingizwa kwenye muswada ni ndogo, walau ingekuwa zaidi ya silimia 50 ama 60 ingawa sio rahisi kupita mapendekezo yote.

“Tutaishauri vizuri kamati pale tutapokutana ili kuangalia yale yaliyoachwa nje na umuhimu wa kuyajumuisha kwenye muswada,” alimema Salome.

Mbunge Justin Ngamoga, wa Kilolo akizungumza na James Marenga kutoka MISA TAN na Deus Kibamba ambaye ni mjumbe wa CoRI alisema, ni muhimu sana kuangalia marekebisho yake.

Mbunge huyo alisema, eneo la habari ni eneo muhimu kwa jamii nan chi hivyo, inahitaji uangalizi wa kutunga sheria zitazowezesha uhuru ambao utaisaidia jamii na serikali.

“Najua eneo la habari lina umuhimu mkubwa kwa nchi, sheria zake zinapaswa kutoa nafasi katika utendaji uliotukuka. Tutaangalia na kuishauri kamati namna bora ya kuwa na sheria zenye uahi mrefu kwenye tasnia ya habari,” alisema.

By Jamhuri