Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Baadhi ya wadau wa mchakato wa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari wamewasili mkoani Dodoma kwa nia ya kukutana na wabunge ili kufafanua mapendekezo ya vipengele vya sheria viliyoachwa kwenye muswada wa habari uliowasilishwa Februari 10, 2023.

Akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani humo, Deus Kibamba ambaye ni Mhadhiri wa Masuala ya Diplomasia pia Mjumbe wa Umoja wa Wadau wa Kupata Habari (CoRI), amesema lengo kubwa la kukutana na wabunge ni kufafanua zaidi mapendekezo ya mabadiliko ya vipengele vya sheria viliyoachwa nje.

Kibamba amesema kuwa sababu ni kuhakikisha wabunge wanaelewa dhamira ya wanahabari na uhuru wa habari nchini.

“Tumekuja kukutana na wabunge ili tueleze baadhi ya vifungu vilivyoachwa nje ni muhimu kuingia kwenye muswada” amesema.

Naye James Marenga, MISA TAN amesema wabunge ndio watunga sheria, na muswada umeishafikishwa kwao hivyo ni muhimu kukutana nao.

“Tulianza na serikali na wakatusikiliza, wakawasilisha kile walichowasilisha bungeni.

“Ni wakati sasa na sisi kukutana na wabunge kwa ufafanuzi zaidi, naamini wabunge ni waelewa na watatuelewa,” amesema Marenga ambaye pia ni wakili wa kujitegemea.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Neville Meena, amesema kinachofanywa na CoRI (kukutana na wabunge) ni jambo la kawaida pale kunapokuwa na hatua za utungwaji wa sheria.

“Ni suala la kawaida pale panapokuwepo na hatua za utungwaji wa sheria, taasisi husika ikawa inatoa ufafanuzi zaidi juu ya kile inachopigania.

“Tumeona ni fursa kwetu sasa kukutana na wabunge ili kuwaeleza nini tunapigania na kwa nini. Nafasi hii tunapaswa kuitumia vizuri na ndio maana tupo hapa Dodoma,” amesema.

Baadhi y wajumbe hao wa CoRI ni pamoja na Deus Kibamba; Saumu Mwalimu, Baraza la Habari Tanzania (MCT); Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN).

Akizungumza kwenye mkutano wa wadau hao uliofanyika jijini Dar es Salaam Februari 20, 2023, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema, ni muhimu kwa CoRI kukutana na wabunge ili kushawishi baadhi ya vipengele ‘vilivyotelekezwa’ kwenye muswada huo.

“Tutakwenda kuzungumza na wabunge kuhusu athari zinazoweza kuifika tasnia ya habari kutokana na baadhi ya vifungu vilivyomo kwenye sheria na marekebisho yaliyofanywa na serikali ili watusaidie kurekebisha siku wakianza kujadili bungeni,” alisema.

Hata hivyo amesema, Bunge la sasa ni la bajeti lakini linaweza kubadili ratiba yake mwishoni na kuamua kupitia mapendekezo ya marekebisho ya sheria yaliyowasilishwa katika bunge lililopita.

“Tunafanya hivyo kwa kuwa huwenda nafsi ikapatikana katika bunge hili, lakini ikishindikana basi itakuwa kwenye Be unge la Septemba mwaka huu,” amesema.

Miongoni mwa vipengele ambavyo CoRI wanapenda viingizwe kwenye muswada wa sheria kabla ya kujadiliwa ni pamoja na sehemu ya saba inayohusu adhabu na makosa yake ambapo walipendekeza kupungua adhabu hasa kwa makosa yanayohusu kitaalamu.

Walipendekeza Serikali iondoe ukomo wa chini wa adhabu kwa vifungu vyote kwa kuwa inambana hakimu au jaji kuamua vinginevyo.

Na kwamba, sheria nyingi kwenye mataifa yaliyoendelea zinaweka ukomo wa juu wa adhabu kwa kuwa inatoa fursa kwa jaji au hakimu kutoa adhabu kulingana na mazingira ya kesi husika.

Pia wanaeleza kifungu cha 7(2) kinaeleza kuwa serikali inaweza kutoa agizo habari fulani kuchapisha au kutangaza habari kwa kuwa ina umuhimu kwa Taifa CoRI wanaeleza kifungu hicho ni kuingilia uhuru wa uhariri kwa kuwa, uhariri unafanywa nje ya chumba cha habari ambacho kina watu wenye weledi na uzoefu mkubwa.


CoRI wanalalamikia kifungu cha 5(e)a,b kinachohusu utoaji wa leseni ambapo Mkurugenzi wa Habari (Maelezo), anaweza kukataa maombi ya leseni au kuhuisha kulingana na matakwa yake.

Pia kinampa mamlaka ya kusitisha leseni wakati wowote anapoona chombo husika hakina mwenendo anaoutaka yeye.

By Jamhuri