WADUNGUAJI HATARI KUMI DUNIANI

Rob Furlong (7)

Anayeshikilia namba saba katika orodha ya wadunguaji kumi hatari duniani ni Rob Furlong. Huyu alikuwa ni koplo katika jeshi la Canada.

Anashikilia kuwa mdunguaji aliyeweza kumlenga mtu na kumpiga katika umbali mrefu kuliko wadunguaji wengi. Rekodi zake zinaonyesha kuwa aliweza kumlenga na kumdungua mtu aliyekuwa umbali wa maili 1.51 au meta 2,430. Umbali huu ni kama kilometa mbili na nusu hivi.

Rekodi hii aliiweka mwaka 2002 aliposhiriki katika operesheni Anaconda. 

Timu yake ya wadunguaji ilikuwa makoplo wawili, na master watatu. 

Katika tukio lililoweka rekodi, Furlong na timu yake waliwagundua wanamgambo watatu wa kundi la Al-Qaeda wakiwa wamejificha pembeni ya mlimani wakiwavizia wanajeshi wa Marekani ili wawashambulie. 

Baada ya kuwaona wanamgambo hao, Furlong akainua bunduki yake na kuweka risasi ndogo aina ya A-MAX, ambazo zina sifa ya kutoyumbishwa na upepo zinapopigwa kutoka kwenye bunduki.

Akamlenga mmoja wao kumpiga risasi lakini akamkosa. Risasi yake ya pili ikapiga begi alilokuwa amebeba mmoja wa wanamgambo hao.

Wakati wanamgambo walipobaini kuwa walikuwa wanashambuliwa, Furlong tayari alikuwa ameshapiga risasi ya tatu mara ya tatu. Mapigo ya risasi hizo yalipishana kwa muda wa sekunde tatu kila moja.

Wataalamu wa udunguaji wanaamini kuwa ukizingatia umbali huo, mdunguaji alikuwa anahitaji muda mrefu sana wa kulenga shabaha, lakini Furlong aliweza kupiga risasi mfululizo na kumdungua mwanamgambo.

Risasi yake ya tatu ilimpiga mmoja wa wanamgambo hao kwenye paji la uso na kumuua palepale. Vilipofanyika vipimo baadaye ilibainika kuwa mtu yule alikuwa umbali wa meta 2,430.

Rob Furlong alizaliwa Novemba 11, 1976. Kati ya Machi 2002 hadi Novemba 2009, alishikilia rekodi ya kuwa mdunguaji aliyemlenga na kumuua mtu katika umbali mrefu.

Rekodi hiyo ilidumu kwa miaka saba na ilivunjwa na Craig Harrison aliyefanikiwa kumdungua mtu katika umbali wa meta 2,475 akitumia bunuki aina ya L115A3 Long Range Rifle.

Furlong alijiunga na jeshi baada ya kusisimka alipoiona picha ya video ya wanajeshi.

Desemba 2003, Furlong na wenzake kadhaa walitunukiwa tuzo na jeshi la Marekani kutokana na ushujaa waliouonyesha katika operesheni Anaconda iliyoanza Machi 2 hadi 11, 2002. 

Baada ya kuacha kazi jeshini, Furlong alienda kuishi Edmonton, Alberta na kujiunga na Jeshi la Polisi katika eneo hilo mwaka 2004, ingawa ndoto zake zilikuwa ni kujiunga na wapelelezi wa jeshi.

Mwaka 2012, Furlong alifukuzwa kutoka Jeshi la Polisi kutokana na tabia mbaya. Alifukuzwa baada ya kumshambulia polisi mwenzake na kumkojolea mkojo.

Baada ya kuachishwa kazi ya jeshi akaanzisha chuo chake cha ulengaji shabaha alichokiita Rob Furlong’s Marksmanship Academy huko huko Alberta.