Na Theonestina Kaiza-Boshe

Kwa muda mrefu sasa Tanzania imekuwa ikiimba wimbo kuwa ‘kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa’. 

Na kwa nyakati mbalimbali serikali imetengeneza sera na kaulimbiu mbalimbali kuchochea dhana hiyo ili kuboresha matokeo.

Kuna wakati serikali ikaja na kaulimbiu ya ‘Siasa ni Kilimo’. Ama kwa hakika, juhudi nyingi zimefanywa na serikali katika azima ya kuinua kilimo, sambamba na kuondoa umaskini nchini. 

Bahati mbaya sote tunashuhudia matokeo yasiyorandana na nguvu na kauli zinazoelekezwa kwenye kilimo kwa sera, kaulimbiu na programu maalumu za serikali. 

Kwa ujumla mavuno na kipato kitokanacho na kilimo mashambani na vijijini hayaendani kabisa na juhudi za serikali katika kuhimiza kilimo. 

Kwa mujibu wa Hotuba ya Bajeti ya 2020/2021, kilimo kimeendelea kutoa ajira kwa asilimia 58 ya Watanzania na kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa. 

Hotuba hiyo iliainisha ukuaji wa kilimo kati ya mwaka 2015 na 2019 kuwa wastani wa asilimia 5.2. 

Inaelekea ukuaji huu unatokana zaidi na kilimo cha maua, matunda na mboga, ambayo miaka ya nyuma hayakuwa ya biashara.

Hivyo mchango wa kilimo sasa unatokana zaidi na ongezeko la wakulima na mazao mapya mchanganyiko, na si kutokana na ongezeko la tija kwa mazao makuu yanayolimwa na wakulima walio wengi. 

Mambo yanayosababisha hali hiyo yamejadiliwa mara nyingi, na serikali imefanya juhudi za hapa na pale kukabiliana na hali hiyo.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, si lengo la makala hii kuzungumzia sababu hizo, ila ninaomba hata hivyo utambue kuwa nimekuwa nikiizungumzia Serikali Kuu bila kutaja Serikali za Mitaa/Vijiji kunakofanyika shughuli za kilimo.  

Hii ni kwa sababu juhudi nyingi za kuinua kilimo zinaonekana kufanywa na Serikali Kuu na uhusika na ushiriki wa Serikali za Mitaa ukiwa hauendani na kinachosemwa na kufanywa na Serikali Kuu. 

Isitoshe, uhusika wa Serikali za Mitaa haulingani na wajibu na matarajio kwa mujibu wa mfumo wa tawala za serikali na sheria. 

Hili ni tatizo kubwa linalohitaji mkakati na juhudi mahususi na za dhati, kama kweli tunataka kuinua kilimo. Hata hivyo, hili si somo la makala hii.

Makala hii inajikita zaidi kwenye fursa mpya za kimataifa zinazoweza kumuinua mkulima hata katika msimu mmoja tu na taifa likanufaika kiuchumi. 

Fursa hizi ni masoko ya nje ya nchi yaliyotangazwa na vyombo vya habari kuwa nchi husika zimeingia mikataba ya maelewano na serikali. 

Taarifa zinasema nchi hizo zinahitaji kiasi kikubwa cha mahindi ya njano, ufuta na muhogo kiasi kwamba, kwa kuanzia, Tanzania haiwezi kukidhi mahitaji ya masoko kwa mazao hayo.

Kiwango kinachohitajika, Serikali ikitimiza wajibu wake barabara, zao moja au mawili, yanaweza kuinua maisha ya wakulima wengi na kuongeza Pato la Taifa kwa kiwango kikubwa sana.

Lakini kwa kile kilichoonekana AGOA ya Marekani na mkataba wa serikali ya China kuhusu muhogo mwaka juzi, wakulima wa kawaida wanaweza wasiambulie chochote, wala hata habari wasiipate.

Mheshimiwa, nikiangalia, kwa mfano, mkataba wa mwaka juzi baina ya serikali na China kwenye muhogo, ninaona kuna kizungumkuti wizarani kwako kinachohitaji kutanzuliwa, kama serikali yetu hakika inataka kumuinua mkulima na kukuza Pato la Taifa kutokana na fursa kubwa za masoko ya mazao ya kilimo nje ya nchi.

Kilichowasibu wakulima wa muhogo baada ya kujua kulikuwa na soko kubwa China na kuhimizwa kulima kwa wingi, ninasema, kifupi, ni kizungumkuti. Mimi mwenyewe ni mwathirika na ninawajua wenzangu walioathiriwa na kizungumkuti hicho.

Baada ya msimu kuanza, na tukiwa na taarifa za mkataba huo wa soko la muhogo mbichi China, tulianza kutafuta taarifa wizarani tukitaka kujua utaratibu. 

Japo tulipata mawasiliano na mratibu wizarani, hakukupatikana taarifa zilizohitajika, na taarifa nyingine zilizotolewa zilikuwa za kukatisha tamaa. 

Kwa mfano, niliwahi kupata maelekezo ya kumtafuta mnunuzi wa muhogo Kiwangwa, Bagamoyo, Mtanzania aliyekuwa akinunua muhogo mbichi kwa kupelekewa kiwandani kwake kwa bei ya Sh 100 kwa kilo!

Cha ajabu, Wizara haikutoa taarifa za wapi waliko hao Wachina waliokuwa wananunua muhogo! 

Katika kutafuta taarifa huku na kule, wakati mmoja nilipata taarifa kuwa wapo Wachina Mtaa wa Zanaki na Bibi Titi Mohamed wananunua makopa safi ya muhogo kwa Sh 300 kwa kilo! 

Huko nako ilitakiwa mkulima/muuzaji awapelekee muhogo kwa gharama zake; tena kwanza awapelekee sampuli, wakiupenda ndipo awapelekee wa kuwauzia. 

Kingine cha kushangaza, ni kushauriwa kusindika muhogo na kujaribu soko la Burundi!  Hapo ndipo nilianza kuona kwamba kuna kizungumkuti. Kwa maana wakati huo huo kuna matukio matatu yaliyotuchanganya.

Tukio la kwanza ni la taarifa za Wachina tulioambiwa wapo Dar es Salaam, halafu baadaye kuambiwa wamekwenda Tanga bila taarifa za mahali walikokuwa wanapatikana au namna ya kuwasiliana nao.  

La pili ni kuona kwenye vyombo vya habari Wachina fulani wakitoa mashine za kuchakata muhogo kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Tanga.

Tukio la tatu ni wakati tukizidi kuwa na maswali kuhusu mradi huo wa muhogo na wanunuzi wa China, gazeti moja likachapisha taarifa ya mfanyabiashara mashuhuri nchini kupeleka shehena kubwa ya muhogo China.

Wakati hayo yote yanaendelea, muhogo shambani ulishakomaa na kupitiliza. Walioweza waliamua kuchakata muhogo uliokuwa bado unawezekana kusindika unga na kutafuta soko la ndani; kazi iliyokuwa ngumu kwa vile soko linatakiwa kutafutwa kabla hata ya kulima. 

Matokeo yake mihogo mingi iliharibikia mashambani na kukatisha tamaa wakulima.

Ombi langu, Mheshimiwa Waziri, ukiwa mpya katika wizara hiyo muhimu kwa ustawi wa wananchi na uchumi wa taifa, una fursa ya kutanzua kizungumkuti kuhusu mikataba ya kimataifa ya masoko ya mazao kinachoonekana kuwapo wizarani na wadau wengine kama Wizara ya Viwanda na Biashara na kuwawezesha wakulima kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu masoko ya mahindi ya njano, ufuta na muhogo.

Aidha, ichunguzwe na kufahamika kwa nini wakulima nchini hawajanufaika na AGOA, kwa lengo la kurekebisha mambo yaliyosababisha hali hiyo kwa muda wa zaidi ya miaka 20. 

[email protected]

By Jamhuri