Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wagombea udiwani 127 kutoka vyama 18 vya siasa wanatarajiwa kupigiwa Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 20 Machi, 2024.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele jijini Dar es Salaam wakati akitoa risala ya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara.

Jaji Mwambegele amesema kati ya wagombea hao 127 wagombea wanaume ni 89 na wanawake ni 38 na kuongeza kuwa wapiga kura 128,157 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki katika uchaguzi huo mdogo na jumla ya vituo 373 vya kupigia kura vitatumika.

“Tume inatoa pongezi kwa wadau wote wakiwemo wapiga kura na wananchi katika kata (22) zenye uchaguzi kwa utulivu waliouonesha wakati wote wa kipindi cha kampeni,” amesema Jaji Mwambegele.

Jaji Mwambegele wasimamizi wa uchaguzi katika kata husika wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi.

“Mawakala wanawajibika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao na katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu za uchaguzi na Maelekezo ya Tume.”, amefafanua Jaji Mwambegele.

Aliwataka wapiga kura katika uchaguzi huu mdogo, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura hapo kesho, ili kuwachagua viongozi wanaowataka huku akivikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wengine wa Uchaguzi kujiepusha na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

“Mafanikio ya uchaguzi huu yatatokana na kuwepo kwa hali ya utulivu na amani katika maeneo yote yenye uchaguzi. Hivyo, Tume inatarajia kuona hali ya amani na utulivu iliyopo sasa inaendelea kuwepo hadi shughuli za uchaguzi zitakapokamilika.”, aliongeza Jaji Mwambegele.

Alivikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala, wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi mdogo wa Udiwani katika kata 22, zinahitimishwa rasmi leo tarehe 19 Machi, 2024, hivyo vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao hawatakiwi kufanya kampeni za aina yeyote zaidi ya saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni ya leo.

Ametaja mambo mengine ambayo hayaruhusiwi kufanyika baada ya saa 12:00 na siku ya uchaguzi kuwa ni pamoja na kutumia alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi na kwamba upigaji kura katika maeneo yote ya uchaguzi, utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Alikumbusha kuwa vituo vya Kupigia Kura vitafunguliwa saa moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni. Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi kamili jioni (10:00) na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura na mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni.

“Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kata husika na wana kadi zao za mpiga kura. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala kama vile, Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili mradi majina yaliyopo katika vitambulisho hivyo, yawe sawa na yaliyokuwepo katika kadi ya mpiga kura.”, amefafanua Jaji Mwambegele na kuongeza kuwa:

“Mpiga Kura aliyepoteza kadi yake au kadi yake kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala, iwapo tu; atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo katika orodha ya wapiga kura katika kituo anachokwenda kupiga kura. Aidha, majina yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yawe yanafanana na yale yaliyopo katika kitambulisho mbadala.”

Jaji Mwambegele alieleza kuwa kutakuwa na majalada ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye uoni hafifu na wenye ulemavu wa kuona ili yawasaidie kupiga kura bila usaidizi na kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona na ambao hawawezi kutumia majalada hayo, wataruhusiwa kwenda vituoni na watu ambao wanawaamini na ambao watawachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.

Kuhusu kipaumbele kwa wapiga kura, Jaji Mwambegele alisema katika vituo vya kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaofika na watoto wao vituoni.

Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa maelekezo yaliyomo kwenye Maadili ya Uchaguzi ya Mwaka 2020, wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu baada ya kupiga kura. Hivyo, Tume inawashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.

Kata zinazofanya uchaguzi ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Mshikamano (Halmashauri ya Manispaa ya Musoma), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga), Fukayosi (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).

Kata nyingine ni Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu), Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).”