Ni mwitikio wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu juu ya uongezaji thamani madini

Eneo la Mgodi wa Buzwagi unaofungwa sasa kujengwa zaidi ya viwanda 100

Buzwagi kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za migodini kwa nchi Afrika Mashariki na Afrika ya Kati

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutekeleza kwa dhati Sera ya uongezaji thamani ya Madini ndani ya nchi kwa kutengeneza Bidhaa zitokanazo na Madini ghafi kwa kutenga eneo maalumu la ukanda wa kiuchumi (Buzwagi Special Economic Zone) katika eneo la ekari 1333 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini na uzalishaji wa bidhaa za migodini ambapo awali palikuwa pakifanyika shughuli za uchimbaji madini kupitia Kampuni ya Madini ya Barrick.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde amezungumza hayo jana tarehe 18 Machi, 2024 mkoani Shinyanga Wilaya ya Kahama wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo cha ‘Barick – Buzwagi Academy’ ambacho kitakwenda kutoa mafunzo mbalimbali katika kuongeza uelewa na maarifa katika masuala muhimu ya kwenye Sekta ya Madini.

“Moja kati ya maelekezo ya Mhe. Rais ni kuhakikisha Madini yetu yanaongezewa Thamani Nchini na kuongeza fursa za ajira kwa watanzania,kuongeza ujuzi kwa nguvu kazi na kuchochea upatikanaji wa mapato ya nchi,na hapa Buzwagi ndio panakwenda kuleta mabadiliko makubwa,” amesema Mavunde.

Mwitikio wa ujenzi wa viwanda katika eneo hili umekuwa mkubwa na husasan katika viwanda vya kungeza thamani madini na uzalishaji wa bidhaa za migodini ambazo awali nyingi zilikuwa zinanunuliwa nje ya nchi na sasa kupitia viwanda hivi zitapatikana hapa nchini.

Viwanda vitakavyokuwepo kwa awamu ya kwanza ni Kiwanda cha usafishaji na uongezaji madini thamani(Multi Metals Facility) ambacho kipo chini ya Kampuni ya Tembo Nickel, Steel Balls Manufacture – Oriental Grinding Media ( China), Mine Conveyors Belts – East Africa Conveyers Services, Solar Farms – Voltalia Ltd and SSI Energy Underground Wiremesh – Wireforce South Africa na Portable Water Plant chini ya Kampuni ya City Engineering.

Awali, Mkuu wa Wilaya wa Kahama **Mhe.Mboni Mhita ** aliipongeza na kuishurkuru Kampuni ya Barick kwa uwekezaji wa kipekee katika eneo la Kahama pamoja na ushirikiano mzuri baina ya Serikali na Kampuni ya Barick na kusema kwamba hatua hizi za makusudi zitasaidia kuchochea uchumi wa wilaya ya Kahama ambao baada ya mgodi wa Buzwagi kufungwa ulidorora.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Barick Dkt. Mark Bristow alieleza kuwa Kampuni yao inaunga mkono juhudi za Serikali Juu ya uongezaji thamani madini na ushiriki wa wazawa kwa kuwekeza kwenye elimu ya Vijana kama vile kituo cha mafunzo kwa wadau wa madini cha ‘Barick Academy’ ambacho kinatarajiwa kutoa mafunzo kwa watu 1024 kwa mwaka 2024, akaongeza pia wapo mbioni kuwapa nafasi za juu za uendeshaji migodi hapa nchini hiyo kwa watanzania.

Naye, Mbunge wa Kahama Mjini Mhe. Jumanne Kishimba aliiomna Kampuni ya Barrick kuandaa mafunzo mafupi kwa wachimbaji wadogo kuwafundisha usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini na hasa dhahabu kwa kuwa wananchi wengi ambao ni wachimbaji hawana uelewa mkubwa wa biashara ya madini.

By Jamhuri