Waumini wa Kiislamu katika Kijiji cha Butiama na uongozi wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mara wamo kwenye mgogoro kuhusu umiliki na uendeshaji wa msikiti uliojengwa kwa msaada wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kijijini hapo.

Msikiti huo ulianza kujengwa wakati Mwalimu akingali hai, na ulifunguliwa rasmi na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma, Oktoba, 2000.

Wiki iliyopita viongozi watatu wa msikiti huo – Imam Athuman Muhaya, Aboubakar Nyambareka na Katibu Azizi Magambo – waliwekwa rumande wakituhumiwa kupinga uamuzi wa BAKWATA, jambo ambalo limeibua simanzi miongoni mwa Waislamu wa Butiama wanaoamini kuwa wanaonewa.

“Wako rumande [walidhaminiwa] hakuna hati yoyote ya mashtaka, na taarifa tulizonazo ni kuwa wanaandaliwa mashtaka ya ugaidi. Wanajua wakiwabambikia mashtaka ya ugaidi hawawezi kupewa dhamana – wataozea rumande. Ugaidi Butiama utoke wapi?” amehoji mmoja wa waumini.

Mgogoro huo umemuumiza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Butiama, Yohana Mirumbe, ambaye ameliambia gazeti hili kuwa anafanya kila awezalo akutane na pande zinazogombana katika msikiti huo ili kulinda heshima ya Butima na ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Anasema: “Nimepanga nakutana nao wiki hii, hatuwezi kukubali mgogoro huu mdogo uendelee kuharibu taswira na heshima ya Butiama, ni aibu. Heshima ya Butiama ni kubwa sana, ni aibu kutajwa kwenye migogoro ya aina hii. Ni aibu. Hatutaki masuala ya dini yapelekwe mahakamani, tunataka yamalizwe huku huku kwa njia za mazungumzo. Atakayekaidi tutajua huyo ndiye hatutakii mema. Tunataka Butiama iwe ya amani ili kulinda heshima ya Baba wa Taifa,” amesema Mirumbe.

Wazo la ujenzi wa msikiti huo lilitolewa na Mwalimu Nyerere wakati ambao waumini wa Kanisa Katoliki kijijini hapo wakiwa wamejengewa kanisa zuri, hivyo kuwaondolea adha ya sehemu ya kuabudia.

Mmoja wa Waislamu waliozungumza na JAMHURI amesema: “Waislamu walikuwa wanaswalia kwenye kibanda kichakavu pale stendi – jambo lile lilimuuma Mwalimu Nyerere, na siku moja akasema: “Hawa Waswahili wangu wanastahili wapate msikiti, sasa nitafanyaje, lakini ngoja niwatafute marafiki zangu wanisaidie.”

Inaelezwa kuwa mapema mwaka 1999, Mwalimu alikwenda nchini Libya kwa kiongozi wa taifa hilo, Kanali Muammar Gaddafi, na kumwomba msaada wa kujengewa msitiki kijijini Butiama.

Gaddafi alikubali na kumpa Mwalimu fedha za kutosha ujenzi huo. Mwalimu aliporejea alikabidhi fedha hizo kwa kamati iliyoundwa kusimamia ujenzi. Kamati hiyo iliongozwa na msaidizi wake, Raphael Mkanzabi.

Mwalimu aliuomba uongozi wa kijiji kutenga kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa msikiti, makazi ya sheikh, hosteli na kadhalika. Kwa sasa hosteli hizo ni kitega uchumi na zinatajwa kuwa miongoni mwa cheche za mgogoro unaoendelea kutokana na mapato.

Taarifa ya uongozi wa msikiti huo inamtaja Nathani Alute kuwa ndiye aliyesanifu ujenzi huo. Mkandarasi alikuwa ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Taarifa inasema: “Mwalimu aliteua watu watatu kusimamia ujenzi wa msikiti – msimamizi mkuu alikuwa Mkanzabi, Mbaraka Rusheke na Chifu Japhet Wazangi. Pamoja na jengo la msikiti, kulijengwa ofisi nne, madarasa mawili, sehemu ya kushikia udhu zenye vyoo kwa pande zote mbili, nyumba ya makazi ya sheikh wa msikiti pamoja na hosteli kwa wageni mbalimbali. Kwenye ujenzi sisi Waislamu tuliwakilishwa na Kamati ya Mipango na Fedha iliyoundwa na Mwalimu mwenyewe. Waislamu tulishiriki ujenzi kama sharti tulilopewa na Mwalimu, maana aliamini kwa kufanya hivyo Waislamu wangeona msikiti huo ni mali yao.

“Tulifanya hivyo na tukachangia tripu 78 za mawe na tripu 120 za mchanga. Kazi hii ilifanywa na Waislamu wa Butiama, sasa hao [mkoa] wanaodai kuwa msikiti huu ni mali yao waeleze wamechangia nini? Hatukuona ushiriki wowote wa mkoa kwenye ujenzi huu, kwa hiyo wanaotaka kutunyang’anya wajue wanatuonea.”

Wanasema kulikuwa na sehemu kuu mbili kwenye ujenzi wa msikiti huo. Sehemu ya kwanza ni kamati iliyoundwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe ambayo iliitwa Kamati ya Mipango na Fedha ikiwa na wajumbe watatu.

“Kazi ya kamati hiyo ilikuwa kudhibiti matumizi ya fedha na kuratibu mipango yote ihusuyo ujenzi. Wao ndio waliokuwa watia saini kwenye akaunti iliyokuwa na fedha zote za ujenzi, na wao ndio waliokuwa wasimamizi wakuu wa shughuli nzima ya ujenzi.

“Sehemu ya pili ilikuwa kamati iliyoundwa na uongozi wa msikiti ambayo iliitwa Kamati ya Ujenzi. Dhima yake ilikuwa kuratibu shughuli zote za kila siku za ujenzi kupitia na kuidhinisha mahitaji ya mjenzi na kumwombea kwa Kamati ya Fedha na Mipango malipo ambayo yalifanyika moja kwa moja kutoka Kamati ya Fedha.

“Jukumu jingine lilikuwa kuhamasisha Waislamu washiriki ujenzi pale mchango au nguvu zao zinapohitajika. Wajenzi walikuwa askari wa JKT walioombwa na Mwalimu – na walifanya kazi bila malipo. Askari hao waliongezewa nguvu na mafundi raia ambao walilipwa kutoka kwenye fungu la ujenzi.

“Msanifu wa majengo hatukujua walikubaliana nini na Mwalimu, na baada ya Mwalimu kufariki dunia kuna gharama alilipwa msanifu huyo,” inasema taarifa ya waumini wa Butiama.

Ujenzi ulianza mwaka 1999 wakati Mwalimu akiwa bado hai, lakini jiwe la msingi liliwekwa Machi, 2000. Ulizinduliwa na Dk. Omar mwaka 2000 mwishoni kwa mwaliko unaodaiwa kuandaliwa na uongozi wa msikiti huo.

“Siku ya ufunguzi walialikwa viongozi wa madhehebu mbalimbali, ukakabidhiwa kwa uongozi wa wakati huo uliokuwa chini ya Aziz na Rusheke. Kwenye hotuba yake, Makamu wa Rais alitamka wazi kuwa msikiti huu ni mali ya Waislamu wa Butiama na serikali itajitahidi kukamilisha ahadi za Mwalimu kwa Waislamu pamoja na kumsomesha sheikh. Haya yote yalitekelezwa Dk. Omar akiwa bado hai,” wanasema Waislamu hao.

Taarifa kutoka Butiama zinasema tangu mwaka 2000 hadi mgogoro ulipoanza, msikiti huo umekuwa ukiendeshwa na kamati zinazochaguliwa na Waislamu wenyewe wa Butiama.

“Uchaguzi unafanyika na mabadiliko mbalimbali yamekuwa yakifanyika kadiri inavyotakikana. Pamoja na changamoto mbalimbali, hali ya amani ya msikiti imekuwa shwari kabisa. Migogoro midogo midogo imekuwa ikimalizwa na Waislamu wenyewe na mara chache sana imehusisha dola.

“Kwa pamoja waumini wa msikiti huu ambao ndio wamiliki wameamua kuwa msikiti huu uwe kumbukumbu ya kazi za Mwalimu na ikiwezekana uwekwe chini ya mamlaka zinazoangalia, zinazoenzi na kutunza kazi za mikono ya Mwalimu.

“Tunashauri utengenezewe utaratibu kwa msaada wa serikali ambao utauweka kuwa huru, yaani usiwe chini ya taasisi yoyote ili malengo ya Mwalimu yafikiwe, hasa kwa walengwa wakuu ambao ni Waislamu wa Butiama na wageni wanaofika hapa,” inasema taarifa ya waumini hao.

 

Mwanzo wa mgogoro

Mgogoro wa umiliki wa msikiti huo ulianza Mei, 2012 baada ya barua ya BAKWATA Mkoa wa Mara ya Juni 23, mwaka huo iliyopelekwa Butiama ikieleza kuwa msikiti huo umepandishwa hadhi na kuwa Msikiti wa Wilaya ya Butiama.

Mei 5, 2012 timu ya uongozi wa BAKWATA Mkoa wa Mara ilifika Butiama wakiwa na uongozi wa wilaya na kudai ukabidhiwe hati ya umiliki wa msikiti huo; jambo ambalo lilipingwa na waumini.

Julai mosi, 2012, Katibu wa Kamati Tendaji ya Msikiti wa Butiama, Magambo alimwandikia barua Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Mara, akipinga uamuzi wa Baraza hilo wa kuupandisha hadhi msikiti huo – kitendo anachosema kililenga kuwapoka haki zote za umiliki.

Magambo anasema kwenye barua hiyo: “Utakumbuka kuwa kikao [Mei 26, 2012] yapo maazimio mahususi yaliyofikiwa mbele ya viongozi wa serikali ambayo kwa makusudi umeendelea kuyakiuka, hivyo kuleta uvunjifu wa amani msikitini na Butiama kwa jumla.

“Baadhi ya maazimio hayo ni BAKWATA mkoa wana wajibu wa kutambua uongozi uliopo madarakani katika msikiti wa Butiama kwani umechaguliwa kihalali na waumini na si haki kupora madaraka ya uongozi kiholela bila kufuata taratibu.

“Kwamba BAKWATA Mkoa watambue kuwa wamiliki wa msikiti wa Butiama ni waumini wa Kiislamu wa Butiama, kwani wao ndio waliojenga msikiti huo si BAKWATA na ndio waliokabidhiwa msikiti huu Oktoba 13, 2000 baada ya kufunguliwa rasmi na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma.

“Kama BAKWATA Mkoa wa Mara  wana nia ya kupata msikiti wa Wilaya ya Butiama wanaweza; mosi, kuomba kiwanja ili wajenge msikiti eneo lolote wapendalo ndani ya wilaya; pili, kupandisha hadhi msikiti wowote ulio ndani ya Wilaya ya Butiama ili uwe msikiti wa wilaya.”

Anaendelea kushauri kuwa kama BAKWATA Mkoa wa Mara wanataka kupandishwa hadhi kwa msikiti wowote wanaotaka, wafanye hivyo baada ya kuketi pamoja na uongozi na waumini.

“Kitendo cha BAKWATA Mkoa kutamka kuwa msikiti wa Butiama umepewa hadhi ya kuwa msikiti wa wilaya bila kwanza kuwasiliana na viongozi na waumini wa msikiti huu ambao ndio wajenzi na wamiliki ni kitendo cha dharau na kinacholenga kuleta mvurugano na uvunjifu wa amani msikitini.

“Kitendo cha BAKWATA Mkoa kukiuka maazimio yaliyofikiwa mbele ya viongozi wa serikali wakiwamo wa vyombo vya ulinzi na usalama Mei 26, 2012 kuhusu namna bora ya kupata msikiti wa wilaya ni dharau ya hali ya juu kwa uongozi wa serikali,” anasema Magambo.

Waumini wa Butiama wanasema viongozi wa BAKWATA wameshindwa kuwathibitishia kikao halali kilichoufanya msikiti wa Butiama kuwa msikiti wa wilaya.

“Kwa kuwa viongozi wa Baraza walikiri na kuomba radhi kwa viongozi/waumini wa msikiti wa Butiama mbele ya viongozi wa serikali na kuwa utaratibu wa uteuzi wa msikiti kuwa wa wilaya haukufuata taratibu na kanuni za Kiislamu, hivyo wakaahidi kurejea mchakato wa uteuzi na kuridhiwa na viongozi na waumini wa msikiti; kwa msingi huo, sisi waumini wa msikiti wa Butiama kwa kauli moja tunapinga msikiti wetu kuwa msikiti wa wilaya. Badala yake tunashauri BAKWATA Mkoa wa Mara wapeleke maombi yao katika misikiti mingine au waombe kiwanja ili sote tushirikiane kujenga msikiti wa wilaya.

Hali bado tete

JAMHURI limebaini kuwa licha ya msimamo huo wa waumini na viongozi wa msikiti wa Butiama, mgogoro umeendelea kufukuta, huku baadhi ya viongozi ‘wavamizi’ wakidaiwa kuwajeruhi wenzao waliowakuta katika msikiti huo.

Mapema mwaka jana, mtu anayejimbulisha kuwa ni Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Butiama, Mohamed Nyonga, alituhumiwa kumpiga na kumjeruhi ndani ya msikiti, Imam Magambo; hali iliyomfanya imam huyo afungue kesi mjini Musoma.

Nyonga yuko rumande kwa amri ya mahakama baada ya kile kinachodaiwa kuwa ni kukaidi mwito wa kufika mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

Wakati shambulizi hilo likitokea, Nyonga alikuwa amempangisha kwenye hosteli, Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Butiama, na kukawapo mvutano wa malipo ambapo uongozi wa msikiti ulitaka ulipwe lakini uongozi wa BAKWATA wilaya na mkoa ukawa unataka ndio upokee malipo hayo.

 

Viongozi wazungumza

Kiongozi wa BAKWATA Mkoa wa Mara, Sheikh Msabaha Kassim, amezungumza na JAMHURI na kusema BAKWATA mkoani humo ndio wamiliki halali wa msikiti huo; tofauti kabisa na madai yanayotolewa na baadhi ya waumini na viongozi wa msikiti huo kijijini Butiama.

Anasema uongozi kwenye msikiti huo ulifanywa mwaka 2013, lakini mara zote kumekuwapo kikundi kisichokubaliana na mabadiliko hayo.

Ameulizwa mchango wa BAKWATA kwenye uejenzi wa msikiti huo, amejibu: “Mchango upi, sisi tunajua msikiti huo ni mali ya BAKWATA, Mwalimu alitoa fedha ukajengwa, sasa sijui unauliza umiliki upi.”

Ameulizwa pia kama wanazo hati zozote za umiliki wa eneo na majengo ya msikiti huo. “Msikiti tulikabidhiwa kwa maneno, hakuna hati. Hata hao wanaodai kuwa ni wao hawana hati. Nadhani hati wanazo walioujenga. Hao wanaodai kuwa ni wao wanahaha kutafuta hati, hawana pia,” amesema.

Sheikh Kassim anasema kundi la waumini na viongozi hao limekuwa likitaka msikiti huo uwe wa Wazanaki tu; jambo ambalo anasema halikubaliki. Kwa upande wao, viongozi wa msikiti huo wamesema kauli hiyo ya Sheikh Kassim ni ya kutunga na inataka kuhalalisha nia ovu ya kuwapoka msikiti kwa sababu anajua ubaguzi wa aina yoyote ni jambo lisilokubalika nchini.

“Wanatunga maneno mengi, ugaidi ni jambo zito sana. Hivi kweli Butiama, Butiama watoto waliozaliwa hapa wawe magaidi kwa sababu tu wanadai haki yao? Tunajua tunaandamwa na polisi na vyombo vya usalama kwa sababu mmoja wa kiongozi hapa ana udugu na sheikh aliyefunguliwa kesi. Wanasikika wakisema lazima Wazanaki wakomeshwe maana wanajifanya wajuaji. Msimamo wetu ni kuwa msikiti huu tumejengewa kihalali na Baba wa Taifa,” anasema mmoja wa viongozi wa msikiti huo.

Kwa upande wake, Mkanzabi, ambaye ndiye kiongozi na msimamizi mkuu wa ujenzi wa msikiti huo ameliambia JAMHURI: “Niliusimamia ujenzi wa msikiti huo, nalielewa vizuri suala hili lakini sipendi kulizungumza hapa [kwenye vyombo vya habari].

“Kwa kuwa bado nipo, nawashauri kama wanahitaji maelezo yangu, iwe kwenye vikao vya hapo au kwingine, waniite tu- nipo tayari kwenda kuwaeleza ninayoyajua.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, ambaye alikuwa mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Mwalimu Nyerere, amezungumzia mgogoro huo na kusema hauna sababu ya kuwapo.
“Ule msikiti kila mtu anajua Mwalimu aliujenga kwa ajili ya upendo wake kwa Waislamu – hasa wakati ule ambao kulikuwa na kanisa, lakini hakuna msikiti. Sasa kusikia kuna vijana wanakamatwa eti washtakiwe kwa sababu wanaitwa magaidi ni jambo la kusitikisha. Watuite sisi wazee tunaolijua suala hilo vizuri. Muhimu ni kuhakikisha kuwa jina na heshima ya Mwalimu haivurugwi na vurugu za aina yoyote,” amesema Butiku.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Butiama, John Lwamlema, ameulizwa kuhusu kukamatwa kwa viongozi hao wa msikiti, lakini amekataa kuzungumza kwa maelezo kwamba yeye si msemaji wa Jeshi la Polisi. Ameshauri aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara. Juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Please follow and like us:
Pin Share