Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

WAKULIMA wanaozalisha mazao ya viungo kwa mfumo wa kilimo hai katika vijiji vya Kizerui na Antakae wilayani Muheza mkoani Tanga wameiomba Serikali kutengezeza sheria za kusimamia mazao hayo ili kuweza kuyalinda na kuyaongezea thamani.


Ombi hilo wamelitoa wakati wakizungumza na waandishi wa habari, wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), ambao walitembelea vijiji hivyo kati ya 20 vinavyozunguka Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani, iliyopo chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kizerui ambaye pia ni mkulima wa mazao ya viuongo amesema pamoja na uhakika wa soko la mazao hayo bado kuna changamoto ya kisheria, hivyo anaiomba Serikali kuangalia namna ya kuitatua.

“Tunawashukuru wadau wote wakiwemo USAID Tuhifadhi Maliasili ambao wameliwezesha Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na GFP Organic kutupatia elimu ya namna ya kulima kilimo hai na kututafutia masoko ya karafuu, iliki, pilipili manga na mdalasini, ila tunaomba kuwepo sheria ya mazao hayo, hasa yanayozalishwa kwa njia ya kilimo hai, kwani sheria ya sasa ni ngumu sana kufanikiwa,” amesema.

Kusaga amesema wakulima wa mazao ya viungo katika Ukanda wa Hifadhi ya Amani wameamua kujikita katika kilimo hai, ili kuhakikisha kilimo hicho kinakuwa endelevu kupitia mifumo ya kisheria.

Amesema mazao ambayo yamezalishwa kwa mfumo wa kilimo hai yana soko la uhakika, hivyo iwapo sheria itawalinda siku chache zijazo wataweza kunufaika na kilimo hicho na kuondokana na umaskini.
Pamoja na kuiomba Serikali kutunga sheria ya kutambua mazao hayo, pia ameziomba kampuni mbalimbali kujitokeza kununua mazao ya viungo, ili kuleta ushindani wa bei katika soko.

Kwa upande wake Francis Kusaga amesema kilimo cha mazao ya viungo kimeanza kumpatia faida, ila anaamini sheria rafiki ndizo zitaweza kumkomboa moja kwa moja na kumpa nguvu ya kuendeleza kilimo hicho.

“Mimi ni kijana wa miaka 20 nalima karafuu, iliki, pilipili manga na mdalasini kusema kwenye mazao haya yana faida, sitarajii kuondoka kijijini kwenda mjini, lakini naungana na wenzangu kuiomba serikali kuangali upande wa sheria, ili ziweze kutulinda,” amesema.

Naye Bertha Maguluko mkulima kutoka kijiji cha Ntakae amesema mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umekuwa chachu kwao, kwani wameweza kupata elimu, ikiwemo kujua thamani ya mazao ya viungo, ikiwemo kupanda kwa kufuata utaratibu hivyo kuweza kuvuna kwa wingi.

Maguluko amesema kutokana na kasi ya wananchi kujiunga na kilimo cha mazao ya viungo kwa njia ya kilimo hai ni vema eneo hilo likatungiwa sheria yake, hali ambayo itadhibiti watu wanachakachua.

“Mimi naomba masoko ya uhakika ndani na nje nchi, ila muhimu zaidi ni uwepo wa sheria ya kutulinda sisi wakulima wa mazao ya viungo yanayozalishwa kwa njia ya kilimo hai, ili soko letu lisianguke,” amesema.

Mdoe Kijazi amesema miradi hiyo imezingatia usawa wa kijinsia hasa kwenye kilimo, hivyo ili iweze kuwa endelevu ni lazima kuwepo sheria nzuri zitakazowalinda wakulima na kutunza mazingira.

Wenyeviti wa vijiji hivyo, Andrea Kingazi na Hamza Magembe wamesema sheria nzuri zitaweza kupaisha soko la mazao ya viungo huku wakiweka bayana kuwa mafanikio yameanza kupatikana.

Meneja Mwendeshaji wa Kampuni ya GFP Organic, Magreth Lutege amesema wao kama wanunuzi, wanaungana na wakulima kuhusu uwepo wa sheria ya kusimamia na kulinda mazao hayo ambayo yana soko kubwa duniani.

Lutege amesema mazao ya viungo yana soko kubwa duniani, akitolea mfano karafuu kwa mwaka zaidi ya tani 80,000 zinahitajika, hivyo ili kuhakikisha uzalishaji unakuwa endelevu lazima kuwepo sheria ambazo zitayalinda.

“Kwenye soko la dunia mazao ya viungo yanalipwa kwa njia ya kilimo hai yanahitajika, hivyo naomba Serikali iangalie namna ya kutengeneza sheria ambayo ni rafiki kwa mkulima na munuaji,” amesema.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Muheza, Hoyange Mbwambo, amesema mazao ya viungo wilayaji humo yamechangia zaidi ya shilingi milioni 200 katika mapato ya mwaka 2023/2024 na kwamba hawatamvumilia mkulima au mfanyabiashara anayechafua taswira ya mazao hayo katika soko la dunia.

Mbwambo amesema ujio wa miradi mbalimbali ukiwemo USAID Tuhifadhi Maliasili na wanunuzi kama GFP umekuwa na manufaa zaidi hasa katika eneo la matumizi bora ya ardhi na kuongeza ulizalishaji.