Wakunga, Wauguzi waliotahiniwa watakiwa kuripoti kwenye vituo vya mitihani

Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

BARAZA la Uuguzi na Ukunga Tanzania limewataka watahiniwa wa mtihani wa usajili na leseni kwa wakunga na wauguzi waliosajiliwa kuhakikisha wanafika kwenye vituo walivyoomba kufanyia mtihani kesho Desemba 28 mwaka huu kuanzia saa mbili asuhuhi bila kukosa kwa ajili ya kupata maelekezo na namba za mtihani.

Hayo yameelezwa leo Desemba 27,2023 jijini hapa na Kaimu Msajili wa Baraza hilo Happy Masenga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kufanyika kwa mtihani huo huku akiwataka kufika na mahitaji yaliyo orodheshwa katika tangazo ikiwemo kitambulisho, kadi ya usajili na kalamu nyeusi.

Aidha amefafanua kuwa mtihani unatarajiwa kufanyika mapema siku ya ijumaa Desemba 29,2023 kuanzia saa tatu asubuhi huku jumla ya watahiniwa 4165 wakiwa wanekidhi sifa za kufanya mtihani huo wakiwemo waombaji 3917 ambao wanafanya mtihani kwa mara ya kwanza na 248 kati Yao wanaorudia wanaume 1648 na wanawake 2518.

Masenga amesema mtihani huo utafanyika katika vituo vilivyotambuliwa na kukubalika na baraza katika mikoa mbalimbali hapa nchini kuwa ni Mwanza kwenye kituo cha Taasisi ya afya na sayansi shirikishi (TANDABUI)ambapo idadi ya watahiniwa watakaofanya mtihani ni 991,Dar Es Salaam-Chuo Kikuyu cha Kampala watahiniwa 972 na Dodoma -Chuo Kikuyu cha St. John’s watahiniwa 450 na Chuo cha elimu ya Biashara (CBE) 350.

Vituo vingine ni Kilimanjaro-Chuo cha Stephan Moshi watahiniwa 477,Mbeya-Chuo cha Afya na Sayansi shirikishi Mbalizi 569,Iringa-Chuo kikuu cha Katoriki Ruaha watahiniwa 191 na Tabora 166.