Mwandishi wetu,JamhuriMedia,Monduli

Wananchi wa Kata ya Selela na Engaruka wilayani Monduli mkoa Arusha,wameomba serikali kuwasaidia kuweka uzio katika vyanzo vya maji vya asili katika maeneo yao ili visiendelee kuharibiwa na wanyamapori.

Afisa Maliasili wa tarafa ya Makuyuni na Manyara Happiness Masaki akizungumzia umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji.

Kata hizo zina vyanzo vya maji vya asili ambazo zimekuwa zikitoa maji kwa mwaka mzima ambayo ndio tegemeo kwa mahitaji ya Maji katika Kata hizo kwa matumizi ya majumbani,kilimo na mifugo

Wakizungumza na waandishi wa habari za mazingira,kupitia mradi wa Utunzwaji Mazingira kwa maarifa asilia unaendeshwa na taasisi ya wanahabari ya MAIPAC na taasisi ya CILAO mradi ,anaofadhiliwa na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa(UNDP) kupitia program ya miradi midogo na kuratibiwa na taasisi ya jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF) walisema kama vyanzo hivi havitakwa uzio vitaharibika.

Wakazi Selala wakielezea vyanzo vya maji wanavyotunza

Halima Mollel amesema wanyamapori hasa Tembo wamekuwa wakivamia vyanzo hivyo na kuleta madhara jambo ambalo linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuwekewa uzio.

“Sisi kama jamii tunavitunza vyanzo hivi kwa maarifa yetu ya asili Sasa tunaomba na serikali kutuunga mkono”amesema.

Awali Afisa Misitu wa tarafa ya Makuyuni na Manyara, Happiness Masaki alisema Wananchi wa Selela na Engaruka wametunza vyanzo ya Maji kwa maarifa ya asili na Sasa wananufaika.

Masaki amesema Kata hizo kwa Sasa Zina maji mwaka mzima licha ya maeneo mengine kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi.

“Sisi kama serikali tunawapongeza Hawa Wananchi kwa kutumza hivi vyanzo kutokana na kujiwekea sheria ndogondogo za kimila ambazo zimekuwa rafiki kwa vyanzo vya maji na Mazingira”amesema.

Katibu wa Kamati ya Mazingira Kata ya Selala,Isack Diagwa amesema Siri ya mafanikio ni kushirikisha jamii katika.utunzwaji vyanzo vya maji.

“Lichaya ya kuwa na sheria za serikali kutunza maji pia tunatumia maarifa ya asili ambapo kila mwananchi anawajibika kutunza vyanzo hivi ikiwepo kutoingiza mifugo kwenye vyanzo,kutokana mti ama kulima”amesema.

Mradi wa uhifadhi Mazingira kwa maarifa asilia unatekelezwa na taasisi ya wanahabari ya Usaidizi wa jamii za Pembezoni (MAIPAC) na shirika la msaada ya kisheria la CILAO na kuratibiwa na jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF).

By Jamhuri