MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Februari 19,2024 inatarajia kuanza kusikiliza kesi ya kujeruhi vibaya na kutoa lugha ya matusi inayomkabili wanandoa Bharat Nathwani (Maarufu ka Chiku wa Songea) (57), na mke wake Sangita Bharat Nathwani (54), ambao wanatuhumiwa kwa mashitaka manne.

Kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aaron Lyamuya, lakini ilishindikana kwa sababu hakimu huyo hakuwepo mahakamani kutokana na majukumu mengine aliyokuwa nayo.

Wakili wa Serikali, Frank Michael alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga wa mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa na pia wanamashahidi wawili na wapo tayari kuendelea.

“Mheshimiwa tunao mashahidi wawili na tupo tayari kuendelea, lakini tulikuwa tunaomba tarehe nyingine ya usikilizwaji kwa sababu hakimu anayesikiliza kesi hii hayupo,” alidai Wakili Michael.

Hakimu Kiswaga aliwaonya mashahidi hao na kuwataka kufika mahakamani hapo Februari 19,2024 kwa ajili ya kutoa ushahidi wao.

” Mashahidi nawaonya kufika tarehe hiyo na huyo shahidi ambae amesema tarehe hiyo hatakuwepo atawasiliana na wakili wa serikali atatoa ushahidi wake kwa njia ya mtandao ‘Video Conference’ kwa sababu vifaa vipo,” alidai

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya India wanaoishi Mrima – Kisutu kwenye jengo la Lohana, Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023.

Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani (Chiku) peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la Mrima-Kisutu, jengo la Lohana ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa mke wa jirani yake kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo ya saruji ambapo alimjeruhi katika macho na sikio na pia kumpiga ngumi katika shingo na kumsababishia maumivu makali.

Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani (Chiku) peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara jirani yake katika mwili wake kwa kumpiga ngumi na mateke.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili mke wake Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi dhidi ya majirani zake kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa ushahidi Februari 19 mwaka huu