Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Wakazi wa kijiji cha Makuka Halmashauri ya Wilaya Iringa mkoani Iringa,wanalazimika kutembea zaidi ya km 12 hadi kijiji cha Izazi kufuata huduma ya maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.

Wameiomba Serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA), kuharakisha ujenzi wa mradi wa maji ili kuwaondolea kero hiyo ambayo imeathiri sana utekelezaji na usimamizi wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake mkazi wa kijiji cha Makuka Rehema Nyambala amesema,tangu uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na sasa Tanzania kijiji hicho hakijawahi kupata maji kutokana na ukosefu wa mvua za uhakika .

Mkazi wa kijiji cha Makuka Rehema Nyambala akiwanywesha maji Punda wake wanaotumika kwa ajili ya kubeba maji kutoka kijiji hicho hadi kijiji cha Izazi umbeli wa km 12

Amesema,wanatumia kati ya masaa 2 hadi 3 kwenda kijiji cha jirani Izazi kuchota maji na wenye uwezo wa kifedha wananunua ndoo moja ya maji ya lita 20 kwa Sh.2,000 na 3,000 hivyo kusababisha maisha yao kuwa magumu.

Aidha amesema,ukame na ukosefu wa vyanzo vya maji vya uhakika umepelekea hata kupoteza mifugo ambayo ndiyo chanzo kikubwa cha uchumi na maisha yao.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Iringa Mhandisi Humphrey Mbuba amesema, wameanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa Mkumbwanyi ambao unakwenda kumaliza tatizo la maji safi na salama kwa wakazi wa kijiji hicho.

Amesema,mradi huo ni utanuzi wa skimu mbili za maji mojawapo ni ya Izazi ambayo inapeleka maji katika kijiji cha Makuka na nyingine inapeleka maji katika kijiji cha Mbweleli na Makatapola ambayo kuna changamoto kubwa ya ukame na wananchi wanalazimika kutumia maji ya visima vya asili ambayo yana chumvi.

Aidha amesema,wakati mwingine wanatumia maji ya mito ambayo wakati wa kiangazi mito hiyo inakauka na njia pekee ni kutembea umbali wa km 12 hadi kijiji cha Izazi kwenda kufuata maji kwa matumizi yao ya kila siku.

Tenki linalojengwa kupitia mradi wa maji kijiji cha Makuka wilaya ya Iringa mkoani Iringa ambalo litakapokamilika litahudumia  takribani wakazi  8,000 wa vijiji vitatu vya kata ya Izazi.

Mbuba amesema, kutokana na hali hiyo,serikali kupitia wizara ya maji imeshatoa zaidi ya Sh.bilioni 1.7 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili katika vijiji vitatu vinavyokadiriwa kuwa na wakazi 8,000.

Ameeleza kuwa,utekelezaji wa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na kwa upande wa skimu ya kijiji cha Makuka umekamilika kwa asilimia 85 ambapo wameruhusu maji kwa ajili ya majaribio Kijiji Cha Makuka wakati wakiendelea kukamilisha ujenzi upande wa skimu ya Izaz ili wananchi waanze kupata huduma ya maji.

Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita,kutoa fedha hizo ambazo zinakwenda kumaliza kabisa tatizo la maji kwa wananchi wa vijiji hivyo na kuwataka wananchi kuhakikisha wanatunza mradi huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu.