Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amewaonya Watumishi wa umma wanaoendekeza Vitendo vya Rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao hususani katika kuwahudumia wananchi.

Onyo hilo amelitoa leo wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa 2022 yaliyoanza leo Desemba 6, jijini Dodoma.

Dkt.Ndumbaro amesema kuwa tayari wameweka mifumo madhubuti ya kuwanasa wote wanaopokea na kutoa rushwa katika kuhudumia wananchi.

Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro,akizungumza na waandishi wa habari wakati  akifungua maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa 2022 yaliyoanza leo Desemba 6,2022 jijini Dodoma.

“Nimeeleza hapo juu kwamba siku ya Maadili na Haki za Binadamu tunayoadhimisha kila mwaka hapa nchini, imetokana na siku mbili tofauti ambazo huaadhimishwa kimataifa ambazo ni siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa pamoja na Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. 

“Rushwa ni tatizo katika nchi nyingi duniani hivyo mwaka 2003, Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilikubaliana kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa kila Desemba 9,kuanzia mwaka 2004 ikiwa ni fursa mojawapo kwa kila nchi kutathmini juhudi zake za kudhibiti vitendo vya rushwa”amesema Dkt.Ndumbaro.

Amesema kuwa vita ya rushwa bado ni kubwa hivyo wanahabari wanalojukumu la kutumia vizuri kalamu zao katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kushiriki kwa vitendo katika kuikataa na kufichua vitendo vya rushwa.

Aidha amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini,kadhalika,huduma za afya nchini zimeimarika kutokana na juhudi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita za kusimamia kwa karibu ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya na majengo katika hospitali za wilaya na za mikoa. 

”Serikali imeendelea kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi mpaka sekondari kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye uwezo wa kusoma anapata haki hiyo”amesema.

Hata hivyo amesema kuwa katika ngazi ya vyuo vya kati na vya elimu ya juu,Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji ili waweze kupata haki ya elimu katika ngazi hiyo ambapo Kwa ujumla, miradi mingi inayoendelea nchini, inalenga kuboresha maisha ya Mtanzania.

Ikumbukwe kuwa tafiti iliyofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania TAKUKURU ilibainisha Taasisi zinazoongoza kwa rushwa ni Polisi, Sekta ya Afya, Mahakama na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA‎.

By Jamhuri