Watu 30 wameripotiwa kufa baada ya tetemeko kubwa la ardhi kupiga pwani ya katikati mwa Japan siku ya mwaka mpya huku Waziri Mkuu Fumio Kishida akionya uwezekano wa majeruhi kuongezeka.

Tetemeko hilo la Richter 7.6 lilipiga eneo la Peninsula ya Noto katika Mkoa wa Ishikawa, na kusababisha uwezekano wa kutokea kwa tsunami tangu tetemeko la ardhi na tsunami lilipotokea Machi 2011 na kusababisha vifo vya watu 18,500 na wengine kupotea.

Akizungumza Jumanne, Kishida alisema “uharibifu mkubwa” umethibitishwa na tetemeko hilo kuangusha majengo na kusababisha moto.

Mamlaka ilisema juhudi za uokoaji zilitatizwa na barabara zilizoharibika na kwamba wanapata shida kutathmini kiwango kamili cha ajali hiyo.