Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Serikali inathamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Sekta za kidini katika kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi mjini na vijijini.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 2 Januari 2024 wakati alipotembelea Hospitali ya San Pio iliyopo wilayani Bukombe mkoani Geita akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella na viongozi wa Chama cha Mapinduzi. Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa 2000 kwa
mwaka.

Kwa kutambua mchango huo wa Sekta za Kidini, Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali ipo tayari muda wote kushirikiana nao ili kuendeleza yale wanayokusudia kuyafanya katika jamii.

Dkt. Biteko amepongeza uongozi na wafanyakazi wa Hospitali hiyo chini ya Mkurugenzi, Sista Teresa Goska, kwa kutoa huduma bora za kiafya kwa wananchi na pia uamuzi wao wa kuanza kutoa huduma katika Sekta ya Elimu ambapo wameanza na darasa la awali.

Akiwa katika Hospitali hiyo ya San Pio, Dkt. Biteko aliwafariji wagonjwa mbalimbali waliolazwa na wanaosubiri huduma pamoja na kukagua majengo na miundombinu ya kutolea huduma hospitalini hapo.

Uongozi wa Hospitali hiyo umemshukuru Dkt. Biteko kwa kutembelea hospitali hiyo ikionesha kuwa, anatambua na kuthamini huduma inayotolewa kwenye hospitali ya San Pio ambayo ipo chini ya Jimbo Katoliki la Kahama.

By Jamhuri